Papa Francisko anasema, maisha ya Mkristo yanafumbatwa katika huduma kwa Mungu na jirani! Papa Francisko anasema, maisha ya Mkristo yanafumbatwa katika huduma kwa Mungu na jirani!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Maisha ya Mkristo ni huduma kwa Mungu na jirani!

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Barnabas Mtume, amekazia umuhimu wa kudumisha moyo wa sadaka na majitoleo kwa kuambatana na Mwenyezi Mungu. Pili, neema na baraka ziwasaidie kuboresha maisha yao ya kiroho na wala wasiwe ni watu wanaoelemewa na uchu wa fedha na mali. Wamepewa bure, watoe bure kama sadaka safi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 11 Juni 2019, Kumbu kumbu ya Mtakatifu Barnabas mtume, amekazia mambo makuu matatu yanayopaswa kutekelezwa na waamini: Mosi ni kuhakikisha kwamba, wanakuza na kudumisha moyo wa sadaka na majitoleo kwa kuambatana na Mwenyezi Mungu katika maisha yao na kwamba, neema na baraka ziwasaidie kuboresha maisha yao ya kiroho na wala wasiwe ni watu wanaoelemewa na uchu wa fedha na mali.

Neema ambayo viongozi wa Kanisa wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu na wala si vinginevyo! Wanapaswa kuwa ni wahudumu wa furaha ya Injili na kamwe wasiwe ni watu wanaodhani kwamba, wanapaswa wao kuhudumiwa kwanza! Tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko imekita mizizi yake katika sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Mathayo 10:7-13; anakumbusha kwamba, huu ni wito ambao wameupata bure na wanapaswa kuutoa bure! Yesu anawaambia Mitume wake, shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.

Katika kuenenda kwao, wahubiri kwa kusema, Ufalme wa mbinguni umekaribia! Akawapatia pia uwezo wa kuponya wagonjwa, kufufua wafu, kutakasa wakoma na kutoa pepo wachafu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni utume unaofumbatwa katika huduma kwa watu wa Mungu na kwamba, maisha ya Kikristo ni maisha ya huduma. Baba Mtakatifu anasikitika kuona jinsi ambavyo baadhi ya waamini wanapoongoka na kumwambata Mungu katika maisha yao, wanakuwa na ari na moyo wa kujitoa na kujisadaka, lakini wanapoendelea na safari ya imani, wanajikuta wanakuwa mzigo kwa Jumuiya ya waamini, badala ya kuhudumia, wanataka sasa wao ndio wawe wa kwanza kuhudumiwa!

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, maisha ya Kikristo yanafumbatwa katika sadaka na majitoleo binafsi kwa ajili ya Mungu na jirani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, wokovu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Wamepewa bure na wanapaswa hata wao kutoa bure! Hakuna mtu aliyelipia wokovu wake, kwani wote wameokolewa kwa huruma na upendo wa Mungu, jambo jema sana! Lakini, Mwenyezi Mungu anawataka waja wake, kumfungulia malango ya nyoyo zao, ili kujenga na kudumisha mahusiano mema kama wanavyofanya wakati wa kusali Sala ya Baba Yetu.

Sadaka na majitoleo, yawasaidie waamini kushikamana zaidi na Mwenyezi Mungu katika maisha yao! Kufunga, kujinyima na kutoa sadaka kwa maskini hakutafua dafu, ikiwa kama mwamini hataweza kufungua moyo wake, ili kupokea wokovu ambao ni zawadi kutoka kwa Mungu na kamwe mwanadamu hawezi kumlipa Mungu kwa neema, baraka na wokovu anaomkirimia katika maisha yake! Waamini waondokane na kishawishi cha kudhani kwamba, wanaweza kuuza neema na wawe makini kabisa ili wasitumbukie katika uchu wa fedha na mali katika maisha na utume wao. Maisha ya Kikristo ni mwaliko wa kutoka kifua mbele, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; Kwa kuwahudumia maskini, wagonjwa na wale wote wanaoteseka: kiroho na kimwili. Yote haya yawe ni ushuhuda wa sadaka na maisha ya kujitolea kwa ajili ya Mungu, Kanisa na jirani!

Papa: Maisha ya Kikristo
11 June 2019, 15:22
Soma yote >