Papa Francisko anawaalika waamini kusimika maisha na matumaini yao katika mwamba imara na thabiti ambao ni Kristo Yesu. Papa Francisko anawaalika waamini kusimika maisha na matumaini yao katika mwamba imara na thabiti ambao ni Kristo Yesu.  (ANSA)

Papa Francisko awataka waamini kusimika maisha na matumaini yao katika mwamba thabiti

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu ndiye mwamba ule imara na thabiti unaowataka waamini kutafakari kuhusu hekima ya kimungu na udhaifu wa binadamu; yaani mahali ambapo waamini wanaweka na kuhifadhi matumaini, uhakika na usalama wa maisha yao. Kristo Yesu ni mwamba thabiti kwa mtu yeyote anayemtumaini atapata usalama na uhakika wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, Alhamisi tarehe 5 Desemba 2019 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican amewaalika waamini  kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao kwa kuyajenga na kuyasimika juu ya mwamba thabiti ambao ni Kristo Yesu mwenyewe. Kwa sababu kila asikiaye hayo maneno ya Kristo Yesu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba, mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno ya Kristo Yesu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa. Hii ni sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 7: 21; 24-27.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu ndiye mwamba ule imara na thabiti unaowataka waamini kutafakari kuhusu hekima ya kimungu na udhaifu wa binadamu; yaani mahali ambapo waamini wanaweka na kuhifadhi matumaini, uhakika na usalama wa maisha yao. Kristo Yesu ni mwamba thabiti kwa mtu yeyote anayemtumaini atapata usalama na uhakika wa maisha. Huu ni mwaliko kwa waamini kukita matumaini yao kwa Kristo Yesu. Mambo na mapambo ya nje yanayotaka kuteka akili na nyoyo za watu ni sawa na mchanga tu, mafuriko yakija hakuna kitu kinachoweza kusalia. Hii ndiyo hali inayojitokeza hata katika ujenzi wa majengo, ikiwa kama msingi si imara, majengo kama hayo “yatashuka na kuteketea kama biskuti”. Kumbe, hata waamini wanapaswa kujitahidi kuhakikisha kwamba, maisha yao ya kila siku yanasimikwa katika mwamba thabiti.

Ili kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha, mwamini hana budi kwanza kabisa kuangalia msingi wa maisha yake umesimikwa katika mambo gani? Bila kuwa na msingi imara nathabiti, maisha yanaweza kuporomoka na kutoweka kama “ndoto ya mchana”. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu neema na busara ya kuweza kuchagua msingi thabiti ambao wataweza kuutumia kukita matumaini na usalama wa maisha yao. Watu watambue udhaifu wao kama binadamu na kwamba, wanaweza kutindikiwa na kuanguka dhambini. Katika muktadha kama huu, wataweza kuwa na ujasiri wa kukita maisha yao kwa Kristo Yesu, mwamba thabiti. Kumbe, toba na wongofu wa ndani unapaswa kuelekezwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Waamini wawe na uthubutu wa kujenga na kuyasimika maisha yao katika mwamba thabiti, Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu na maisha ya uzima wa milele. Katika kipindi cha majilio, waamini wajifunze kutafakari na kuona ni mahali gani ambako wamesimika matumaini na usalama wa maisha yao!

Papa: Mwamba Thabiti
05 December 2019, 15:25
Soma yote >