Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amewaonya wale wote wanaotaka kujinufaisha kutokana na janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, kuacha mara moja! Baba Mtakatifu Francisko amewaonya wale wote wanaotaka kujinufaisha kutokana na janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, kuacha mara moja!  (AFP or licensors)

Papa Francisko aonya! Msitake kujinufaisha na janga la Corona!

Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa takatifu, amemwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia watu wake dhamiri safi na nyofu, katika ukweli na uwazi, ili waguswe na mahangaiko na mateso ya jirani zao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya huruma na mapendo. Baba Mtakatifu anawapongeza wale wanaowahudumia jirani zao kwa upendo mkamilifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waswahili wanasema, ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni! Katika kipindi hiki cha taharuki, wasi wasi na hofu ya wimbi kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 sehemu mbali mbali za duniani, kuna baadhi ya watu wameamua kutumia fursa hii kwa ajili ya kujitajirisha kwa mateso ya jirani zao. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumamosi, tarehe 4 Aprili 2020 amemwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia watu wake dhamiri safi na nyofu, katika ukweli na uwazi, ili waguswe na mahangaiko na mateso ya jirani zao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya huruma na mapendo. Baba Mtakatifu anawapongeza wale wanaowahudumia jirani zao kwa upendo mkamilifu

Huu ni wakati muafaka wa kushinda vishawishi vya uchu wa mali na faida ya haraka haraka, kwani, matendo haya madogo madogo yanapelekea watu kuanguka dhambi na hivyo kueneza madhara ya dhambi kwa watu wengine! Katika kipindi hiki cha mateso na mahangaiko makubwa ya watu sehemu mbali mbali za dunia, Baba Mtakatifu ameungana na Mzaburi kwa kusali ile Sala ya mateso na matumaini ya mwadilifu, ambayo Kristo Yesu aliitumia pia alipokuwa ametundikwa pale juu Msalabani: “Elì, Elì, lemà sabactàni? Yaani: “Mungu wangu, Mungu wangu mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, na maneno ya kuugua kwangu? Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu na wakati wa usiku lakini sipati raha.” Zab. 21: 1-2.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake ametafakari kwa kina kuhusu Injili ya Yohane: 11:45-56, ile sehemu inayosema, “Yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu”. Wakuu wa Makuhani na Mafarisayo waliitisha baraza na kukata shauri la kumuua Yesu. Hii inatokana na wivu wao baada ya kuona kwamba watu wengi katika Wayahudi walipoona jinsi alivyomfufua Lazaro, wakamwanini. Maamuzi haya machungu yalifikiwa baada ya mchakato uliofanyika taratibu, kama ilivyo safari ya kishawishi inayomvuta na hatimaye, kumtumbukiza mwamini katika dhambi na baadaye, anatumia kila mbinu kutaka kuhalalisha matendo haya maovu! Nyuma ya maovu yote haya yupo Shetani, Ibilisi anayetaka “kujitangazia ushindi dhidi ya Kristo Yesu”.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuomba neema na baraka kutoka kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia kutambua udhaifu wao wa ndani, tayari kukimbilia toba na wongofu wa ndani, ili kuanza maisha mapya yanayowawezesha waamini kutembea katika mwanga wa Kristo! Mwishoni wa Ibada ya Misa takatifu, Baba Mtakatifu amewaongoza waamini na watu wote wenye mapenzi mema ambao wamekua wakifuatilia Ibada ya Misa Takatifi inayorushwa moja kwa moja kutoka kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa kitambo kifupi na hatimaye, akawapatia baraka kuu ya Ekaristi Takatifu.

Papa: Mateso ya mtu mwadilifu

 

04 April 2020, 13:55
Soma yote >