Watu wote wanaalikwa kwenye karamu ya maisha na uzima wa milele! Jambo la msingi ni kukubali na kuitikia mwaliko huu! Watu wote wanaalikwa kwenye karamu ya maisha na uzima wa milele! Jambo la msingi ni kukubali na kuitikia mwaliko huu!  (Vatican Media)

Papa Francisko: watu wote wanaalikwa kwenye Karamu ya uzima!

Sehemu hii ya Injili kama ilivyoandikwa na Luka ni muhtasari wa historia nzima ya wokovu inayoonesha hata mienendo mbali mbali wa maisha ya Wakristo. Karamu ni kielelezo cha furaha ya maisha na uzima wa milele. Ni mahali pa watu kukutana na kufahamiana; kusherehea na kupongezana kwa majitoleo mbali mbali. Sherehe inapaswa kuwa na mvuto unaofumbatwa katika sadaka.!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu anaendelea kuwaalika watu mbali mbali ili waweze kushiriki katika karamu ya maisha na uzima wa milele kama anavyofafanua Mwinjili Luka, 14:15-24, lakini kwa bahati mbaya anakumbana na watu ambao hawako tayari kuitikia mwaliko wake, kila mtu akiwa na sababu zake maalum. Kwa vile wale waliokuwa wamealikwa walikataa, Bwana mwenye sherehe akawaalika maskini, vilema na vipofu, wakaijaza nyumba yake. Hii ni changamoto mamboleo, kwani hata leo hii, Kristo Yesu anawaalika waja wake ili kushiriki katika karamu yake, Jambo la msingi ni kujiuliza, Je, wanakubali mwaliko au pengine, wanaamua kujifungia katika ubinafsi wao. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 5 Novemba 2019 amesema kwamba, sehemu hii ya Injili kama ilivyoandikwa na Luka ni muhtasari wa historia nzima ya wokovu inayoonesha hata mienendo mbali mbali ya maisha ya Wakristo.

Karamu, chakula au dhifa ni kielelezo cha furaha ya maisha na uzima wa milele. Ni mahali pa watu kukutana na kufahamiana; kusherehea na kupongezana kwa majitoleo mbali mbali. Sherehe inapaswa kuwa na mvuto unaofumbatwa katika sadaka na majitoleo ya watu. Mwenyezi Mungu anawaalika waja wake kuingia katika karamu ya Ufalme wa mbinguni, bureee kabisa bila malipo, kwa sababu tayari amekwisha kujisadaka kwa ajili ya maandalizi, kinachobakia ni ustashi tu wa kuamua kwenda kushiriki sherehe hii. Lakini kwa bahati mbaya, kuna tabia ya watu kutaka kujifungia katika ubinafsi wao kwa kuonesha shingo ngumu, “huko mimi siendi”. Hawa ni watu wanataka kubaki pekee yao wakiwa wamejifungia katika ubinafsi wao. Hii ndiyo dhambi ya Waisraeli, dhambi ambayo inaendelea kuwapekenya waamini mbali mbali hata katika nyakati hizi, kwa kupenda mno kujifungia katika ubinafsi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, tabia ya kukataa kuitikia mwaliko ni kuonesha dharau kwa yule mwenye sherehe aliyewaalika; ni kukataa kushiriki katika furaha ya kukutana na Kristo Yesu.

Kwa bahati mbaya, katika hija ya maisha ya waamini, daima watajikuta wakiwa wanakabiliana na changamoto kama hizi, yaani changamoto ya kuitikia mwaliko na kuamua kushiriki, au kukataa na kuendelea kubaki katika ubinafsi. Utajiri wa mali pamoja na kumezwa na malimwengu ni kati ya mambo ambayo yanawachanga waamini kiasi hata cha kushindwa kuitikia mwaliko. Lakini hata kundi la matajiri, wapo matajiri ambao wametumia vyema utajiri wao kwa ajili ya huduma kwa maskini, leo hii  wamekuwa ni watakatifu  na mifano bora ya kuigwa. Hii ni changamoto kwa waamini kutojifungamanisha sana na fedha pamoja na mali, bali wawe tayari kuachia yote ili kushiriki katika karamu ya maisha na uzima wa milele. Mwaliko huu ni kwa watu wote, wema na wabaya pasi na ubaguzi. Sehemu hii ya Injili iwakumbushe waamini huruma na upendo wa Baba mwenye huruma alipomwona yule Mwana mpotevu, akamkumbatia na huo ukawa ni mwanzo wa sherehe.

Mtakatifu Paulo, Mtume katika somo la kwanza anakazia unyenyekevu na upendo katika maisha ya kijumuiya ili kuondokana na unafiki katika maisha. Kuna Wayahudi waliomkata Kristo Yesu kwa kudhani kwamba, wao ni wenye haki, lakini anawaonya kwamba, wasipotubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, wasije wakashangaa kuwaona wadhambi, maskini na watoza ushuru wakiwa wamewatangulia katika Ufalme wa Mungu. Hii ni changamoto na mwaliko wa kutoka katika ubinafsi na kuanza hija ya kumwendea Kristo Yesu. Waamini wajiulize, Je, hali yao ya maisha kwa sasa iko namna gani? Je, wako tayari kuitikia mwaliko wa Kristo au wametingwa na mambo mengi ya maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kukubali mwaliko, ili hatimaye, kushiriki katika karamuya maisha na uzima wa milele.

Papa: Karamu
05 November 2019, 14:15
Soma yote >