Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 17 Machi 2020 amesali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wazee ambao ni pweke na wanaogopa kwa sababu wameachwa pweke-Virusi vya Corona. Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 17 Machi 2020 amesali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wazee ambao ni pweke na wanaogopa kwa sababu wameachwa pweke-Virusi vya Corona. 

Papa awakumbuka na kuwaombea wazee walioathirika na Corona!

Wazee watambue kwamba, Mwenyezi Mungu yuko daima pamoja nao. Katika hali hii, tete, wazee wengi wametekelezwa na ndugu zao. Baba Mtakatifu anawaalika wazee hawa kuwasemehe wote hawa kutoka katika undani wa mioyo yao! Mwenyezi Mungu amewakirimia hekima, maisha na historia na kwamba, Kanisa liko karibu nao kwa njia ya sala. Amekazia pia umuhimu wa kusamehe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sala na sadaka ya wazee ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwani zinalitegemeza Kanisa: Hii ni changamoto na mwaliko kwa wazee kuhakikisha kwamba, wanakuwa karibu na vijana ili kuwarithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Wazee waendeleze majadiliano na watoto wadogo pamoja na vijana wa kizazi kipya kwani katika maisha yao, wamebahatika kuwa na kumbu kumbu, ujuzi, maarifa na imani, mambo ambayo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya na kamwe wasijisikie kuwa ni watu waliopitwa na wakati. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 17 Machi 2020 amewakumbuka na kuwaombea wazee ambao wanaishi katika hali ya upweke na wamekumbwa na woga kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19.

Wazee watambue kwamba, Mwenyezi Mungu yuko daima pamoja nao. Katika hali hii, tete, wazee wengi wametekelezwa na watoto pamoja na ndugu zao. Baba Mtakatifu anawaalika wazee hawa kuwasemehe wote hawa kutoka katika undani wa mioyo yao! Mwenyezi Mungu amewakirimia hekima, maisha na historia na kwamba, Kanisa liko karibu nao kwa njia ya sala. Baba Takatifu katika mahubiri yake amezungumzia kuhusu umuhimu wa kusamehe daima, jambo ambalo si kawaida katika maisha ya binadamu. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna watu ambao wana tabia ya kuwahukumu wenzao, lakini Mwenyezi Mungu anawataka waja wake kujenga utamaduni wa kusamehe kutoka katika sakafu ya mioyo na hatimaye, kusahau. Umoja, udugu na mshikamano kati ya ndugu ni katekesi ambayo Kristo Yesu aliitoa kwa wanafunzi wake.

Umoja huu utakuwa ni chemchemi inayobubujikia: urafiki  na amani; ndoana ya wema wa Mungu. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kusamehe, ili kuondokana na tabia ya kutaka kulipiza kisasi, ubinafsi na uchoyo ambao umekita mizizi yake katika undani wa maisha ya mwanadamu. Chuki na uhasama ni chanzo kikuu kinacho sambaratisha familia nyingi duniani kutokana na tabia ya kutaka kulipiza kisasi hata kwa makosa yaliyotendwa na kizazi kingine. Kwa bahati mbaya chuki inachukua nafasi ya huruma na upendo na matokeo yake ni majanga makubwa katika maisha ya mwanadamu. Mwenyezi Mungu anasherehekea pale mdhambi mmoja anapotubu na kumwongokea, na kuanza kuambata utakatifu wa maisha.

Mwenyezi Mungu anasamehe na kusahau yote yaliyopita, changamoto na mwaliko kwa waamini nao kujenga utamaduni wa kusamehe na kusahau. Kuna watu ambao kutoka katika undani wa mioyo wao, hawana hata chembe kidogo ya kutaka kusamehe, ni watu wanaotaka kulipiza kisasi. Baba Mtakatifu anawataka watu wanao chafua majina ya jirani zao, wafanyakazi wenzao na hata ndugu zao wenyewe wajifunze kusamehe kama kielelezo cha kupandikiza mbegu ya Injili ya upendo. Waamini wanapokwenda kujipatanisha na Mungu, wasikie ndani mwao umuhimu wa kujipatanisha na jirani pamoja na ndugu zao. Baba Mtakatifu amehitimisha mahubiri yake kwa maneno ya Kristo Yesu anayesema kwamba, watu wasipowasamehe ndugu zao kutoka katika undani wa miyo yao, hata Baba yake wa mbinguni hatawasamehe kamwe!

Papa: Wazee
17 March 2020, 14:52
Soma yote >