Tafuta

Vatican News
Mkutano wa 19 wa AMECEA, Addis Ababa, Ethiopia. Mkutano wa 19 wa AMECEA, Addis Ababa, Ethiopia. 

Ujumbe wa AMECEA kwa familia ya Mungu Afrika Mashariki na Kati, 2018

Mababa wa AMECEA amegusia umuhimu wa Kukuza na kudumisha tofauti msingi miongoni mwa familia ya Mungu kama utajiri, ili kusimama kidete kulinda utu, haki msingi za binadamu, umoja, haki na amani. Mababa wa AMECEA wameonesha mshikamano wa dhati na shukrani kwa Ethiopia na Eritrea ambazo kwa sasa zimeanza mchakato wa kujenga umoja, amani na maridhiano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, lililokuwa linaadhimisha mkutano wake mkuu wa 19 kuanzia tarehe 13 - 23 Julai 2018 huko Addis Ababa, nchini Ethiopia kwa kuongozwa na kauli mbiu “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA”, umemalizika kwa kuchagua viongozi watakaongoza jahazi kwa muda wa miaka minne kuanzia sasa pamoja na kutoa ujumbe kwa familia ya Mungu katika Ukanda wa AMECEA.

Mababa wa AMECEA amegusia mambo msingi ambayo yamejadiliwa na utekelezaji wake unapaswa kuanza mara moja kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki katika nchi husika: Kukuza na kudumisha tofauti msingi miongoni mwa familia ya Mungu kama utajiri, ili kusimama kidete kulinda utu, haki msingi za binadamu, umoja, haki na amani. Mababa wa AMECEA wameonesha pia mshikamano wao wa dhati na shukrani kwa Ethiopia na Eritrea ambazo kwa sasa zimeanza mchakato wa kujenga umoja, amani na maridhiano.

Mababa wa AMECEA katika ujumbe huu, wanapenda kutoa shukrani za dhati kwa mshikamano ulioneshwa na Baba Mtakatifu Francisko, Mabaraza ya Kipapa, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani pamoja na wadau mbali mbali wa maendeleo endelevu na fungamani kwa familia ya Mungu Afrika Mashariki na Kati. AMECEA imepania kujitosa kimasomaso kushughulikia changamoto za kichungaji na kijamii kwa ari na moyo mkuu. AMECEA inawashukuru watu wa Mungu kutoka Ethiopia, walioandaa maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 19 wa AMECEA bila kuwasahau viongozi waliomaliza muda wao.

Tofauti mtetemo kwa watu wote wa Mungu ni changamoto na mwaliko kwa watu wote kuhakikisha kwamba, wanakumbatia na kuambata tofauti hizi kama sehemu ya amana, utajiri na urithi unaowaunganisha na kamwe zisiwe ni chanzo cha mafarakano na mipasuko ya kijamii. Tofauti hizi zimo katika mpango wa Mungu anayetaka kila mtu apokee kile anachohitaji, kwa lengo la kushirikishana, kutajirishana na kukamilishana. Watu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wamekirimiwa akili na utashi; wana hali na asili moja na hivyo wana hadhi sawa! Mababa wa AMECEA wanaitaka familia ya Mungu kuwa ni shuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo na kamwe wasikubali kupekenyuliwa na ukabila wala tofauti msingi zinazojitokeza kati yao!

Hadhi sawa inafumbatwa katika usawa wa binadamu pamoja na haki jamii kama wanavyofafanua Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wamekombolewa kwa njia Fumbo la Pasaka. Haki na usawa ni mambo msingi katika kudumisha mafungamano ya kijamii. Lakini, Mababa wa Mtaguso wanakaza kusema, uwepo wa tofauti kubwa za kiuchumi na kijamii kati ya wanajamii na kati ya mataifa ya familia ya Mungu iliyo moja katika ubindamu ni kunasababisha taksiri, au kikwazo. Hali hii inapingana na  na haki jamii, usawa na hadhi ya binadamu pamoja na amani duniani.

