Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana na wale wote wanaolia na kuomboza kutokana na kuguswa na kutikiswa na janga la Virusi vya Corona. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana na wale wote wanaolia na kuomboza kutokana na kuguswa na kutikiswa na janga la Virusi vya Corona.  (Luigi Avantaggiato 2019)

Baba Mtakatifu Francisko: Jumapili ya Kilio cha Watu wa Mungu

Kristo Yesu alitokwa na machozi ya uchungu alipomwona Mariamu na waombolezaji wengine wakimlilia Lazaro, kielelezo cha urafiki na upendo wa dhati. Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kama sehemu ya mchango wa Kanisa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19! MACHOZI!

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya V ya Kipindi cha Kwaresima inawatafakarisha waamini kuhusu fumbo la mateso, kifo, ufufuko na uzima wa milele unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu. Katika kipindi hiki maalum cha historia ya mwanadamu, ambako kuna maambulizi makubwa ya ugonjwa wa mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ni wakati muafaka wa kuomba neema ya kuweza kuomboleza na wale wanaomboleza! Kristo Yesu alitokwa na machozi ya uchungu alipomwona Mariamu na waombolezaji wengine wakimlilia Lazaro, kielelezo cha urafiki na upendo wa dhati. Kwa muda wa majuma matatu, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican kama sehemu ya mchango wa Kanisa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Baba Mtakatifu, Jumapili tarehe 29 Machi 2020 amesali na kutolea nia ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wale wote wanao omboleza kutokana na kuondokewa na ndugu, jamaa na rafiki zao kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona. Kuna maelfu ya watu waliolazwa kwenye vyumba vya wagonjwa mahututi, ICU; kuna watu ambao wamewekewa karantini hawawezi kutoka; kuna wazee ambao wanaelemewa na upweke; kuna wazazi na walezi ambao wanahofia hatima ya maisha ya watoto wao kutokana na kukosa fursa ya ajira. Kimsingi, kuna umati mkubwa wa watu wa Mungu unaomlilia Mungu, kuomba huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana na watu wote hawa ili kumlilia Mwenyezi Mungu, kama alivyofanya hata Kristo Yesu, mbele ya rafiki yake Lazaro.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amefafanua kuhusu ufufuko wa Lazaro kama anavyosimulia Mwinjili Yohane: 11: 1-45, lakini kwa namna ya pekee, kilio cha Kristo Yesu, kutokana na kifo cha Lazaro! Yesu alilia kwa upendo mkubwa, akaungana na ndugu, jamaa na marafiki wa Lazaro kuomboleza; akawaonesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuomba neema na baraka ya kuweza kuomboleza na wale wote wanao omboleza kutokana na janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kristo Yesu alikuwa na urafiki wa karibu sana na familia ya Martha, Mariamu na Lazaro, ndiyo maana alipokutana mubashara na waombolezaji, hata Yesu, akatokwa machozi.

Katika sehemu nyingine ya Maandiko Matakatifu, Kristo Yesu anaoneshwa akiulilia mji wa Yerusalemu. Hiki ni kilio kinachobubujika huruma na upendo. Hakuna uhakika kwamba, Yesu alipokuwa kwenye Bustani ya Gethsemane alilia pia! Kristo Yesu, daima aliguswa na mahangaiko ya watu waliomzunguka kiasi cha kuwaonea huruma na mapendo; akawasikiliza na kuwakirimia kadiri ya mahitaji yao: kiroho na kimwili; akawaondolea dhambi na kuwaponya magonjwa yao; akawafufua; akawalisha na kuwanywesha. Kristo Yesu alikuwa na jicho la huruma na upendo. Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuguswa na mahangaiko ya watu wanaolia, wanaomboleza na kuteseka, tayari kujibu kilio chao kama kielelezo cha imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, amewaalika waamini kumkimbilia na kumlilia Mungu ili aweze kuwakirimia huruma na upendo wake wa daima. Mwishoni mwa Ibada ya Misa Takatifu amewaombea wale wote ambao kutokana na sababu za ulinzi na usalama, wanashindwa kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu, ili waweze kumkaribisha Kristo Yesu katika undani ya maisha yao, tayari kuungana naye! Baba Mtakatifu amewaalika waamini kuimba ule wimbo wa Bikira Maria “Ave Regina Caelorum”: Salam Malkia wa Mbingu!

Papa: Fumbo la Kifo

 

29 March 2020, 14:55
Soma yote >