Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa: neema, huruma na mapendo, kwa wale wote wanaotubu na kumwongokea. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa: neema, huruma na mapendo, kwa wale wote wanaotubu na kumwongokea.  (ANSA)

Papa Francisko: Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo!

Kristo Yesu, ufunuo wa huruma ya Mungu, amekuja kuokoa na wala si kulaani na kuangamiza. Papa amefafanua kuhusu mapambano kati ya Nabii Yona na Mwenyezi Mungu; Yona anayejaribu kutoroka Neno la Mungu; Yona anayemezwa kwenye tumbo la samaki; naye anamwokoa na kwa mahubiri ya Yona, Waninawi wanamwongokea Mungu, naye anawasamehe baada ya kutubu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 8 Oktoba 2019 amekazia umuhimu wa waamini kujinyenyekesha katika safari ya maisha yao, kwani Mwenyezi Mungu anapenda kuwa karibu na waja wake katika uhalisia wa maisha yao, kwa njia ya huruma na upendo. Kristo Yesu, ufunuo wa huruma ya Mungu, amekuja kuokoa na wala si kulaani na kuangamiza. Baba Mtakatifu amefafanua kuhusu mapambano kati ya Nabii Yona na Mwenyezi Mungu; Yona anayejaribu kutoroka Neno la Mungu; Yona anayemezwa kwenye tumbo la samaki, anayemwomba Mwenyezi Mungu naye anamwokoa na kwa mahubiri ya Yona, Waninawi wanamwongokea Mungu, naye anawasamehe baada ya kutubu na kumwongokea, kwa kuyaacha matendo yao maovu.

Baba Mtakatifu anasema, Nabii Yona alikaa ndani ya tumbo la samaki kwa muda wa siku tatu, mchana na usiku, kielelezo cha ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Na kwa upande wa Nabii Yona, huu ni ufufuko wake, ambao ni chimbuko la wito wake na chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Ninanwi. Hata hivyo, Yona anamkasirikia sana Mwenyezi Mungu kwa kuwa na huruma kwa wadhambi, kwani Mungu alitenda kinyume na mahubiri yake, kwa kusema kwamba, baada ya siku arobaini, mji wa Ninawi ungeangamizwa. Nabii Yona anasikitika kwa sababu anafahamu fika kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwenye neema, amejaa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema naye anaghairi mabaya. Nabii Yona alikasirika kiasi cha kumwomba Mwenyezi Mungu amwondolee uhai wake, kwani alikuwa anatenda kinyume cha unabii wake!

Nabii Yona akajificha ili kuangalia ikiwa kama Mwenyezi Mungu atauangamiza mji wa Ninawi, lakini hata katika shida na mahangaiko yake ya ndani, bado Mwenyezi Mungu aliendelea kumlinda, kumtunza na kumponya katika hali yake mbaya, kiasi cha Yona kuufurahia ule mtango, lakini kesho yake, akapigwa na jua kiasi cha kujutia kuzaliwa! Mwenyezi Mungu akamwambia kwamba, hata yeye alipaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu katika maisha na utume wake. Nabii Yona alikuwa ni mtu mwenye imani ya masharti; akataka hata kumwamuru Mwenyezi Mungu atende kama alivyotaka yeye. Huu ni mfano wa wale Wakristo wenye imani ya masharti na wanataka kudhibiti matendo ya Mungu. Hawa ni waamini wanao ogopa kukua na kukomaa katika imani na matokeo yake, wanaishia kutumbukia katika siasa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni waamini ambao wanashindwa kukabiliana na changamoto katika historia na maisha; ni watu waliogandamana na mawazo yao, wanaotamani zaidi siasa badala ya imani ya kweli, kiasi kwamba, wanajikuta wakiwa mbali na jamii ya waamini. Ni watu wanao ogopa kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu na badala yake, wanageuka kuwa ni majaji, hali inayoonesha unyonge kutoka katika undani wa maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha mahubiri yake kwa kusema, kwamba, wahusika wakuu katika Liturujia ya Neno la Mungu Jumanne, tarehe 0 Oktoba 2019 yaani: Nabii Yona na Martha ndugu yake Lazaro, ni mifano hai inayoonesha jinsi ambavyo Kristo Yesu anajihusisha na kila hali ya maisha ya waja wake. Huu ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuonja huruma, upendo na msamaha wake wa daima. Ni Mungu anayeheshimu utu wa binadamu, anawakumbatia na kuwahurumia wadhambi na wagonjwa wa Ukoma; kwa sababu Kristo Yesu amekuja ili kuganga, kuwaponya na kuwakomboa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na wala si nia yake, kuhukumu!

Papa: Nabii Yona

 

08 October 2019, 15:23
Soma yote >