Tafuta

Papa Francisko asema, Shetani, Ibilisi ana wivu sana dhidi ya Fumbo la Umwilisho linalotukuza utu na heshima ya binadamu. Papa Francisko asema, Shetani, Ibilisi ana wivu sana dhidi ya Fumbo la Umwilisho linalotukuza utu na heshima ya binadamu.  (ANSA)

Papa Francisko: Shetani ana wivu dhidi ya Fumbo la Umwilisho!

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kumbe, ni watoto wateule wa Mungu, kifo ni matokeo ya husuda wa Shetani, ambaye hakuwa tayari kukiri kuhusu ukuu wa Fumbo la Umwilisho. Ingewezekana kabisa kuishi katika misingi ya umoja, udugu na amani, lakini daima Shetani, Ibilisi yuko kati kati yao, akijitahidi kuharibu mahusiano yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 12 Novemba anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Josafat Kuncewicz, Askofu na shahidi aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko katika mahubuiri yake amegusia kuhusu Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kukaa kati ya watu wake na hila za Shetani, Ibilisi anayetaka kumwangamiza mwanadamu. Maandiko Matakatifu yanabainisha kwamba, Mwenyezi Mungu alimuumba mwanadamu ili apate kutokuharibika, kwa mfano wake mwenyewe, ila ulimwengu uliingiwa na mauti kwa husuda yake Shetani, Ibilisi nao walio wa upande wake hupata kuionja (Rej. Hek. 2:23-3:9). Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kumbe, ni watoto wateule wa Mungu, kifo ni matokeo ya husuda wa Shetani, Ibilisi ambaye hakuwa tayari kukubali kupokea na kukiri kuhusu ukuu wa Fumbo la Umwilisho.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, kwamba, licha ya binadamu wote kuwa ndugu na kwamba, ingewezekana kabisa kuishi katika misingi ya umoja, udugu na amani, lakini daima Shetani, Ibilisi yuko kati kati yao, akijitahidi kila kukicha kuharibu mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu kwa kuwasengenya wengine, kwa kuwaharibia sifa njema na utu wao kama binadamu. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, ulimi ni silaha kali sana pengine hata kuliko upanga wenye makali kuwili.  Waamini licha ya kupokea Sakramenti ya Ubatizo na kuondolewa ile dhambi ya asili, lakini ndani mwa mwanadamu kuna mapambano makali sana kama ilivyokuwa tangu enzi ya Kaini na Abeli nduguye. Hawa walikuwa ni ndugu wamoja, lakini, wivu na kijicho kilipoingia, matokeo yake, Kaini “akamfyekelea mbali” ndugu yake Abeli. Huu ndio ukweli wa mambo hata leo hii bado kuna watu wengi wanapoteza maisha kutokana na vita, njaa na magonjwa.

Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 11 Novemba 2019 imefanya kumbu kumbu ya Miaka 30 tangu Ukuta wa Berlin ulipobomolewa; watu wengi waliuwawa kutokana na chuki za kisiasa na bado kuna madhara makubwa ya mauaji ya kimbari yanayoendelea sehemu mbali mbali za dunia. Zote hizi ni jitihada za Shetani, Ibilisi na waamini wasipokuwa makini kuna watu ambao kila siku kazi yao ni kutaka kupandikiza “ndago za chuki, uhasama, vita na kinzani” mambo yanayoendelea kuusambaratisha ulimwengu. Kuna mamilioni ya watoto wanaokufa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; watoto ambao hawana tena nafasi wala fursa ya kwenda shuleni kupata elimu itakayowakomboa katika maisha kutokana na vita Kuna watu wanateseka kutokana na kukosekana kwa huduma bora za afya, maji safi na salama. Lakini, kwa vyombo vingi vya mawasiliano ya jamii, hizi si habari zenye mashiko wala mvuto! Rasilimali fedha ambayo ingetumika kwa ajili ya maboresho ya uhakika na usalama wa chakula, huduma ya afya na elimu bora, inatumika kwa ajili ya kutengengezea silaha za maangamizi ya binadamu.

Ibilisi anaendelea kupandikiza ndago za chuki na uhasama hata katika nyoyo za waamini, hii inatokana na ukweli kwamba, Shetani, Ibilisi anaona wivu juu ya Fumbo la Umwilisho. Kumbe, vita, chuki, uhasama na magomvi yanayoendelea sehemu mbali mbali za dunia ni matokeo ya wivu wa Shetani, Ibilisi. Hayo ndiyo yanayoendelea kujitokeza hatika katika medani za kisiasa, kwani kuna watu kazi yao ni kupandikiza ndago za chuki, ili kuona watu wakifarakana. Misingi ya ukweli, uwazi, ustawi na maendeleo ya wengi kwao ni ndoto ya mchana. Hawa ni wale wanasiasa “uchara” wanaotaka kujijengea jina kwa kuwachafua wenzao kwa sifa mbaya! Hawa wanaendesha siasa kwa falsafa yak ile kinachodaiwa “eti niguse kinuke”. Ni kwa njia ya usuda na wivu wa Shetani, Ibilisi, mauti imeingia ulimwenguni. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu, ili awasaidie kuimarisha imani, matumaini na mapendo yao kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na kamwe wasitumbukie katika mtego wa Shetani, Ibilisi, mwongo mkubwa na mpandikizaji wa chuki na uhasama kati ya watu!

Papa: Shetani

 

12 November 2019, 15:12
Soma yote >