Papa Francisko: Acheni kulalamika kwani Mwenyezi Mungu anafariji na kuonya kwa huruma na mapendo! Papa Francisko: Acheni kulalamika kwani Mwenyezi Mungu anafariji na kuonya kwa huruma na mapendo!  (ANSA)

Papa Francisko: Acheni kulalama! Mungu anafariji na kuadhibu!

Paza sauti yako, usiogope; iambie miji ya Yuda, Tazameni, Mungu wenu! Tazameni, thawabu yake i pamoja naye, na ijara yake i mbele zake. Atalilisha kundi lake kama mchungaji, atawakusanya wanakondoo mikononi mwake; na kuwachukua kifuani mwake, nao wanyonyeshao atawaongoza polepole. Papa Francisko anasema, Mwenyezi Mungu anafariji na kuwaadhibu watu kwa huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Sikiliza ni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni nyikani njia ya Bwana, nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu. Kila bonde litainuliwa, na kila mlima na kilima kitashushwa; palipopotoka patakuwa pamenyoka, na palipoparuza patasawazishwa. Na utukufu wa Bwana utafunuliwa, na wote wenye mwili watauona pamoja, kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena haya. Wewe uuhubiriye Sayuni habari njema, panda juu ya mlima mrefu; wewe uuhubiriye Yerusalemu habari njema, paza sauti kwa nguvu. Paza sauti yako, usiogope; iambie miji ya Yuda, Tazameni, Mungu wenu! Tazameni, thawabu yake i pamoja naye, na ijara yake i mbele zake. Atalilisha kundi lake kama mchungaji, atawakusanya wanakondoo mikononi mwake; na kuwachukua kifuani mwake, nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.

Huu ni muhtasari wa Liturujia ya Neno la Mungu, uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumanne, tarehe 10 Desemba 2019 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Mwenyezi Mungu kwa njia ya Nabii Isaya anasema atawafariji watu wake kwa kuwatangazia Injili ya matumaini kwa wale waliopondeka moyo. Mwenyezi Mungu yuko tayari kuwafariji wale wote wanaojiaminisha kwa faraja yake, kwani atawakusanya watoto wake, atawarekebisha wale waliokengeuka kwa kuwachukua kifuani pake kwa huruma. Hii ni faraja inayopata chimbuko lake kutoka katika undani wa mtu, kwa kutambua hali yake ya dhambi na udhaifu wake, tayari kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu katika maisha. Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, kama anavyojionesha kwenye mfano wa Baba mwenye huruma. Alipomwona mwana mpotevu, akamkimbilia na kumlaki.

Huu ndio mwelekeo wa Kristo Yesu mchungaji mwema anayethubutu kuacha Kondoo 99 na kuanza kujitaabisha kumtafuta mmoja aliyetokomea porini. Hii ndiyo chemchemi ya furaha na matumaini ya Kristo Yesu kwa mdhambi anayetubu na kumwongokea Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumkimbilia Kristo Yesu, ili aweze kuwasamehe na kuwaondolea dhambi zao pamoja na kuwafariji. Angalisho kwa waamini ni kwamba, Shetani, Ibilisi anataka kuwaona wakitumbukia katika huzuni, hofu na mashaka makubwa, kiasi kwamba, litania ya malalamiko inakuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa maisha yao, kiasi hata cha kubahatika kupewa tuzo ya Nobel kwa kulalamika.

Kulalamika ni sehemu ya udhaifu wa binadamu anasema Baba Mtakatifu Francisko, lakini Mwenyezi Mungu yuko tayari kuwasamehe waja wake, wanapo tubu na kumwongokea; anawafariji na kuwaongoza kwenye malisho mazuri na kando ya maji ya utulivu. Huyu ndiye Mwenyezi Mungu aliyeumbwa mbingu na dunia. Kristo Yesu kwa huruma na upendo wake mkuu, akathubutu kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni kwa kuteswa na kufa Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi. Kristo Yesu ni chemchemi ya faraja kwa wale wote wanaohuzunika kama alivyofanya kwa yule Mjane wa Naini, aliyekuwa analia na kumwobolezea binti yake. Kumbe, kwa waamini wote wanaoelemewa na dhambi, wanahamasishwa kumwendea Kristo Yesu, ili aweze kuwafuta machozi na kuwafariji, kwa kuwaondolea na kuwasamehe dhambi zao. Hii inahitaji ujasiri wa kupiga moyo konde na kuanza safari kumwendea Yesu. Yeye atawakaribisha na kuwafariji kama Baba na kaka yao; kama mchungaji mwema anayewaongoza kondoo wake kwenye malisho mabichi.

Papa: Mahubiri

 

10 December 2019, 15:15
Soma yote >