Baba Mtakatifu Francisko ametolea nia ya Misa Takatifu kwa ajili ya watu wasiokuwa na makazi, wakati huu watu wengi wanapolazimishwa kubaki majumbani mwao ili kupambana na Virusi vya Corona. Baba Mtakatifu Francisko ametolea nia ya Misa Takatifu kwa ajili ya watu wasiokuwa na makazi, wakati huu watu wengi wanapolazimishwa kubaki majumbani mwao ili kupambana na Virusi vya Corona. 

Virusi vya Corona: Papa Francisko awaombea wasiokuwa na makazi!

Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 31 Machi 2020 ametolea nia ya Ibada ya Misa kwa watu wasiokuwa na makazi maalum, katika kipindi hiki ambacho watu wanashauriwa kubaki majumbani mwao kama sehemu ya mbinu mkakati wa kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu, maarufu kama Corona.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, watu wa Mungu katika shida na mahangaiko yao ya ndani, watambue kwamba, Mwenyezi Mungu anafanya hija ya maisha, akiwa anaandamana nao kwa njia ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu. Katika hali na mazingira kama haya, wajitahidi kuona na kuguswa na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu. Pale juu Msalabani, Kristo Yesu, ametundika mateso na mahangaiko ya binadamu wote. Akiwa ametundikwa Msalabani, watu wengi walimdhihaki, wakamtukana na kumdhalilisha; wakamchoma mkuki ubavuni, na hatimaye, akafa kifo cha aibu pale Msalabani. Kristo Yesu katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu, isipokuwa hakutenda dhambi. Katika shida na mahangaiko ya binadamu, Kristo Yesu, aliweza kuhuzunika, akatoa machozi, akawa faraja na chombo cha baraka kwa wale waliokuwa wanamzunguka.

Katika shida na magumu ya maisha, waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, wawe wepesi kumkimbilia na kumwangalia Kristo Yesu aliyetundikwa Msalabani, ili kujiaminisha na kujikabidhi katika ulinzi na tunza yake. Kristo Yesu ni jibu makini katika mateso na mahangaiko ya binadamu. Ikumbukwe kwamba, pale mlimani Kalvari, Yesu alipokuwa ametundikwa Msalabani, chini ya Msalaba, alikuwepo Mama yake mpendwa, Bikira Maria. Akajionea na kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya Mwanaye mpenzi, Kristo Yesu. Hata katika shida na mahangaiko ya waamini, wakumbuke kwamba, huko mbinguni, wanaye Mama na Mwombezi; anayewangalia kwa jicho la huruma na mapendo; anayewaombea mbele ya Mwanaye Mpendwa.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 31 Machi 2020 ametolea nia ya Ibada ya Misa Takatifu kwa watu wasiokuwa na makazi maalum, katika kipindi hiki ambacho watu wanashauriwa kubaki majumbani mwao kama sehemu ya mbinu mkakati wa kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu amewapatia matumaini wale wote wanaoteseka kwa wakati huu kwa kutumia maneno ya Mzaburi: “Umngoje Bwana, uwe hodari, upige moyo konde, naam, umngoje Bwana”. Zab. 26:14. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, jamii katika ujumla wake, itawaonea huruma watu wasiokuwa na makazi maalum na kuwapatia hifadhi.

Changamoto hii, ivaliwe njuga na Mama Kanisa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Iwe ni fursa ya kufanya tafakari ya kina kuhusu: Fumbo la Msalaba linaloonesha: Upendo, huruma, msamaha, sadaka na majitoleo ya Kristo Yesu hadi kifo cha aibu! Waamini wawe na ujasiri wa kuangalia undani wa Fumbo la Msalaba. Ibada kwa Madonda Mtakatifu ya Yesu, iwawezeshe waamini kuzama katika Moyo wake Mtakatifu, ili kujifunza na hatimaye, kutambua Fumbo la maisha na utume wa Kristo Yesu; Ukuu na Hekima ya Msalaba. Ni nafasi ya kumshukuru Kristo Yesu kwa mateso na kifo chake ambacho kimekuwa ni chemchemi ya ukombozi wa mwanadamu. Nyoka kadiri ya Maandiko Matakatifu ni adui na daima amekuwa akihusianishwa na kifo kama inavyooneshwa kwenye Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Hesabu: 21:4-9: Mwenyezi Mungu alipotuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma na watu wengi wakafa kutokana na manung’uniko yao kwa Mungu na kwa Mtumishi wake Musa kwani waliyakumbuka “masufuria ya nyama na vikapu vya vitunguu swaumu” na kusahau kwamba, huko walikuwa utumwani.

Katika muktadha huu, nyoka anaoneshwa kuwa ni chanzo cha ubaya na kifo. Lakini watu walipotubu na kuongoka, Mwenyezi Mungu akamwambia Musa kutengeneza nyoka ya shaba na kuiweka juu ya mti na wale wote walioumwa walipotazama ile nyoka, wakapona na kuishi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, unabii huu unapata utimilifu wake kwenye Agano Jipya. Mwinjili Yohane anasema, “Mtakapokuwa mmekwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafasi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo”. Yoh. 8:28. Mtakatifu Paulo Mtume anasema, “Yeye mwenyewe alizuchukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki na kwa kupigwa kwake mliponywa” (Rej. 1Pt.2:24). Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, Msalaba ni kielelezo cha utukufu, uhuruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Dhambi za binadamu zimetundikwa juu ya Msalaba wa Kristo Yesu. Fumbo la Msalaba ni mwaliko wa kulitafakari, kusali na kumshukuru Kristo Yesu.

Papa: Wasio na Makazi
31 March 2020, 14:23
Soma yote >