Tafuta

Papa Francisko: Roho Mtakatifu anapyaisha ujana wa maisha ya kiroho; dhambi inamzeesha mtu kiroho! Papa Francisko: Roho Mtakatifu anapyaisha ujana wa maisha ya kiroho; dhambi inamzeesha mtu kiroho! 

Papa: Dhambi inazeesha; Roho Mt. anapyaisha maisha ya ujana!

Baba Mtakatifu anasema, Roho Mtakatifu ni mdau mkuu wa Uinjilishaji na msaidizi mkuu katika maisha na utume wa kanisa. Dhambi inamzeesha mwamini, lakini Roho Mtakatifu anapyaisha ujana wa maisha ya kiroho, kwa kuvuka vizingiti na hatimaye, kusonga mbele hata pale waamini wanapotakiwa kutoa sadaka kubwa yaani, kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Roho Mtakatifu anayo dhamana na wajibu wa kuwafundisha na kuwakumbusha waamini yale ambayo Kristo Yesu alifundisha wakati akiwa hapa duniani. Kristo Yesu aliwaahidia wafuasi wake kuhusu zawadi ya Baba wa milele, yaani Roho Mtakatifu. Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu! Habari ya dhambi kwa sababu hawakumwamini Mwana wa Mungu. Kwa habari ya haki kwa sababu Yesu anakwenda kwa Baba yake wa mbinguni na kwa habari ya hukumu kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 28 Mei 2019 amesema kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu katika Liturujia ya Neno la Mungu, wakati huu ambapo Kanisa linasubiri kusherehekea Siku kuu ya Bwana Kupaa Mbinguni. Yesu alitumia muda uliokuwa umebaki kwa ajili ya kutoa Katekesi ya kina kuhusu dhamana na wajibu wa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Wosia wa Yesu uliwafanya Mitume kuhuzunika sana mioyoni mwao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huzuni si mwelekeo sahihi wa maisha ya Kikristo, ndiyo maana, waamini wanapaswa kumkimbilia Roho Mtakatifu ili aweze kuwapatia nguvu itakayowapyaisha, ili waendelee kuwa vijana zaidi katika maisha ya roho!

Roho Mtakatifu ndiye anayeendelea kuwapyaisha katika maisha na utume wao, ili waendelee kuwa vijana zaidi. Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kubeba vyema Misalaba yao kama ilivyokuwa kwa akina Mtakatifu Paulo na Sila waliokuwa wameswekwa gerezani, lakini hata huko gerezani waliendelea kumwomba Mwenyezi Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu. Hata katika hali na mazingira haya ya mateso, bado Roho Mtakatifu aliendelea kuwasindikiza wafuasi wa Kristo na kwamba ni nguzo msingi katika maisha na utume wa Kanisa. Roho Mtakatifu ni mwenza wa safari ya maisha ya imani, anayeendelea kupyaisha ile ari na mwamko wa ujana.

Pale Mkristo anapoanza kuzeeka kutoka katika undani wa maisha yake ya kiroho, huo unakuwa ni mwanzo wa kuteleza na kuangukia dhambini, kwa sababu ule wito wa Ukristo unaanza kufifia anasema Baba Mtakatifu. Fumbo la maisha linafumbatwa katika furaha, uchungu na changamoto kama ilivyokuwa kwa akina Paulo la Sila, lakini bado waliendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili hata mle gerezani!Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ndio ushuhuda wa ujana wa maisha ya kiroho, unaowawezesha waamini kuendelea kuwa na matumaini, changamoto na mwaliko wa kujadiliana na Roho Mtakatifu kila kukicha kwa njia ya sala.

Roho Mtakatifu ni zawadi kubwa kutoka kwa Baba wa milele ambayo Kristo Yesu amewaachia wafuasi wake, ili kuwawezesha kusonga mbele kwa imani na matumaini. Hata katika udhaifu na mapungufu yake, mwamini bado anakirimiwa nguvu na Roho Mtakatifu ya kutubu na kumwongokea Mungu tayari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu zaidi. Dhambi inamzeesha mwamini, lakini Roho Mtakatifu anapyaisha ujana wa maisha ya kiroho, kwa kuvuka vizingiti na hatimaye, kusonga mbele hata pale waamini wanapotakiwa kutoa sadaka kubwa yaani, kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu amewataka waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimi neema ya upya wa maisha ya ujana wa kiroho, bila kupoteza ile furaha ya kutangaza na kushuhudia Injili, kwani huu ni wito na utambulisho wao!

Papa: Mahubiri
28 May 2019, 15:00
Soma yote >