Kuishi kwa amani na Yesu ni kama kuwa na utulivu uliopo ndani ya kina cha bahari wakati juu yake kuna mawimbi ya kipiga huku na kule Kuishi kwa amani na Yesu ni kama kuwa na utulivu uliopo ndani ya kina cha bahari wakati juu yake kuna mawimbi ya kipiga huku na kule  (ANSA)

Misa ya Papa:Tunapewa amani ya kudumu na si ya dunia hii!

Wakati wa tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko katika Kanisa la Mtakatifu Marta mjini Vatican tarehe 21 Mei 2019,amejikita kutazama juu ya ahadi ya zawadi ya Yesu aliyowapa mitume wake kabla ya kurudi mbinguni yaani amani ambayo haitokani na dunia hii,bali na Roho Mtakatifu.Amani yake inadumu hata wakati wa majaribu na kutupatia ujasiri wa kwenda mbele na kuifanya mioyo yetu itabasamu na kutoa ucheshi kwa wengine.

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Wakati wa tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko katika Kanisa la Mtakatifu Marta mjini Vatican tarehe 21 Mei 2019, amejikita kutazama juu ahadi ya zawadi ya Yesu aliyowapati mitume wake, kabla ya kurudi  mbinguni yaani “amani”. Baba Mtakatifu Francisko anauliza, ni kwa namna gani ninaweza kujipatanisha na mahangaiko na mateso aliyopata Mtakatifu Paulo kama yanavyo elezwa leo hii katika sura za Matendo ya Mitume na amani ya Yesu ambayo anawaachia wafuasi wake katika maneno yake ya mwisho wakati wa karamu kuu: “ninawaachia amani, nawapa amani yangu” katika maneno yaliyosikika kwenye Injili ya Mtakatifu Yohane?

Heri ninyi mtakapo tukanwa na kuteswa…

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuanza na swali hilo anafafanua kuwa, amani ya Yesu inajikita kwa dhati ndani ya  maisha ya mateso na mahangaiko. Ni amani ambayo iko chini kabisa, na ni  ya kina katika mambo hayo yote. Ni amani ambayo hakuna mtu anaweza kuiondoa, ni amani ambayo ni zawadi, kama iliyopo ndani ya kina cha bahari kwa maana kuna utulivu na wakati huo huo juu yake kuna mawimbi. Kuishi kwa amani na Yesu ni kama kuwa na uzoefu huo wa utulivu  wa kina na ambao unabaki kwa muda mrefu hata wakati wa  majaribu, matatizo yote, hata katika mahangaiko.

Mkristo anabeba mabegani mwake maisha bila kupoteza amani

Mkristo anabeba mabegani mwake maisha bila kupoteza amani. Ni kwa namna hiyo tu inawezekana kutambua jinsi gani waliweza kuishi saa ya mwisho, watakatifu ambao hawakupoteza amani, hadi kufikia kushuhudia kuwa wao walikuwa wanakwenda kufiadini kama vile wanakwenda katika arusi. Hiyo ndiyo zawadi ya amani ya Yesu na ambayo hatuwezi kuipata kwa njia ya zana za kibinadamu, au kwenda kwa daktari kwa mfano au kumeza dawa. Amani ni jambo tofauti sana ambayo inapatikana tu kwa njia ya Roho Mtakatifu ndani mwetu na ambayo inakuja na nguvu yake  ndani mwetu.

Baba Mtakatifu Francisko akitoa mfano mmoja amesema: amani ni kama ya mtu yule mgojwa ambaye alikwenda kumtembelea hivi karibuni kwa maana  yeye alikuwa amezoea kufanya kazi sana na kwa bahati mbaya ameshikwa na ugonjwa na kusababisha asitishe yote, kila mpango, lakini akafanikiwa kubaki daima na amani. “Huyo ni mkristo”, amebainisha Baba Mtakatifu. Yesu anatufundisha, kwamba amani ni kwenda mbele katika maisha. Anatufundisha kuwa na uvumilivu. Uvumilivu ni neno ambalo kwa wakristo wanalitambua vizuri nini maana yake. Na kwa  mkristo uvumilivi maana yake  ni kubeba yote  juu ya mabega. Kuvumilia ni kubeba maisha juu ya mabega, matatizo, kazi kila kitu bila kupoteza amani. Na zaidi kubeba juu ya mabega na kuwa na ujasiri wa kwenda mbele! Hiyo inaeleweka zaidi hasa ikiwa kuna Roho Mtakatifu ndani ambaye anatupatia amani ya Yesu. Lakini iwapo mkristo unaishi na na ghadhabu za kiajabu na kupoteza amani, kuna jambo ambalo halifanyi kazi, amebainisha Baba Mtakatifu!

Amani inakufanya usipoteze hisia zako za ucheshi

Katika moyo uliojaa zawadi ya ahadi ya Yesu na siyo ile itokayo katika dunia au fedha katika benki, tunakabiliana na matatizo hata yaliyo mabaya sana na kwenda mbele na kuwa na uwezo zaidi, hasa wa kutufanya hata moyo uweze kuhisi tabasamu. Watu wanaoishi na uzoefu wa amani, kamwe hawapotezi hisia za ucheshi. Wanatambua kutoa ucheshi binafsi, hata kwa wengine na zaidi hata katika kivuli chao, wanachekeshwa na kila kitu… Hiyo ndiyo maana ya ucheshi ambao uko karibu na neema ya Mungu. Amani ya Yesu katika maisha ya kila siku, amani ya Yesu katika mahangaiko, hata katika maana ndogo ya ucheshi unatufanya tupumue vizuri! Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha akisema: “Bwana aweze utupatia amani hii inayotoka kwake Roho Mtakatifu,  amani hii  ambayo ni yake mwenyewe, ambayo inatusaidia kuvumilia na kupeleka mbele matatizo mengi ya maisha!

21 May 2019, 12:21
Soma yote >