Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 2 Aprili 2020 ametolea Nia ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum sehemu mbali mbali za dunia! Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 2 Aprili 2020 ametolea Nia ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum sehemu mbali mbali za dunia!  (AFP or licensors)

Papa Francisko kuna maskini na wasio na makazi wanaoteseka!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mtakatifu Theresa wa Calcutta, kuamsha tena dhamiri nyofu, ili watu watambue umuhimu wa kujenga na kudumisha ujirani mwema, hasa katika kipindi hiki cha janga kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Ujirani mwema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Agano linatiwa muhuri kwa damu! Na kwa sababu hii ni mjumbe wa Agano Jipya, ili mauti ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya Agano la kwanza, hao walioitwa ili waipokee ahadi ya urithi wa milele! Haya ni maneno ya Antifona ya mwaliko, Liturujia ya Neno la Mungu, Alhamisi, Juma la V la Kipindi cha Kwaresima. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 2 Aprili 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican na kutolea nia ya Misa hiyo, kwa ajili ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum. Baba Mtakatifu anawaalika wale wote wanaoteseka kwa sababu mbali mbali, kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, kwani kwa hakika, awatasikiliza na kuwafariji. Kristo Yesu ni daraja kati ya Agano la Kale na Agano Jipya kwa sababu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake amemkirimia mwanadamu urithi wa milele.

Katika kipindi hiki kigumu cha historia ya maisha ya mwanadamu kutokana na maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19, matatizo mengi ya kijamii yaliyokuwa yamefunikwa chini yanaanza kujitokeza hadharani. Kuna maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum, wanateseka sana na wala hawana mahali pa kujipatia hifadhi na mahitaji ya msingi. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta, kuamsha tena dhamiri nyofu, ili watu watambue umuhimu wa kujenga na kudumisha ujirani mwema, hasa katika kipindi hiki cha janga kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amefafanua: Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Mwanzo: 17: 3-9 na Injili ya Yohane 8: 51-59. Mhusika mkuu katika Liturujia ya Neno la Mungu ni Abramu anayefunga Agano na Mwenyezi Mungu na kupewa jina la Ibrahim, kwa upande mwingine kuna Kristo Yesu, anayekuja kuweka Agano Jipya na la milele, kwa kuwasamehe watu dhambi zao. Wakristo wanapaswa kutambua kwamba, wameteuliwa na kupewa ahadi ambayo wanapaswa kuitekeleza mintarafu uaminifu wa Agano. Dhambi za binadamu mara nyingi zinatendeka katika mwelekeo huu kwa kuabudu miungu wa uwongo, kwa kushindwa kutumainia ahadi ya urithi wa milele pamoja na kusahau agano walilofunga na Mungu. Wakristo wanapaswa kutambua daima kwamba wameteuliwa na wanapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha inayowapatia nguvu ya kusonga mbele katika kutekeleza ahadi ya urithi wa milele, kwa kujikita katika uaminifu wanapotekeleza agano kati yao na Mwenyezi Mungu.

Mara baada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu ameongoza Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kwa kutambua uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika Sakramenti ya Altare. Waamini wanahamasishwa kuonesha upendo wao wa dhati na wawe tayari kumpokea na kumkaribisha Kristo Yesu katika undani wa maisha yao.

Papa: Maskini
02 April 2020, 12:21
Soma yote >