Tafuta

Vatican News
Papa Francisko amewakumbuka na kuwaombea wanahabari wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika mazingira hatarishi ya maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19. Papa Francisko amewakumbuka na kuwaombea wanahabari wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika mazingira hatarishi ya maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19. 

Papa Francisko awakumbuka na kuwaombea wanahabari duniani

Waandishi wa habari wamekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kufundisha, kuelimisha, kuburudisha na kuhabarisha mambo msingi yanayoendelea kujiri sehemu mbali mbali za dunia. Kwa hakika wamekuwa ni msaada mkubwa katika kipindi hiki ambacho watu wengi wamewekewa karantini na hawapaswi kutoka nje! Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea! Tumo hata sisi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wafanyakazi katika tasnia ya mawasiliano ya jamii ni kati ya watu ambao wako hatarini kuambukizwa ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumatano, tarehe 1 Aprili 2020 ametolea nia ya Ibada hii ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwaombea na kuwatia shime wafanyakazi katika tasnia ya mawasiliano ya jamii hasa katika kipindi hiki kigumu, ambacho watu wengi wamewekwa chini ya karantini kama sehemu ya mbinu mkakati wa kuzuia maambukuzi ya Virusi vya Corona. Waandishi wa habari wamekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kufundisha, kuelimisha, kuburudisha na kuhabarisha mambo msingi yanayoendelea kujiri sehemu mbali mbali za dunia. Kwa hakika wamekuwa ni msaada mkubwa katika kipindi hiki ambacho watu wengi wamewekewa karantini na hawapaswi kutoka nje!

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, wafuasi wa Kristo Yesu, wanapaswa kuwa huru, kwa kuzingatia Mapokeo na wawe tayari kukubali mchakato wa upyaisho katika maisha, kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza. Antifona ya mwaliko, Jumatano ya V ya Kipindi cha Kwaresima ni sehemu ya Zaburi ya 17: Sifa kwa Mungu mkuu: Mzaburi anatambua kwamba, Mwenyezi Mungu ni nguvu zake, jabali, boma na mwokozi wake ndiye anayestahili kusifiwa! Katika shida na mahangaiko yake, alimwita Bwana, akaisikia sauti yake! Hii ni changamoto kwa wafuasi wa Kristo Yesu kuendelea kubaki waaminifu katika neno lake, ili waweze kuifahamu kweli ambayo itawaweka huru.

Kristo Yesu katika mahojiano na Waandishi pamoja na Mafarisayo anajitahidi kuwaelewesha utambulisho wake, lakini kwa bahati mbaya, wanaishia kutoa matusi na kashfa. Kristo Yesu anawataka wafuasi wake, kubaki wakiwa wameungana naye na wala hakazii hata kidogo, wasome na kujifunza kwa bidii, lakini anawataka wabaki wakiwa wameungana naye katika maneno na maisha yake, kama kielelezo makini cha utambulisho wa mfuasi wa Kristo. Kukaa katika neno la Kristo Yesu, maana yake ni kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza kwa kuzingatia Mapokeo, sanjari na kuwa tayari kukubali mchakato wa upyaisho wa maisha, unaoendelea kumkomaza mtu katika ufuasi wake.

Wafuasi wa Yesu wanaweza kujadiliana katika ukweli na uwazi, kwa kutambua kwamba, wanapaswa kuongozwa na Roho Mtakatifu anayeishi na kutenda kazi ndani mwao, ikiwa kama watamwachia nafasi. Hiki ni kielelezo makini kwamba, wamepakwa mafuta na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ikumbukwe kwamba, utambuzi huu si rahisi sana kama ilivyokuwa hata kwa Waandishi na Mafarisayo. Wanafunzi wa Yesu wanapaswa kuufahamu ukweli huu kwa kichwa, lakini zaidi kwa kuuhifadhi katika sakafu ya nyoyo zao; hekima kutoka kwa Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu amehitimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, akawapatia waamini na watu wote wenye mapenzi mema Baraka ya Sakramenti kuu ya Ekaristi Takatifu. Hii imekuwa ni fursa ya kumwabudu, kumsifu na kumtukuza Yesu wa Ekaristi pamoja na kujiaminisha katika ulinzi na tunza yake.

Papa: Wanahabari
01 April 2020, 13:47
Soma yote >