Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko akisalimiana na wazee pamoja na wagonjwa. Baba Mtakatifu Francisko akisalimiana na wazee pamoja na wagonjwa.  (Vatican Media)

Mama mgonjwa atembelewa na Papa Francisko nyumbani kwake!

Jumamosi, tarehe 28 Julai 2018, majira ya alasiri, Baba Mtakatifu Francisko alikwenda kumtembelea Mama mmoja mgonjwa aliyekuwa hawezi kitandani, ambaye, kwa muda mrefu alitamani sana kumwona Baba Mtakatifu kabla ya taa ya maisha yake haijazimika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko alijiwekea utaratibu wa Ijumaa ya Matendo ya huruma, muda ambao aliutumia kwa ajili ya kufanya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Jumamosi, tarehe 28 Julai 2018, majira ya alasiri, Baba Mtakatifu alikwenda kumtembelea Mama mmoja mgonjwa aliyekuwa hawezi kitandani, ambaye, kwa muda mrefu alitamani sana kumwona Baba Mtakatifu Francisko kabla ya taa ya maisha yake haijazima.

Baadhi ya watu waliotambua gari la Baba Mtakatifu Francisko waliamua kusubiri ili kuona hatima yake. Baba Mtakatifu alikuwa amezungukwa na askari wachache wa ulinzi na usalama. Baada ya kusalimiana na Mama huyu kwa muda wa saa moja, Baba Mtakatifu wakati akirejea kwenye gari tayari kuondoka, alikutana na umati mkubwa wa watu, ambao walitaka kusalimiana naye na kuomba baraka kutoka kwake. Baba Mtakatifu akawaonjesha furaha ya Injili na kuwapatia baraka zake za kitume.

Mgonjwa mmoja baada ya kuambiwa kwamba, Baba Mtakatifu alikuwa karibu na nyumbani kwake, aliamua kwenda kumsalimia na kuomba baraka zake za kitume na baadaye kuondoka na kurejea tena mjini Vatican. Wenyeji wa eneo hili la Mtaa wa Alessandria, mjini Roma, wamebaki wakiwa wamepigwa na bumbuwazi kwa kuona jinsi ambavyo, Baba Mtakatifu alivyojisadaka kwa ajili ya wazee na wagonjwa, kielelezo makini cha imani inayomwilishwa katika matendo. Karibu na eneo hili, karibu na Uwanja wa Buenos Aires kuna Kanisa kwa ajili ya waamini kutoka Argentina, wanaosali kwenye Kanisa la Bikira Maria, Mama wa matesi; mahali ambapo hata alipokuwa Kardinali alikua anakwenda kusali hapo mara kwa mara!

 

 

30 July 2018, 14:51