Maendeleo endelevu na fungamani yanapaswa kujikita katika ustawi na mafao ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kuwezeshwa na taasisi za Jumuiya ya Kitaifa na Kimataifa, yalenge mafao ya wengi; kwa kuratibiwa na kusimamiwa na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Mababa wa AMECEA wanakaza kusema, wataendelea kusimama kidete kulinda na kutetea tofauti mtetemo, hadhi sawa, umoja wa amani na maendeleo fungamani katika Ukanda wa AMECEA. Kanisa litaendelea kujikita katika mchakato wa ujenzi wa amani, haki na usawa miongoni mwa familia ya Mungu pamoja na kusimamia maendeleo fungamani na haki msingi za binadamu.

Mshikamano na familia ya Mungu nchini Ethiopia na Eritrea umeshuhudiwa na Mababa wa AMECEA, kwa kuvunjilia mbali vikwazo vilivyowatenganisha wananchi wa pande hizi mbili, na hivyo kuanza mchakato wa majadiliano ya amani, umoja na mshikamano wa kidugu. Kanisa lina laani vita. Ni matumaini ya AMECEA kwamba, amani, mshikamano na umoja vitaendelea kudumishwa na nchi hizi mbili pamoja na kujikita katika upatanisho. Haki na amani virejeshwe na wahusika wote na kwamba, wananchi wapewe kipaumbele cha kwanza katika kumwilisha mchakato huu; sauti zao zisikike na mateka na wafungwa warejeshwe makao.

AMECEA inaitaka Sudan ya Kusini kuharakisha mchakato wa kutafuta suluhu ya amani, ili kuwaondolea watu mateso kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe na kwamba, AMECEA iko tayari kushiriki katika kutafuta suluhu ya kudumu. Waamini waendelee kusali kwa ajili ya kuombea amani Sudan ya Kusini.

Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinapaswa kulindwa, kudumishwa na kuendelezwa kwa kukumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Umaskini, kiwango kikubwa cha ukosefu wa fursa za ajira, pengo kubwa kati ya maskini na matajiri ni kati ya changamoto zinazoendelea kuzikumba familia nyingi, Afrika Mashariki na Kati. Malezi na majiundo ya awali na endelevu yataendelea kupewa kipaumbele cha pekee na AMECEA kwa kushirikiana na wadau mbali mbali ili kukuza na kudumisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa familia katika ngazi mbali mbali.

Mawasiliano katika ulimwengu wa digitali yaiwezeshe AMECEA kuendelea kushirikiana na kushikamana na wadau mbali mbali katika tasnia ya mawasiliano ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kanisa liendelee kuwekeza kikamilifu katika vyombo vya mawasiliano ya jamii kama sehemu ya uinjilishaji na maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Wadau wa tasnia ya habari wawajibike, waaminike na kuwa makini katika mawasiliano ya jamii. AMECEA itaendelea kujizatiti katika malezi, makuzi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya, kwa kukazia: imani, wito, mang’amuzi, maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu pamoja na elimu makini. Kanisa litaendelea kuzivalia njuga changamoto za maisha ya vijana kama vile: Ukosefu wa fursa za ajira, umoja katika amani, maendeleo ya uongozi, maongozi ya maisha ya kiroho pamoja na kuwasindikiza vijana kuweza kufanya maamuzi mazito katika maisha yao!

Ekolojia fungamani kama inavyofundishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Laudato si” yaani, “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ni mwaliko kwa familia ya Mungu katika Ukanda wa AMECEA kutambua na kuthamini kazi ya uumbaji. Watu wote wanaathirika na mabadiliko ya tabianchi, matumizi mabaya ya rasilimali na mali ya asili, umaskini pamoja na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Binadamu na mazingira ni sawa na chanda na pete. Uchoyo na ubinafsi ni hatari katika matumizi ya rasilimali za dunia. Uaminifu, ukweli na uwazi; majadiliano; mshikamano unaoongozwa na kanuni auni; mafao ya wengi; upendeleo kwa maskini na matumizi bora ya ardhi ni kati ya mambo yanayopaswa kuzingatiwa na wote.

