Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi, Jumatano tarehe 1 Agosti 2018 Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi, Jumatano tarehe 1 Agosti 2018  (Vatican Media)

Papa Francisko:Ondoeni miungu inayowazengua katika maisha

Waamini wanapaswa kutambua kwamba, Mungu aliye hai ni chanzo cha maisha ya uzima wa milele na ndiye anayepanga na kuratibu historia ya maisha ya mwanadamu. Ibada za miungu hazihusu tu ibada potofu za kipagani. Zinabaki kuwa kishawishi cha kudumu cha imani. Ibada za miungu ni kufanya mungu kile ambacho si Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Amri ya kwanza ya Mungu ina laani “dini ya kuabudu miungu mingi”. Inamtaka mwamini kusadiki Mungu mmoja wa kweli aliyejifunua kwa Taifa lake. Maandiko Matakatifu yanakataza kuhusu sanamu za fedha na dhahabu zinazowafanya watupu wale wanaoziabudu. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, Mungu aliye hai ni chanzo cha maisha ya uzima wa milele na ndiye anayepanga na kuratibu historia ya maisha ya mwanadamu. Ibada za  miungu hazihusu tu ibada potofu za kipagani. Zinabaki kuwa kishawishi cha kudumu cha imani. Ibada za miungu ni kufanya mungu kile ambacho si Mungu.

Hiki ni kishawishi kikuu kwa waamini na wale wasioamini. Mkristo anapaswa kujiuliza swali la msingi, Je, anaamini katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja? Maisha ya kibinadamu hupata umoja katika kumwabudu Mungu mmoja. Kuabudu miungu ni upotofu wa hali za ndani za hisi za dini za mtu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu Amri za Mungu, Jumatano, tarehe 1 Agosti 2018, amegusia kuabudu miungu mingi na kuifanya kuwa ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mtu, kwa kile anachofikiri na kutenda.

Hali hii inaweza kutendeka hata katika familia ya Kikristo kwa kuwa na mawazo potofu yanayosigana na kweli za Kiinjili. Kutokana na hali ya binadamu, ulimwengu unaendelea kuzalisha miungu inayowapagaisha watu. Baba Mtakatifu anatolea mfano wa kupiga bao, ili kufunua wakati ujao, kwa kusoma nyota na alama za viganja. Yote haya yanapingana na heshima, hadhi na uchaji na mapendo anayopaswa kupewa Mwenyezi Mungu peke yake. Kupiga bao anakaza kusema Baba Mtakatifu ni ibada ya kuabudu miungu inayoendelea kushamiri katika ulimwengu mamboleo.

Waamini wanahamasishwa kumwendea na kumkimbilia Mwenyezi Mungu aliye hai, anayewasikiliza na kuwakirimia kadiri ya huruma na upendo wake. Mwenyezi Mungu aliwakataza Waisraeli wasijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Aliwakataza kuvisujudia wala kuvitumikia, kwani vitu hivi vina mvuto sana, vina hatari ya kuwateka watu kama vile: magari ya fahari, simu za viganjani na mambo kama haya yanayotaka kukidhi utupu wa ndani, unaodhaniwa kuwa ni chemchemi ya furaha, lakini kwa bahati mbaya, mwanadamu anaendelea kubaki katika utupu wake bila kufanikiwa kufikia katika kilele cha mafanikio alichokuwa anatamani katika maisha!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, leo hii uchawi na imani za kishirikisha zinaendelea kushika kasi ya ajabu, kiasi hata cha wazazi kuwatoa watoto wao kafara ili kupata: utajiri, mali, cheo na mafanikio katika maisha. Baadhi ya watu wamezama katika ulimbwende na umaridadi, siku nzima wako mbele ya kioo kujiremba na kujipodoa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, umaarufu unawaponza watu kiasi cha kusadaka utu na heshima yao, wakati ambapo miungu inataka damu kama sehemu ya tambiko.

Miundo mbinu ya kiuchumi inawatoa kafara wafanyakazi kwa wafanyabiashara kujikita zaidi katika mchakato wa kutafuta faida kubwa zaidi kwa gharama ya maisha ya wafanyakazi, ndio maana leo hii, baadhi ya wafanya biashara wanadiriki kufunga viwanda vyao na kutafuta mahali ambapo wanaweza kupata faida kubwa, hali inayoleta wasi wasi na mashaka makuu kwa wafanyakazi sehemu mbali mbali za dunia. Wafanyabisahara kama hawa wanamwabudu mungu fedha. Kuna wengine ni maarufu kwa kupika majungu dhidi ya jirani zao bila kusahau kwamba, hata matumizi haramu ya dawa za kulevya yanageuka kwa ni miungu wadogo.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa tabia yake, miungu huwageuza watu kuwa watumwa, kiasi hata cha kuabudiwa na kutukuzwa na wahusika na matokeo yake, watu wengi wanaharibiwa na kuchanganyikwa kwa kubaki watupu pasi na matumaini. Huu ni mwaliko kwa waamini kumkimbilia na kumwendea Mwenyezi Mungu, aliyethubutu kumtoa Mwanaye wa pekee kuwa ni sadaka ya maondoleo ya dhambi na maisha ya uzima wa milele. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo anaongoza na kuratibu historia ya maisha ya mwanadamu!

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuchunguza dhamiri zao na kuangalia katika maisha yao, wanaabudu miungu gani? Kwa kutambua miungu wanayo abudu, huu ni mwanzo wa neema unaowaelekeza waamini kumtafuta Mungu kwa upendo ili kujenga na kudumisha urafiki wa dhati. Uchawi na imani za kishirikina ni chanzo cha maafa makubwa katika jamii, kwani ni mambo yanayoharibu umoja, upendo na mafungamano ya kijamii na kuwapofusha watu, kiasi cha kushindwa kuwa huru katika maamuzi na matendo yao.

Pale waamini watakapogundua miungu inayowazengua wawe tayari kuing’oa na kuitupilia mbali anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kuhitimisha katekesi yake kuhusu Amri za Mungu. Akitoa salam mbali mbali kwa mahujaji na wageni waliofika kwenye Ukumbi wa Paulo VI, amewataka kuchuchumilia tunu msingi za maisha ya Kiinjili, kwa kuendelea kupyaisha maisha yao kila siku.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

01 June 2018, 15:45