Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 21 Machi 2020 ametolea nia ya Misa Takatifu kwa ajili ya familia. Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 21 Machi 2020 ametolea nia ya Misa Takatifu kwa ajili ya familia.  (ANSA)

Virusi vya Corona, COVID-19: Papa Francisko aziombea familia

Papa Francisko anasema, huu ni wakati muafaka kwa familia kusali kwa bidii kwa kutambua kwamba, wengi wao bado wamefungiwa majumbani mwao kutokana na kuenea kwa Virusi vya Corona, COVID-19. Wanafamilia wote katika ujumla wao, wajenge mazingira yatakayowasaidia kuwasaliana vizuri zaidi; kwa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati ndani ya familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waamini wanapaswa kusali kwa uchaji na moyo wa unyenyekevu bila kujidai kwamba, wanayo haki mbele ya Mwenyezi Mungu. Huu ni wakati muafaka kwa familia kusali kwa bidii kwa kutambua kwamba, wengi wao bado wamefungiwa majumbani mwao kutokana na kuenea kwa Virusi vya Corona, COVID-19. Wanafamilia wote katika ujumla wao, wajenge mazingira yatakayowasaidia kuwasaliana vizuri zaidi; kwa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati ndani ya familia. Wasimame imara ili kushinda kishawishi cha mchoko na hali ya kujikatia tamaa.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 21 Machi 2020 wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko Mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuombea amani, upendo na mshikamano ndani ya familia katika kipindi hiki kigumu cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19. Liturujia ya Neno la Mungu inatoa mwaliko kwa waamini kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwaganga na kuwaponya majeraha yao. Wajitahidi kumtambua Mungu katika maisha yao, kwa kujenga imani na matumaini kwake.

Kumbe, sala ni njia makini ya kuweza kuzungumza mubashara na Mwenyezi Mungu. Katika Injili ya Luka, 18:9-14, Kristo Yesu anawafundisha wanafunzi wake namna bora zaidi ya kusali, kwa kujikita katika fadhila ya unyenyekevu, bila kuwadharau wala kuwatweza wengine wasioweza kufunga, kulipa zaka wala kuwa watakatifu kama wao walivyo! Farisayo na yule Mtoto mkubwa wa Baba mwenye huruma si mifano bora ya kuigwa kwani ni watu waliojidau kuwa wana haki na watakatifu. Waamini wajenge ndani mwao moyo wa toba na wongofu wa ndani, wawe tayari kukiri dhambi zao, ili kuomba huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama alivyofanya yule Mwana mpotevu anayesimuliwa kwenye Injili ya Baba mwenye huruma. Lazaro maskini awe ni mfano bora wa unyenyekevu katika kuomba.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kumwendea Mwenyezi Mungu kwa sala na ukweli kutoka katika undani wa maisha yao. Hakuna sababu ya kujiamini kipumbavu wala “kujimwambafai mbele ya Mwenyezi Mungu” kwani hakumsaidii mtu kukua na kukomaa kiroho na kiutu! Kumbe, waamini wajifunze fadhila ya unyenyekevu kama alivyofanya yule Mtoza ushuru, aliyemwomba Mungu radhi, akatambua udhaifu wake kuwa ni mwenye dhambi, akatubu na kumwongokea Mungu. Baba Mtakatifu anasema, huu ni mwanzo wa sala yenye mvuto na mashiko katika maisha ya waamini. Baba Mtakatifu alihitimisha Ibada hii ya Misa Takatifu kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, akawapatia waamini na wale wote waliokuwa wanafuatilia Ibada hii ya Misa Takatifu kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, baraka ya Ekaristi Takatifu.

Papa: familia

 

 

21 March 2020, 16:03
Soma yote >