Tafuta

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina ili hatimaye, waweze kugundua njia mpya za kumwilisha huruma na upendo katika uhalisia wa maisha yao; kwa kujenga amani, upendo na utulivu wa dhati ndani ya familia katika kipindi hiki kigumu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina ili hatimaye, waweze kugundua njia mpya za kumwilisha huruma na upendo katika uhalisia wa maisha yao; kwa kujenga amani, upendo na utulivu wa dhati ndani ya familia katika kipindi hiki kigumu.   (ANSA)

Virusi vya Corona: Familia jengeni mshikamano wa huruma na upendo!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina ili hatimaye, waweze kugundua njia mpya za kumwilisha huruma na upendo katika uhalisia wa maisha yao; kwa kujenga amani, upendo na utulivu wa dhati ndani ya familia katika kipindi hiki kigumu cha mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona, COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 yanazidi kutishia usalama na maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Watu wengi kwa sasa wamewekwa chini ya karantini kama sehemu ya mchakato wa kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huu. Katika muktadha huu, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanapaswa kufanya toba na wongofu wa ndani; kwa kubadili pia mitazamo na vipaumbele vya maisha yao, tayari kumkaribisha Mwenyezi Mungu katika hali ya unyenyekevu, upole na kiasi na wala hakuna sababu ya “kujimwambafai” kusikokuwa na mvuto wala mashiko! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 16 Machi 2020 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, kama sehemu ya mbinu mkakati wa kichungaji kutoka kwa Baba Mtakatifu na kama kielelezo cha mshikamano na familia mbali mbali zinazoteseka kutokana na athari za Virusi vya Corona, COVID-19.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya familia ambazo zimewekwa chini ya karantini pamoja na watoto ambao hawawezi tena kwenda shuleni kwa hofu ya kuambukizwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Katika hali na mazingira kama haya, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina ili hatimaye, waweze kugundua njia mpya za kumwilisha huruma na upendo katika uhalisia wa maisha yao; kwa kujenga amani, upendo na utulivu wa dhati ndani ya familia katika kipindi hiki kigumu. Ni fursa muhimu ya kujielekeza katika kipaji cha ubunifu katika maisha na utume wa familia, ili hata katika shida na magumu ya maisha, familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa: uzuri, ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia.

Baba Mtakatifu anasema, Liturujia ya Neno la Mungu inaonesha jinsi Kristo Yesu alivyokuwa na mvuto kwa wasikilizaji wake na kutukuzwa na wengi, lakini kwa bahati mbaya hakuweza kupata mafanikio makubwa mjini Nazareti, kutokana na dharau kwa wale waliodhani wanamfahamu sana Yesu. Wakadiriki hata kusema, “Huyu siye mwana wa Yusufu?” Je, ameipata wapi hekima yote hii? Amepata Shahada kutoka Chuo gani maarufu? Wakajaa ghadhabu na kutaka kumfundisha adabu, wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata katika Somo la kwanza linalomwonesha Naamani, jemedari wa Mfame wa Shamu, aliyeponywa ukoma lakini baada ya kujinyenyekesha mbele ya Mungu. Alikuwa ni jemedari aliye bahatika kuwa na imani, lakini alikosa unyenyekevu pale alipoambiwa na Nabii Elisha kwenda kuoga katika Mto Yordani mara saba naye angekuwa safi! Lakini, akageuka akaondoka kwa hasira.

Kama ilivyokuwa kwa Naamani jemedari wa Mfalme wa Shamu na kwa wananchi wa Nazareti, walidhani kwamba, Mwenyezi Mungu anajifunua kwa kuonesha mambo ya ajabu na yenye kutisha. Hawakufikiria kwamba, Mwenyezi Mungu angeweza kujifunua katika mambo ya kawaida katika maisha yao, katika hali ya kawaida. Matokeo yake ni kumkasirikia Mwenyezi Mungu. Ni watu waliokuwa wamemezwa na malimwengu, walitaka kuuona utukufu wa Mungu kwa mwonekano wa nje. Nazareti walishikwa na hasira kali, naye Naaman akaondoka kwa hasira, lakini watumishi wake wakamsihi na hatimaye, akakubali ushauri wao na kuoga mara saba katika Mto Yordani, sawa sawa na neno la Nabii Elisha. Akashusha kiburi na kuanza kujivika moyo wa unyenyekevu. Kama ilivyokuwa kwa Mafarisayo, walijikwaa na kuanguka kutokana na unyenyekevu wa Mungu. Mungu anawapenda wanyenyekevu, wanyofu wa moyo na maskini. Anawathamini watu wasiokuwa na makuu katika maisha yao! Chuki na hasira ni chanzo cha misigano na machafuko yanayopelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza na kuthamini unyenyekevu wa Mungu katika maisha yao!

Papa: Ibada ya Misa Takatifu
16 March 2020, 14:46
Soma yote >