Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma katika upendo na unyenyekevu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma katika upendo na unyenyekevu!  (Vatican Media)

Papa Francisko uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma!

Kristo Yesu katika Injili ya Mk. 9:30-37 anafafanua kwamba, mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuondokana na uchu wa mali, madaraka, kwani kwa kufanya hivi watamezwa na malimwengu, kiasi hata cha kugeuka kuwa ni maadui wa Mungu. Uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Uchu wa mali, madaraka na sifa ni kielelezo cha watu kumezwa na malimwwengu, hali inayochochewa na tamaa na wivu na matokeo yake wanakuwa ni rafiki wa dunia na kwa upande mwingine, wanakuwa ni adui wa Mungu. Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu wa moyo! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 25 Februari 2020 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kukita maisha yao katika tunu msingi za Kiinjili, kwa kuepuka kishawishi cha kutaka kuwatala wengine kwa kujielekeza zaidi katika moyo wa huduma kama Mtume Yakobo anavyoelekeza katika Waraka wake kwa watu wote: 4:1-10.

Kristo Yesu katika Injili ya Mk. 9:30-37 anafafanua kwamba, mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuondokana na uchu wa mali, madaraka, kwani kwa kufanya hivi watamezwa na malimwengu, kiasi hata cha kugeuka kuwa ni maadui wa Mungu. Yesu anawaalika wafuasi wake, kushikamana naye katika maisha, vinginevyo watakwenda kinyume chake. Katika utekelezaji wa tunu msingi za Kiinjili hakuna njia ya mkato. Uchu wa baadhi ya watu kutaka kupata umaarufu, ni chanzo cha kutaka kuwanyanyasa na kuwatweza wengine kwa ajili ya mafao binafsi.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, vita, kinzani na mipasuko sehemu mbali mbali za dunia ni kutokana na watu kumezwa na malimwengu pamoja na tamaa kama anavyobainisha Mtume Yakobo katika Waraka wake kwa watu wote. Mbegu ya vita, kinzani na mipasuko inayojionesha sehemu mbali mbali za dunia, kamwe haiwezi kuliacha Kanisa likiwa salama! Hata ndani ya Kanisa kuna vita na misuguano kama ilivyokuwa wakati ule wa Mitume wa Yesu kwa sababu kuna baadhi ya watu wanadhani kwamba wao ni bora zaidi kuliko wengine! Kuna baadhi ya viongozi wa Kanisa ambao wamemezwa na uchu wa mali na madaraka, mambo yanayokwenda kinyume kabisa na tunu msingi za maisha ya Kikristo.

Chuki, wivu, umbea na maseng’enyo kwa watu wengine ni kazi ya Shetani, Ibilisi. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, katika majadiliano kati ya Mitume wa Yesu, mambo yote haya yalijitokeza. Lakini, Yesu akasahihisha mwelekeo huu potofu kwa kukazia kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha huduma na wala si kwa sababu ya baadhi ya watu kuwa na kiwango cha juu cha elimu. Uongozi wa Kanisa unasimikwa katika hali ya upole, unyenyekevu na utu wema. Katika hali na mazingira kama haya, hakuna sababu kwa waamini kujadiliana na Shetani, Ibilisi kwani atawatumbukiza na kuwazamisha kwenye malimwengu na badala yake, wawe makini kumsikiliza Kristo Yesu anayewataka kuwa watumishi wa wote!

Papa: Mahubiri 25 Feb.
25 February 2020, 17:13
Soma yote >