Papa Francisko katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Marko Mwinjili amekazia umuhimu wa waamini kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Papa Francisko katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Marko Mwinjili amekazia umuhimu wa waamini kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko! 

Baba Mtakatifu Francisko: Sikukuu ya Marko Mwinjili: Ushuhuda!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 25, Aprili, amewakumbuka na kuwaombea wafanyakazi wote wanaoshughulikia mazishi ya watu walioaga dunia na kutangulia mbele ya haki! Hii ni kazi nyeti, inayobeba huzuni na uchungu mkubwa na hawa ni kati ya watu wanaoweza kuambukizwa kwa urahisi zaidi ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Aprili, anaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Marko, Mwinjili. Huyu alikuwa ni binamu yake Mtakatifu Barnaba, Mtume. Katika hija ya maisha yake, alifuatana sana na Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa katika safari yake ya kwanza ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Historia inaonesha kwamba, baadaye alifuatana na Mtume Paulo katika safari yake hadi Roma. Alikuwa ni mwanafunzi wa Mtakatifu Petro, Mtume. Akajibidiisha kuandika mafundisho ya Mtakatifu Petro katika Injili yake. Kimsingi Injili ya Marko ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Petro, Mtume! Injili ya Marko inafikia kilele chake katika Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Utukufu wa Kristo unajionesha katika Fumbo la Ufufuko wake! Kiri ya imani ya yule akida aliyesema “Hakika mtu huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu” Mk. 15:39, kwa Mwinjili Mark, hiki kipeo cha hali ya juu kabisa cha Injili yake!

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Marko, Mwinjili, Jumamosi, tarehe 25 Aprili 2020 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, amewakumbuka na kuwaombea wafanyakazi wote wanaoshughulikia mazishi ya watu walioaga dunia na kutangulia mbele ya haki! Hii ni kazi nyeti, inayobeba huzuni na uchungu mkubwa na hawa ni kati ya watu wanaoweza kuambukizwa kwa urahisi zaidi ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko yamechota utajiri wake kutoka katika Liturujia ya Neno la Mungu, Somo la kwanza kutoka katika Waraka wa Kwanza wa Mtume Petro kwa Watu wote Sura 5: 5-14 na Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Marko, Sura ya 16: 15-20 inayomwonesha Kristo Mfufuka akiwatokea wafuasi wake na kuwaagiza kwenda Ulimwenguni kote kuhubiri Injili kwa kila kiumbe, aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Baba Mtakatifu anasema, Injili ya Marko ilikuwa ni ya kwanza kuandikwa ili kusimulia maisha na utume wa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, aliyejifunua kwa Mitume wake. Kwa muda wa miaka mitatu, Kristo Yesu alitekeleza utume wake katika maisha ya hadhara.

Baada ya mateso, kifo na ufufuko wake, akawatokea Mitume wake na kuwapatia Amri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Injili ya Kristo ni chemchemi ya ukuaji wa imani inayopaswa kutangazwa, kushuhudiwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji. Baba Mtakatifu anaitaka Mihimili ya Uinjilishaji kuwa kweli ni mashuhuda wa Kanisa la Kimisionari kama utambulisho wao katika ulimwengu mamboleo. Ushuhuda wa kimisionari uiwezeshe Mihimili ya Uinjilishaji kutoka katika ubinafsi wao, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Katika muktadha huu, hakuna wongofu wa shuruti hata kidogo, bali watu wanavutwa kumfuasa Kristo kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko anasema Baba Mtakatifu Francisko. Wakristo wafikiri, watende na kusema kama wafuasi wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Ushuhuda wa maisha ya Kikristo hauna budi kusimikwa katika unyenyekevu, uthabiti katika imani na huduma kwa kuondokana na kiburi kwa sababu Mwenyezi Mungu huwapa wanyenyekevu neema. Wawe ni watu wa kiasi na wanaokesha daima kwani mshitaki wao Ibilisi, kama Simba angurumaye, huzungukazunguka akitafuta mtu ammeze. Imani thabiti ndiyo silaha ya kupambana na Shetani, Ibilisi. Katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, watambue kwamba, daima Kristo Mfufuka yuko pamoja nao! Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mwenyezi Mungu ili awawezeshe kuwa ni mashuhuda amini wa imani wanayoitangaza na kuimwilisha katika matendo, ili watu wengi zaidi, waweze kupokea na kuambata zawadi ya ukombozi!

Papa: Mwinjili Marko

 

25 April 2020, 13:37
Soma yote >