Baba Mtakatifu Francisko anawataka viongozi wa Kanisa kuwa karibu na kati ya watu wa Mungu kwa ajili ya kuwapatia huduma makini kama alivyofanya Kristo Yesu, Mchungaji mwema! Baba Mtakatifu Francisko anawataka viongozi wa Kanisa kuwa karibu na kati ya watu wa Mungu kwa ajili ya kuwapatia huduma makini kama alivyofanya Kristo Yesu, Mchungaji mwema! 

Papa Francisko: Viongozi kuweni karibu na watu kwa huduma makini

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchungaji mwema ni chachu ya maendeleo ya watu wa Mungu: kiroho na kimwili! Ni kielelezo cha ukarimu na upendo wenye mvuto unaofyekelea mbali “ndago” za uchoyo na ubinafsi na hatimaye, kugeuka kuwa ni mashuhuda na vyombo vya faraja na huruma ya Mungu kwa njia ya sala inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO limezindua mpango mkakati wa elimu wa kimataifa ili kuhakikisha wanafunzi walio nje ya shule kutokana na mlipuko wa ugonjwa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 wanasoma kupitia maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii. Zaidi ya wanafunzi bilioni 1.4 kutoka shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu sehemu mbali mbali za dunia, wameshindwa kuhudhuria masomo kutokana na Janga la Virusi vya Corona, COVID-19. UNESCO imeamua kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kwamba wanafunzi hawa wanapata elimu kwa njia mbalimbali ikiwemo kutumia teknolojia ya mawasiliano ya jamii.

Kuna hatari kubwa kwamba, wanafunzi kutoka katika familia maskini zaidi duniani wakashindwa kupata huduma hii na hivyo kujikuta wakisuasua katika masomo! UNESCO inasema, ukubwa wa changamoto hii unahitaji ubunifu, ushirikiano, na mshikamano, ili kuweza kuchukua hatua haraka na kufanyakazi kama wamoja. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Ijumaa tarehe 24 Aprili 2020 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican ametolea nia ya Misa kwa ajili ya wanafunzi pamoja na walimu wao, ambao wamelazimika kusitisha masomo na kuacha kwenda shuleni kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu amefafanua kwa kina na mapana Liturujia ya Neno la Mungu, Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume Sura ya 5:34-42 na Injili kama ilivyoandikwa na Yohane, 6:1-15.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amekita tafakari yake kwenye Injili ya Siku jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyowashibisha mkutano mkuu kwa Mikate mitano na Samaki wawili, baada ya kumjaribu Filipo kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. Hii ilikuwa ni nafasi nyingine tena ya kuweza kuwafunda wanafunzi wake, ili hatimaye, waweze kukua na kukomaa kama wachungaji wa watu wa Mungu. Kristo Yesu alipenda kuwa kati pamoja na watu, kama alama ya wokovu wa watu wote! Hii ndiyo sababu watu kutoka sehemu mbali mbali walikwenda kumsikiliza. Wakati wakiwa faragha, wanafunzi walichukizwa kuona umati mkubwa wa watu ukimfuata na Kristo Yesu akaaanza kuwafundisha na wao wakamsikiliza kwa umakini mkubwa.

Hizi ni jitihada za Kristo Yesu kuwafunda Mitume wake, ili waweze kuwa karibu na watu wa Mungu, ili kuwahudumia. Si haba kuona katika Maandiko Matakatifu, wanafunzi wa Yesu wakiwakataza watoto kumkaribia Yesu au kama ilivyokuwa kwa yule Kipofu wa Yeriko. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchungaji mwema ni chachu ya maendeleo ya watu wa Mungu: kiroho na kimwili! Ni kielelezo cha ukarimu na upendo wenye mvuto unaofyekelea mbali “ndago” za uchoyo na ubinafsi na hatimaye, kugeuka kuwa ni mashuhuda na vyombo vya faraja na huruma ya Mungu kwa njia ya sala inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Na katika mazingira haya, kwa kuwalisha umati wa watu kwa Mikate mitano na Samaki wawili. Watu kwa kuona ishara aliyoifanya wakataka kumshika Yesu ili wamfanye Mfalme, akajitenga, akaenda tena mlimani.

Baba Mtakatifu anasema, hiki ni kishawishi kikubwa, kinachoweza kumwangusha mchungaji na hatimaye, kumezwa na malimwengu. Kwa Kristo Yesu, uongozi ni huduma makini kwa ajili ya watu wa Mungu, inayomwezesha mchungaji kujisadaka bila ya kujibakiza hata kidogo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwakumbuka na kuwaombea viongozi wao wa kiroho, ili waweze kujiweka katika mazingira ya kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini mkubwa, huku wakitambua kwamba, kwa hakika anawapenda upeo! Wawe wasikivu ili kutambua mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wao; kwa kuwaendea na kuwa karibu zaidi na watu wa Mungu! Mara baada ya adhimisho la Misa takatifu, Baba Mtakatifu amewaongoza waamini katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, akawapatia Baraka Kuu ya Ekaristi Takatifu. Mwishoni, wote kwa pamoja wamesali, Sala ya Malkia wa Mbingu!

SALA YA MALKIA WA MBINGU

Malkia wa mbingu, furahi, aleluya.

Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya.

Amefufuka alivyosema, Aleluya. Utuombee kwa Mungu, Aleluya.

Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Alaluya.

Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya.

TUOMBE. Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristu, Mwanao: fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.

Sala hii kwa Lugha ya Kilatin

Regína caeli laetáre, allelúia.

Quia quem merúisti portáre, allelúia.

Resurréxit, sicut dixit, allelúia.

Ora pro nobis Deum, allelúia.

Oremus: Deus, qui per resurrectionem Filii tui Domini nostri Iesu Christi mundum laetificare dignatus es, praesta, quaesumus, ut per eius Genetricem Virginem Mariam perpetuae capiamus gaudia vitae. Per eundem Christum Dominum nostrum. Amen.

Papa: Shule

 

24 April 2020, 13:41
Soma yote >