AMECEA inaendelea kusema kwamba, itashirikiana na kushikamana na wadau mbali mbali wa maendeleo: kiroho na kimwili, kama vile SECAM, Jumuiya ya Umoja wa Afrika Mashariki na IGAD kwa ajili ya kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu pamoja na kuendelea kuwajengea uwezo Wabunge Wakatoliki katika Nchi za AMECEA ili waweze kutekeleza vyama nyajibu zao. Itaendelea kuimarisha mifumo ya usalama na hifadhi ya jamii kwa wakleri na watawa; kwa kukazia dhana ya kujitegemea kwa taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa.

Wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum ni matokeo ya watu kushindwa kuthamini na kudumisha: tofauti msingi, haki za binadamu pamoja na kujikita katika mchakato wa uchumi endelevu na fungamani. AMECEA itaendelea kujizatiti kuunga mkono jitihada za ulinzi na usalama kwa wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kushirikiana na wadau mbali mbali. Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na AMECEA; ziwe ni majukwaa ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu; mahali pa kuwafunda watu Mafundisho Jamii ya Kanisa; Majadiliano katika ukweli na uwazi.

Utu wa binadamu, maendeleo endelevu na fungamani; ekolojia fungamani, umoja katika amani; mila na desturi; suluhu ya migogoro kwa njia ya amani pamoja na utawala bora ni kati ya mambo ambayo yanapaswa kuingizwa katika mitaala ya chuo kikuu na taasisi za elimu ya juu katika Nchi za AMECEA. Viongozi wa taasisi mbali mbali wawe makini na kuwajibika barabara katika kuziendesha taasisi zao. Waendelee kushikamana na waamini walei katika karama na utawala bora katika taasisi hizi. Misimamo mikali ya kidini na vitendo vya kigaidi ni mambo ambayo yanahatarisha sana usalama na mafungamano ya kijamii kwa nchi za AMECEA.

Mihimili ya uinjilishaji inapaswa kuwa makini sana kwa makundi ya vijana wanaojihusisha na masuala haya. Lengo ni kuheshimu utu wa binadamu, haki msingi na kwamba, Kanisa litaendelea kushirikiana na Serikali mbali mbali ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini ili kudhibiti misimamo mikali ya kidini na kiimani. Ukweli, uwazi na uaminifu, viwe ni nguzo makini katika kupambana na saratani ya rushwa Afrika Mashariki ya Kati, kwa kujikita zaidi katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, malezi na majiundo makini. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa iendelezwe katika Nchi za AMECEA kama sehemu ya utekelezaji wa utume wa kinabii wa Kanisa, daima kwa kushirikiana na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Mababa wa AMECEA wanasema, Kanisa litaendelea kujizatiti katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya kila binadamu. Wana laani vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto wadogo na kwamba, wahusika wote wahakikishe kwamba, watoto wanalindwa na kujengewa mazingira bora zaidi katika malezi na makuzi yao. Idara za kichungaji ziwasaidie Maaskofu kuwa na sera makini za kuwalinda watoto. Uinjilishaji mpya ni mchakato unaopatia kuhakikisha kwamba, tofauti mtetemo, hadhi sawa, umoja wa amani na maendeleo endelevu na fungamani vinakuwa ni mambo msingi katika mchakato wa uinjilishaji mpya.

Lengo ni kujenga umoja na Mwenyezi Mungu; kwa kujikita katika utamadunisho pamoja na kuibua na kutumia mbinu mpya za uinjilishaji zinazotumia maendeleo ya sayansi na teknolojia ya kidigitali sanjari na ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Mababa wa AMECEA wanahitimisha ujumbe kwa watu wa Mungu kwa kusema kwamba, wanawakumbuka na kuwaombea na kwamba, wamewaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Mama wa Bara la Afrika.

Ujumbe wa Amecea

 

 

 

24 July 2018, 12:06