Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko asema, michezo ya kamari ni upatu ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na familia nyingi ambazo kwa sasa zimeathirika na COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko asema, michezo ya kamari ni upatu ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na familia nyingi ambazo kwa sasa zimeathirika na COVID-19.  (ANSA)

Papa Francisko: Michezo ya kamari na upatu ni hatari kwa familia!

Baba Mtakatifu Francisko amewaombea wale wote wanaojihusisha katika michezo hii ambayo ni janga kubwa kwa familia nyingi duniani, Mwenyezi Mungu aguse mioyo yao, ili waweze kutubu na kumwongokea. Katika shida na mahangaiko ya familia nyingi sehemu mbali mbali za dunia, Mwenyezi Mungu aweze kuzitegemeza ili zidumu katika utu na haki zake msingi. Upatu ni hatari sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Michezo ya kamari na upatu ni donda ndugu linaloendelea kusababisha maafa na majanga makubwa katika maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Mchezo wa kamari na upatu ni matokeo ya myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa. Kamari ni dhambi kubwa inayopukutisha maisha ya watu na kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na hivyo kuwa ni chachu ya rushwa, ufisadi na kizingiti katika ustawi, maendeleo fungamani na mafao ya wengi. Kutokana na athari kubwa za Janga la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, familia nyingi zimejikuta zikitumbukizwa humo na sasa hali inazidi kuwa tete zaidi! Kuna watu wanaotaka kuneemeka kutokana na shida na mahangaiko ya jirani zao!

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Alhamisi, tarehe 23 Aprili 2020 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican ametolea nia ya Misa hii kwa ajili ya familia ambazo zinajikuta katika wakati mgumu kutokana na athari za michezo ya kamari na upatu! Watu wengi wameathirika kutokana na ukosefu wa fursa za ajira; wanashindwa kutoka ndani ili kuzitafutia familia zao chakula cha kila siku. Hizi ni familia ambazo zinakumbana na baa la njaa na umaskini, lakini kwa bahati mbaya, kuna watu wanaotaka kuendelea kuzinyonya kwa kuzipigisha “kwata ya michezo ya kamari na upatu”. Baba Mtakatifu amewaombea wale wote wanaojihusisha katika michezo hii ambayo ni janga kubwa kwa familia nyingi duniani, Mwenyezi Mungu aguse mioyo yao, ili waweze kutubu na kumwongokea. Katika shida na mahangaiko ya familia nyingi sehemu mbali mbali za dunia, Mwenyezi Mungu aweze kuzitegemeza ili zidumu katika utu, heshima na haki zake msingi.

Liturujia ya Neno la Mungu ni kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume Sura 5:27-33 na Injili kama ilivyoandikwa na Mwinjili Yohane, 3:31-36. Hii ni sehemu ya Injili inayomhusu Kristo Yesu aliyetumwa na Mwenyezi Mungu ili kuyanena ya Mungu. Baba amempenda Mwana, naye amempa vyote mikononi mwake. Na amwaminiye Mwana ana uzima wa milele! Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekaza kusema, Kristo Yesu Mfufuka yuko mbele ya Baba yake wa milele akiwaombea waja wake, kwa kuonesha Madonda yake Matakatifu, thamani ya wokovu wa binadamu. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa na imani, matumaini na mapendo katika Sala ya Kristo Yesu inayokita mizizi yake katika madonda ya mwanadamu!

Baba Mtakatifu anasema, Somo la kwanza ni mwendelezo wa dhuluma ya Mitume kufungwa na kufunguliwa. Mitume Petro na Yohane wakiwa mbele ya Kuhani Mkuu na baraza lake wakajibu bila woga wala makunyanzi kwamba, imewapasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa ndiye aliyefufuliwa na ametukuzwa na Mwenyezi Mungu mkono wake wa kuume, ili awe Mkuu na Mwokozi, kwa ajili ya toba na msamaha wa dhambi. Mtume Petro anashuhudia Fumbo la Ufufuko kwa ujasiri na moyo mkuu! Lakini, Baba Mtakatifu anasema, huyu ndiye yule Petro aliyemkana Kristo Yesu mara tatu? Tena alikuwa ni mvuvi na sasa amepata wapi ujasiri huu? Mwishoni wanaungama kwa kusema kwamba, wao ni mashuhuda wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mwenyezi Mungu amewapa wote wamtiio!

Mitume walisimamia ukweli wa Fumbo la Ufufuko wa Kristo bila hata ya kupepesa pepesa macho! Huu ndio ukweli na msimamo wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa wokovu wa watu wa Mungu. Mtume Petro ni mtu aliyekuwa na imani, upendo na matumaini thabiti kwa Kristo Yesu. Lakini pia alielemewa na udhaifu na matamanio ya kibinadamu. Kristo Yesu akamwombea neema na baraka; akaweza kupata nguvu ya kusimama kidete kutangaza na kushuhudia: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Kabla ya mateso yake, Kristo Yesu alikuwa amemwahidia Petro kwamba, atamwombea ili imani yake isitindike hata kidogo! Ili baada ya kuimarika katika imani, aweze kuwaimarisha pia ndugu zake katika Kristo Yesu.

Kwa hakika, Kristo Yesu anasali mbele ya Mwenyezi Mungu ili kuwaombea waja wake. Ukweli, ujasiri na ushuhuda wa Mtume Petro ni kazi ya Roho Mtakatifu. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Kristo Yesu neema na baraka, ili aweze kuwaombea kama alivyofanya kwa kumwombea Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu amehitimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, kuwapatia waamini Baraka Kuu ya Ekaristi Takatifu.

Papa: kamari na Upatu

 

 

23 April 2020, 14:02
Soma yote >