Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kukumbuka wema, ukarimu na upendo wa Mungu katika maisha yao! Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kukumbuka wema, ukarimu na upendo wa Mungu katika maisha yao!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Kumbukeni wema na ukarimu wa Mungu kwenu!

Kipindi cha Kwaresima ni fursa kwa waamini kujizatiti katika kujenga utamaduni wa kumsikiliza Mungu, ili kupyaisha kumbu kumbu ya wema na ukarimu wa Mungu aliowatendea watu wake katika historia yao. Kwa bahati mbaya, anasema Baba Mtakatifu Francisko, watu ni wepesi sana kusahau historia ya walikotoka na kudhani kwamba, mafanikio yote waliyopata ni kwa nguvu zao wenyewe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Mwenyezi Mungu alimjalia Musa kuwaandaa watu wake ili waweze kuingia katika Nchi ya ahadi iliyojaa maziwa na asali, lakini watu hawa walitakiwa kwanza kabisa kumrudia Mwenyezi Mungu kwa utii na unyenyekevu; kwa kuyashika maagizo na Amri zake zilizoandikwa kwenye Kitabu cha Torati, kwa kumwelekea Mwenyezi Mungu kwa moyo na akili zao zote! Mwenyezi Mungu aliweka mbele ya macho yao changamoto ya kukumbatia maisha au kuangamia kwa mauti na kifo! Lakini, Mwenyezi Mungu anawaachia watu wake uhuru wa kuamua.

Kumbe, hii ni nafasi ya kufanya tafakari ya kina kuhusu: Moyo kulegea na kuanza kurejea nyuma; kwa kutomsikiliza Mungu na kwa kuabudu miungu wengine! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 7 Machi 2019, baada ya Jumatano ya Majivu, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, pale moyo unapoghafirika, ukalegea na mtu kuanza kurudi nyuma na hatimaye, kutumbukia katika uovu ni hatari sana kwa maisha ya hadhara!

Ni hatari kwa mtu mwenyewe pamoja na usalama wa watu wengine. Hii ni tabia ya kushindwa kusikiliza kwa makini na matokeo yake ni kutumbukia na hatimaye, kumezwa na malimwengu! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kuna wakati hata waamini wanakuwa na moyo mgumu kama wa jiwe kiasi hata cha kushindwa kumsikiliza Mwenyezi Mungu. Kuna wakati Mwenyezi Mungu anafanya ishala mbali mbali, lakini watu wamefunga macho na masikio yao, kiasi hata cha kushindwa kuziona. Sababu kubwa ni kwamba, hawa ni watu waliomezwa na malimwengu na wanapenda kuabudu vitu badala ya Mungu aliyewaokoa kutoka utumwani. Kipindi cha Kwaresima ni safari kuelekea katika nchi ya ahadi, ili kukutana na Kristo Yesu, Mfufuka!

Kipindi cha Kwaresima, iwe ni fursa kwa waamini kujizatiti katika kujenga utamaduni wa kumsikiliza Mwenyezi Mungu, ili kupyaisha kumbu kumbu ya wema na ukarimu aliowatendea watu wake katika historia ya maisha yao. Kwa bahati mbaya, anasema Baba Mtakatifu Francisko watu ni wepesi sana kusahau historia ya walikotoka na kudhani kwamba, mafanikio yote waliyopata ni kwa nguvu zao wenyewe. Kwaresima kiwe ni kipindi cha kumwomba Mwenyezi Mungu awajalie waamini wake, neema ya kuwa na kumbu kumbu hai ya hija ya maisha ambayo Mwenyezi Mungu ameamua kuambatana nao! Pale mambo yanapokwenda vyema, binadamu anakuwa na tabia ya kusahau kwa wepesi wema na neema ya Mungu, kiasi hata cha kushindwa kuisikiliza sauti ya Mungu anayezungumza kutoka katika undani wa moyo wa mtu!

Baba Mtakatifu anasema, hata Waisraeli katika safari ya maisha yao walipoteza kumbu kumbu kwamba, ni Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaokoa kutoka utumwani kwa mkono wenye nguvu! Ni Waisraeli hao hao walioanza kumlilia na kumnung’unikiwa Mungu kwa kukosa chakula na maji jangwani, kiasi hata cha kuanza kukumbuka “masufuria ya nyama na makapu ya vitunguu swaumu! Walisahau kwamba, walikua wanakula na kushiba lakini wakiwa kwenye kongwa la utumwa. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya kumbu kumbu endelevu ya historia ya maisha na uwepo wa Kristo Yesu katika maisha yao, ili kuwa na ari na mwamko wa kusonga mbele, pasi ya kukata tamaa na kuanza kurejea tena nyuma na kuanza kuabudu miungu wa uwongo!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, tabia ya watu kupenda kuabudu miungu wa uwongo ni kutokana na kukosa kumbu kumbu, kiasi hata cha kusahau uwepo wa Mungu katika maisha yao. Kipindi cha Kwaresima, kiwawezeshe waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia neema ya kumbu kumbu, ili kutambua tena na tena upendo wa Mungu katika maisha yao! Kiri ya imani ambayo waamini wanapaswa kuikumbuka daima ni kwamba, Kristo Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kristo Yesu anaendelea kuwasindikiza waja wake katika safari ya maisha yao, hadi siku ile watakapofika mbele yake kwa ajili ya hukumu ya wazima na wafu. Kumbe, neema ya kutunza kumbu kumbu ni muhimu sana katika kipindi hiki cha Kwaresima!

Papa: Kumbu kumbu
07 March 2019, 15:17
Soma yote >