Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asema, mapambano ya maisha ya kiroho ni endelevu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuomba neema ya Roho Mtakatifu! Papa Francisko asema, mapambano ya maisha ya kiroho ni endelevu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuomba neema ya Roho Mtakatifu!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Mapambano ya maisha ya kiroho ni endelevu!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, amekazia umuhimu wa kukuza na kudumisha mapambano ya ndani dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo, daima wakiomba msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Haya ni mapambano ambayo kila mwamini ameyapitia na watakatifu wameweza kufanikiwa katika maisha yao kwa njia ya msaada na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Ijumaa tarehe 25 Oktoba 2019 ni mwaliko kwa waamini kuchunguza dhamiri zao na kuangalia jinsi wanavyopambana na ubaya ulioko ndani mwao kwa kushindwa kutekeleza jambo jema kutokana na uwepo wa dhambi katika maisha ya mwanadamu. Mtakatifu Paulo Mtume anawakumbusha Warumi kwamba, ndani ya mwanadamu kuna sheria inayomsukuma mtu kutenda jema, lakini pia lipo lililo baya. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichopo mjini Vatican amekazia umuhimu wa kukuza na kudumisha mapambano ya ndani dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo, daima wakiomba msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Haya ni mapambano ambayo kila mwamini ameyapitia na watakatifu wameweza kufanikiwa katika maisha yao kwa njia ya msaada na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Roho Mtakatifu anawahimiza kutenda yaliyo mema, lakini Shetani, Ibilisi anawadanganya kwa kuwataka watende mabaya.

Haya ni mapambano endelevu ya maisha na wala hakuna jambo la kujidanganga kwa kudhani kwamba, yote ni kawaida na yanapita! Mwamini anaweza kupambana na hali na mazingira yake, akafanikiwa kwa siku moja, lakini atambue kwamba, Shetani, Ibilisi daima anatafuta mbinu mpya za kutekeleza azma ya kutaka kuwaangusha watu wa Mungu dhambini. Hii ni changamoto kwa kila mwamini kupambana kufa na kupona ili kulinda imani kama alivyofanya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu. Akiwa kitandani, dakika za mwisho za uhai na maisha yake, akajisikia kwamba, ndani mwake, alikuwemo Shetani, Ibilisi, aliyetaka kumvuruga na kumgiribu na kumng’oa katika uwepo wa Kristo Yesu ndani mwake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna nyakati maalum za mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi na kuna nyakati za mapambano ya kawaida tu! Mwinjili Luka katika Injili ya leo anawaambia waamini kusoma na kutambua alama za nyakati.

Waamini waangalie na kujichunguza ikiwa kama mawazo yao yanapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu au wanafanya maamuzi kwa kujisikia na kwa kadiri ya vionjo vyao? Wajiulize ikiwa kama Mwenyezi Mungu amewasaidia kutenda wema kwa kujiaminisha kwake. Kabla ya kuhitimisha siku, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuchunguza dhamiri zao ili kutambua yale yanayojiri katika undani wa maisha yao! Ni rahisi sana kutambua ya wengine, lakini yale ambayo yamefichika katika undani wa mtu si rahisi sana kuweza kutambuliwa!

Papa: Dhamiri

 

25 October 2019, 15:30
Soma yote >