Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 18 Machi 2020 ametolea nia ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wagonjwa wa Corona waliofariki dunia sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 18 Machi 2020 ametolea nia ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wagonjwa wa Corona waliofariki dunia sehemu mbali mbali za dunia. 

Papa Francisko anawaombea wagonjwa waliofariki kwa Virusi vya Corona, COVID-19

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, 18 Machi 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wagonjwa wote wa Virusi vya Corona, COVID-19 waliofariki dunia sehemu mbali mbali za dunia, pamoja na kuwaombea wafanyakazi katika sekta ya afya ambao pia wametangulia mbele ya haki! Wafanyakazi wamekuwa ni kielelezo cha sadaka katika huduma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma, upendo na msamaha, awalinde watoto wake na Virusi vya Corona, COVID-19, awakirimie amani, utulivu wa ndani na matumaini; awajalie nguvu ya uponyaji na rehema marehemu wote waliotangulia mbele ya haki wakiwa na imani na matumaini ya ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu Francisko katika nia yake ya Misa wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatano tarehe 18 Machi 2020 imekuwa ni kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliofariki dunia sehemu mbali mbali za dunia, kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19 pamoja na kuwaombea wafanyakazi katika sekta ya afya ambao pia wametangulia mbele ya haki!

Baba Mtakatifu anasema, hawa wamekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa kwa sadaka inayonafsishwa katika huduma kwa jirani! Liturujia ya Neno la Mungu kutoka katika Kitabu cha Kumb. 4:1, 5-9 na Injili kama ilivyoandikwa na Mt. 5:17-19 inagusia “Sheria” na Kristo Yesu anawakumbusha wasikilizaji wake kwamba, wasidhani ya kuwa alikuja kuitangua Torati au Manabii; bali kutimiliza. Hii ni Sheria iliyotolewa na Mwenyezi Mungu na inapata utimilifu wake katika Kristo Yesu. Musa katika Kitabu cha Kumbu kumbu ya Torati anawahimiza Waisraeli kusikiliza Amri na Hukumu zitolewazo na Mwenyezi Mungu ili wapate kuishi na kuingia katika nchi ya ahadi.

Musa alizungumza kama rafiki ya Mungu kutokana na ukaribu aliokuwa nao. Kwa kutimiza Amri na Hukumu za Mungu, Waisraeli wangetambulikana kuwa ni watu wenye hekima na akili, kwa sababu hili ni taifa ambalo liko karibu sana na Mungu na daima anawasikiliza kila wamwitapo kwa moyo wa unyenyekevu. Huyu ni Mungu ambaye amewasindikiza na kuwalinda watoto wake katika hija ya maisha yao Jangwani, mchana kwao akawa ni Wingu zito lililowafunika na usiku Mnara wa moto uliowaongoza. Mwenyezi Mungu aliandika Sheria na Hukumu zake katika mwamba na kumkabidhi Musa, Mtumishi wake, lakini akaendelea kuonesha uwepo wake wa karibu kati pamoja nao!

Kwa bahati mbaya Waisraeli katika Agano la Kale, walitaka kumjaribu Mwenyezi Mungu ili kuona uwepo wake kati pamoja nao. Mwanadamu daima amekuwa akiukimbia uwepo wa Mungu katika maisha yake kwa kujificha kama ilivyokuwa kwa Adamu na Eva au kwa mauaji ya ndugu zake kama ilivyotokea kwa Kaini kumfeyekelea mbali ndugu yake Abeli. Kimsingi anasema Baba Mtakatifu, dhambi inamfanya binadamu kumkimbia Mwenyezi Mungu na hivyo kujificha mbali na uso wake wa huruma na mapendo. Daima mwanadamu anataka kuratibu uhusiano na mafungamano yake na Mwenyezi Mungu kadiri ya vionjo vyake. Mwenyezi Mungu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho amejinyenyekesha na kujitwalia hali ya ubinadamu katika mambo yote akawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi; akawa mtii hata mauti ya Msalaba.

Baba Mtakatifu amekazia kwa namna ya pekee kabisa fadhila ya unyenyekevu, ambayo Mwenyezi Mungu ameitumia ili kumsaidia mwanadamu, kwa kukaa pamoja naye na wala hayuko mbali sana na mwanadamu. Huu ni ushuhuda ambao umetolewa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Kristo Yesu aliambatana na wanafunzi wake, akafundisha na kuwaonya kwa upendo pale waliopotoka na kupotea njia kwa kutaka kumezwa na malimwengu. Kristo Yesu anaendelea kutoa changamoto kwa wafuasi wake, kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya upendo, badala ya kujiweka mbali na wengine hasa katika kipindi hiki kigumu cha mlipuko wa ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19.

Watu wajenge uwepo na ukaribu wao kwa njia ya sala na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, daima Mwenyezi Mungu yuko karibu sana na waja wake, tayari kuwasindikiza katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka waamini kumwomba Mwenyezi Mungu neema itakayowawezesha kujenga uhusiano wa karibu na mafungamano ya kijamii, kwa kuguswa na mahitaji ya jirani zao badala ya kuwageuzia kisogo.

Papa: Misa ya Wafu

 

 

18 March 2020, 14:49
Soma yote >