Vatican News
2018.06.27 Udienza Generale Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kwa mahujaji, wageni na waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Amri za Mungu ni safari kuelekea uhuru kamili.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutekeleza Amri za Mungu wakiwa na moyo wa waana wa Mungu na kuachana na mwelekeo wa kutekeleza Amri hizi kwa woga na wasi wasi, kwani Amri za Mungu ni njia kuelekea uhuru kamili wa watoto wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S. -Vatican.

Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lolote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mwenyezi Mungu! Basi Bwana ndiye Roho, walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru! Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu kutoka katika Waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho 3: 5-6. 17; umekuwa ndio msingi wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoitoa Jumatano, tarehe 20 Juni 2018 kuhusu Amri za Mungu”. “Maneno kumi” ili kuishi Agano na Mwenyezi Mungu.

Kristo Yesu alikuja hapa duniani si kwa ajili ya kutangua Sheria bali kuzipatia utimilifu wake. Amri za Mungu zinalenga kuboresha mahusiano na mafungamano ya Agano kati ya Mungu na Taifa lake! Mwenyezi Mungu aliwapatia Waisraeli Amri Kumi kama sehemu muhimu sana ya masharti ya Agano. Baba Mtakatifu anakaza kusema, haya ni maneno ambayo yametamkwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe ni: Sheria na Amri zinazopaswa kufuatwa na taifa la Mungu. Mkazo hapa ni Neno ambaye anaumba, yaani Mwanaye mpendwa, Neno aliyefanyika mwili. Upendo unarutubishwa kwa njia ya neno kama ilivyo pia kwa ushirikiano wa dhati ili kujenga na kudumisha mawasiliano.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, pale mtu anapozungumza hadi kufikia hatua ya “kukuna sakafu ya moyo wa mtu, hapo kwa hakika upweke hutoweka! Mwenyezi Mungu kwa njia ya maneno kumi amependa kujenga mawasiliano na binadamu na sasa anasubiri majibu muafaka kutoka kwa waja wake. Ni mawasiliano yanayofumbatwa katika mchakato wa majadiliano. Ambao kimsingi ni chemchemi ya ukweli, furaha, upendo na utajiri ambao, wahusika wanatajirishana katika undani wao!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Shetani, Ibilisi aliwaadaa Adamu na Hawa, wakala matunda ya mti uliokatikati, wakafunguliwa macho na kujua mema na mabaya! Changamoto kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amempatia mwanadamu katika Amri zake, ili kumlinda na kumwongoza aweze kuishi Agano kwa uaminifu zaidi. Mwenyezi Mungu hana wivu wala kijicho, bali anawataka watoto wake wawe na uhuru kamili, kwa kusikiliza kwa makini maneno yake, kielelezo cha upendo wake usiokuwa na mipaka. Katika mazingira ya kutatanisha ili kutambua Amri za Mungu kuwa ni: Sheria, Neno au majadiliano waamini watambue kwamba yeye ni Baba mwenye upendo usiokuwa na kifani!

Baba Mtakatifu anaendelea kudadavua kwa kusema kwamba, mapambano yanayojionesha ndani na nje ya mtu mwenyewe ni mwaliko wa kufanya maamuzi sahihi kwa kuondokana na mawazo mgando kwamba, Mwenyezi Mungu anataka kuwagandamiza waja wake. Ikumbukwe kwamba, Amri inatolewa na wakuu wa dunia, lakini “Neno” linabubujika kutoka kwa Baba. Roho Mtakatifu ni Roho wa Mwana anayewawezesha waamini kupokea Amri za Mungu kwa kuzingatia haki na wajibu; mwelekeo wa pili ni kubeza Amri za Mungu kwa kuwa na mwelekeo wa kitumwa unaoharibu mahusiano na mafungano, kiasi hata cha kumtupilia mbali Mwenyezi Mungu katika maisha. Roho Mtakatifu ni mleta uzima katika maisha ya Kikristo. Ni Neno wa Baba wa milele na wala si hukumu ya Mwenyezi Mungu, ndiyo maana alikuja ulimwenguni ili kumwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya Neno lake. Huu ndio ushuhuda unaopaswa kutolewa na waamini katika hija ya maisha yao ya kila siku. Baba Mtakatifu anawaalika wakristo kufikiri na kutenda kama watoto wa Mungu na wala si kama watumwa!

Hali hii inajionesha hata katika malezi, ikiwa kama walezi wenyewe wametekeleza dhamana na wajibu wao vyema, au wamewatwisha wengine mzigo wa sheria. Amri Kumi za Mungu ni safari kuelekea kwenye uhuru kamili, kwani Neno la Mungu linawafanya kuwa huru kweli kweli!. Ulimwenguni unahitaji utawala wa sheria, lakini pia huduma; unawahitaji Wakristo wenye moyo wa waana na wala si moyo wa watumwa!

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa Katekesi yake kuhusu Amri za Mungu, amewakumbusha waamini kwamba, Mwezi Juni, Kanisa linaotolea kwa ajili ya Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Huu ni moyo unaobubujika huruma na mapendo, shule makini ya kupenda bila masharti; ni Moyo unaomwezesha mwamini kufanya maamuzi mazito katika maisha. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali na kumwombea katika maisha na utume wake, lakini bila kusahau kuwakumbuka na kuwaombea mapadre wote ili waendelee kujibidisha kuwa waaminifu kwa wito na maisha yao ya Kikasisi!

 

20 June 2018, 08:46