Vatican News
2018.06.27 Udienza Generale 2018.06.27 Udienza Generale  (Vatican Media)

Papa: Sakramenti ya Kipaimara ni zawadi ya ushuhuda na amani!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Sakramenti ya Kipaimara ni zawadi ya umoja wa Kanisa; upendo na mshikamano katika kutangaza, kushuhudia; kulinda na kutetea imani ya Kanisa. Ni zawadi inayowawezesha waamini kuwa alama ya upendo, mashuhuda na vyombo vya amani katika jamii inayowazunguka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican

Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara muungano wa wabatizwa na Kanisa hufanywa kuwa mkamilifu zaidi, kwani wanatajirishwa kwa nguvu ya pekee ya Roho Mtakatifu na hivi hulazimika kwa nguvu zaidi kuineza na kuitetea imani kwa maneno na matendo, kama mashuhuda wa kweli wa Kristo Yesu. Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara waamini wanampokea Roho Mtakatifu anayewawezeshwa kufanywa wana wa Mungu; kwa kuunganishwa zaidi na nguvu za Kristo pamoja na kupata mapaji ya Roho Mtakatifu na hivyo kuwasaidia kukamilika zaidi kama viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Kwa njia hii, waamini wanajitoa sadaka na kuwa ni zawadi kwa ajili ya jirani zao!

Waamini wanapopakwa mafuta ya Krisma wanapokea mhuri wa Paji la Roho Mtakatifu kutoka kwa Askofu mahalia: Huyu ni Roho wa hekima na akili; Roho wa shauri na nguvu; Roho wa elimu na ibada na ni Roho wa Uchaji Mtakatifu. Mapaji yote haya yanapaswa kukua na kuzaa matunda kwa ajili ya jirani zao. Haya ndiyo maisha ya Kikristo, anayewawezesha waamini kujisadaka kwa ajili ya jirani zao kwa kuondokana na ubinafsi; ili hatimaye, kufungua njia katika maisha ya jumuiya inayopokea na kutoa. Waamini wakumbuke kwamba, wao ni vyombo vya Roho Mtakatifu kwa ajili ya jirani zao.

Hii ni sehemu ya katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 6 Juni 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya mwendelezo wa tafakari kuhusu Sakramenti ya Kipaimara. Kwa njia ya Sakramenti hii, wabatizwa wanakamilishwa na hivyo kufanana na Kristo Yesu. Ni Sakramenti inayowaunganisha waamini kuwa viungo hai zaidi vya Fumbo la Mwili wake yaani Kanisa.

Utume wa Kanisa unapata asili na chimbuko lake kwa wale wote wanaofanyika kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Hakuna mtu awaye yote ndani ya Kanisa anayeweza kujigamba kwamba, Kanisa ni mali yake! Kila mwamini anao wajibu wa kusaidiana na waamini wenzake katika mchakato wa kutakatifuzana, kusaidiana na kutaabikiana. Kila mwamini anayo dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa, lakini wote kwa pamoja wanaunda Kanisa la Kristo linatoka kifua mbele ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara wote wamefungwa pamoja katika kifungo cha upendo kati ya waamini, Askofu mahalia pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mhudumu wa Sakramenti ya Kipaimara ni Askofu mahalia. Itakumbukwa kwamba, Maaskofu ni waandamizi wa Mitume; wao wamepokea utimilifu wa Sakramenti ya Daraja, kumbe, wanaendeleza utume wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu. Askofu kwa njia ya sala na kazi kwa ajili ya watu, anawamiminia  waamini ukamilifu wa utakatifu wa Kristo. Adhimisho la Sakramenti ya Kipaimara linapofanywa na Maaskofu huonesha wazi wazi matokeo ya kuwaunganisha wale wanaoipokea kwa undani zaidi na Kanisa, na vyanzo vyake vya kitume, na utume wake wa kumshuhudia Kristo! Busu la amani linalohitimisha madhehebu ya Sakramenti ya Kipaimara huonesha na kudhihirisha umoja wa Kanisa, Askofu mahalia pamoja na waamini wote.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara waamini wanapokea zawadi ya amani, wanayopaswa kuwashirikisha pia majirani zao; kwa kuendeleza Injili ya upendo na mshikamano, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu katika Kristo, huku wakitakiana mema! Wakristo wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya amani, umoja, mshikamano katika udugu. Sakramenti ya Kipaimara hutolewa mara moja tu na huchapa katika roho alama ya kiroho isiyofutika ambayo ni ishara kwamba, Kristo Yesu amemtia Mkristo alama ya mhuri wa Roho wake, kwa kumvika nguvu itokayo juu, ili aweze kuwa shuhuda wake kwa kutoa harufu nzuri ya utakatifu wa maisha unaobubujika kutoka katika tunu msingi za Kiinjili.

Waamini walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara wanapaswa kutambua kwamba, wanawajibika kuwasaidia jirani zao kukua na kukomaa katika maisha ya kiroho. Waamini wawe na ujasiri wa kutoka katika ubinafsi wao, tayari kukutana na jirani zao, ili kwa pamoja waweze kukua na kusaidiana katika kuziishi karama mbali mbali walizokirimiwa na Roho Mtakatifu, ili kuzaa matunda kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika Wakristo wote walioimarishwa kwa Roho Mtakatifu, kamwe wasimfungie Roho Mtakatifu katika ubinafsi wao; wasizime moto wa upendo uliowasha na Roho Mtakatifu, wala kuzuia upepo wa mageuzi unaovumishwa na Roho Mtakatifu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaombea waamini wote waimarishwe na Roho Mtakatifu ili waweze kuwa na ujasiri wa kitume ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa njia ya maneno na matendo yenye mvuto na mashiko! Waamini wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa amani inayojikita katika nyoyo ya watu!

 

 

06 June 2018, 09:14