Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Sala makini inasimikwa katika imani, ujasiri na udumifu! Papa Francisko: Sala makini inasimikwa katika imani, ujasiri na udumifu!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Sala inasimikwa katika imani, ujasiri na udumifu

Papa Francisko anasema, Sala inaweza kuwa ni kwa ajili ya kuomba ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu kama ilivyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu na watu kama Mtumishi wa Mungu Mussa, Abramu, Anna na Mama yake Samuel bila kumsahau yule mwanamke Mkananayo ambaye kwa njia uthabiti wa moyo, aliweza kupata neema ya mtoto wake kuponywa na Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waamini wanapaswa kusali kwa imani na ujasiri pamoja na kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, kama sehemu muhimu ya kipindi cha Kwaresima kinachokazia pia: toba, kufunga na wongofu wa ndani pamoja na matendo ya huruma, kama kielelezo cha imani tendaji! Sala inaweza kuwa ni kwa ajili ya kuomba ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu kama ilivyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu na watu kama Mtumishi wa Mungu Mussa, Ibrahimu, Anna na Mama yake Samuel bila kumsahau yule mwanamke Mkananayo ambaye kwa njia uthabiti wa moyo, aliweza kupata neema ya mtoto wake kuponywa na Kristo Yesu!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 4 Aprili 2019 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Waisraeli walipoona kwamba Musa anakawia kushuka, wakajitengenezea ndama wa dhahabu na kuanza kumwabudu kuwa ndiye mungu aliyewakomboa kutoka utumwani Misri. Wakatoa dhabihu, wakaleta sadaka za amani, watu wakala, wakanywa na kucheza! Mambo haya yakawasha hasira ya Mungu akataka kuwafyekelea mbali kutoka kwenye uso wa dunia!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Musa akamsihi sana Mwenyezi Mungu, akiomba msamaha kwa ajili yao kwa kumkumbusha matendo makuu aliyowafanyia Waisraeli, ili aweze kugeuka na kughairi uovu juu ya watu wake. Akamkumbusha watumishi wake waaminifu Ibrahimu, Isaka na Israeli aliowaahidia kukizidisha kizazi chao na kukipatia nchi ijaayo maziwa na asali, ili wapate kuirithi. Mwenyezi Mungu akamwambia Musa angemfanya yeye kuwa taifa kuu! Lakini Musa aliendelea kuwaombea watu wake kiasi cha kumwekea Mungu masharti, kwamba, urithi huu apewe pamoja na watu wake, vinginevyo, hauna maana kwake!

Huu ndio mfano uliooneshwa pia na Ibrahimu wakati hasira ya Mungu ilipowaka dhidi ya mji wa Sodoma, akataka kuukoa kwa kumwomba Mwenyezi Mungu! Alianzia idadi ya watu 30 hadi kufikia mtu mmoja mwenye haki! Mwishoni ikaonekana kuwa familia ya Ibrahimu peke yake ndiyo iliyohesabiwa haki mbele ya Mungu. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kuna mifano mingi katika Maandiko Matakatifu, kama Mama yake Samueli, aliyekuwa anapambana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala, akiomba apate mtoto, kiasi hata cha kuonekana kuwa kama mlevi.

Hata katika Injili kuna mwanamke jasiri na mwenye imani thabiti, yaani Mwanamke Mkananayo aliyeonesha ujasiri wa kiimani akimtaka Kristo Yesu aweze kumwokoa binti yake, hata kama hakuwa mtoto wa nyumba ya Israeli na wala haikuwa vyema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa! Lakini, yule mwanamke jasiri kwa uthabiti kabisa bila kupepesa macho akamwambia Kristo Yesu kwamba, hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao! Yesu kwa kuona imani kubwa kiasi hiki, akamponya binti yake tangu saa ile!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, yote hii ni mifano ya sala inayotolewa kwenye Maandiko Matakatifu, kwani ujasiri na imani thabiti, vinahitajika katika sala. Kuna umuhimu wa kudumu katika sala, hadi kieleweke bila ya kukata tamaa. Kwa njia ya imani thabiti, waamini wanapomwomba Mungu anawakirimia kadiri ya mapenzi yake! Sala si wingi wa maneno na litania ya matatizo yanayopelekwa mbele ya Mwenyezi Mungu, lakini zaidi ni ujasiri, imani thabiti na kujiaminisha mbele ya Mungu.

Baba Mtakatifu anawahakikishia kwamba, kwa hakika Kristo Yesu anawasikiliza na ndiye Mwombezi wao mkuu, kwani ameketi kuume kwa Baba yake wa mbinguni, akiwaombea daima! Kristo Yesu anasikiliza sala za waja wake, wanapomkimbilia kwa imani thabiti! Waamini watambue kwamba, wanaposali, wanaungana na Kristo Yesu, anayewasilisha sala zao mbele ya Mungu! Kwa hakika Kristo Yesu ni ujasiri na usalama wa watu wake, tayari kuwaombea kwa Baba yake wa mbinguni.

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha mahubiri yake, kwa kuwataka waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia neema ya kuwa na ujasiri na imani thabiti wakati wa sala. Sala ya kweli itolewe mbele ya Kristo Yesu kwa ari, moyo mkuu na imani thabiti! Ibada hii ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, imehudhuriwa pia na Rais Sergio Mattarella wa Italia!

Papa: Sala
04 April 2019, 15:17
Soma yote >