Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu anawataka waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Roho Mtakatifu ili waweze kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu! Baba Mtakatifu anawataka waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Roho Mtakatifu ili waweze kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu!  (ANSA)

Papa: Mpeni Roho Mtakatifu nafasi katika maisha yenu!

Ni Roho Mtakatifu anayeweza kuwainua na kuwapandisha juu kutoka katika makaburi ya maisha na nyoyo zao. Huu ndio ujumbe wa Pasaka kwamba, kuna haja ya kuzaliwa kutoka juu kwa maji na Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni mdau mkuu katika maisha ya Wakristo, ndiye anayewaongoza na kuwasindikiza hatua kwa hatua; anawapatia nguvu ya kufanya mageuzi ya maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Roho Mtakatifu ndiye kiongozi mkuu wa maisha ya waamini, anayeweza kuwasaidia kuzaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu na hivyo kuondokana na dhambi pamoja na mapungufu yao wa kibinadamu. Mwenyezi Mungu anatambua fika changamoto zinazowasibu waja wake, ndiyo maana akamtuma Roho Mtakatifu, ili aweze kuwafundisha, kuwakumbusha na kuwategemeza katika mambo msingi ya maisha. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 30 Aprili 2019 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican.

Mahubiri ya Baba Mtakatifu yamejikita zaidi katika maswali na majibu kati ya Kristo Yesu na Nikodemo ambaye alishangaa kuhusu mtu kuzaliwa mara ya pili! Lakini, Yesu anakaza kusema, mtu asiyezaliwa kwa maji na kwa Roho hawezi kuingia katika Ufalme wa Mungu. Lazima waamini wazaliwe upya kutoka juu, ujumbe mahususi katika kipindi hiki cha Pasaka ya Bwana. Tangu siku ile ya kwanza ya Juma, Kristo Mfufuka alipowatokea Mitume wake, aliwavuvia Roho Mtakatifu, nguvu inayowawezesha waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka!

Bila Roho Mtakatifu waamini si mali kitu! Maisha na utume wa Kikristo unafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanatoa nafasi ya pekee kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwasindikiza vyema katika maisha yao! Ni Roho Mtakatifu anayeweza kuwainua na kuwapandisha juu kutoka katika makaburi ya maisha na nyoyo zao. Huu ndio ujumbe wa Pasaka kwamba, kuna haja ya kuzaliwa kutoka juu kwa maji na Roho Mtakatifu.

Roho Mtakatifu ni mdau mkuu katika maisha ya Wakristo, ndiye anayewaongoza na kuwasindikiza hatua kwa hatua; anawapatia nguvu ya kufanya mageuzi ya maisha, anapambana na hatimaye, kuhakikisha kwamba, waamini wanashinda vita yao. Kristo Yesu anakaza kusema katika Injili kwamba, hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani Mwana wa Adamu. Kristo Yesu ndiye anayewapatia waja wake Roho Mtakatifu, zawadi ya Baba wa mbinguni kwa njia ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu.

Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu amewasihi waamini kuomba neema ya kutambua umuhimu wa uwepo wa Roho Mtakatifu katika maisha yao, ili waweze kufikiri na kutenda kadiri ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Ni wajibu wa waamini kujiuliza Je, Roho Mtakatifu anachukua nafasi gani katika maisha yao? Roho Mtakatifu ni mwandani wa mwamini katika hija ya maisha yake hapa duniani!

Papa: Roho Mtakatifu
30 April 2019, 15:08
Soma yote >