Tafuta

Papa Francisko asema, hata leo hii bado kuna magharika yanayoendelea kumwaandama watu wa Mungu katika maisha yao! Papa Francisko asema, hata leo hii bado kuna magharika yanayoendelea kumwaandama watu wa Mungu katika maisha yao!  (Vatican Media)

Papa: bado watu wanaandamwa na magharika katika maisha!

Papa Francisko anasema, hata leo hii bado kuna matatizo na changamoto mbali mbali. Kuna umaskini wa hali na kipato; kuna watoto wanaoteseka kwa njaa na utapiamlo wa kutisha; kuna watu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia; kuna maelfu ya watu wanaofariki dunia vitani! Kuna watoto ambao hawana nafasi ya kupata malezi na makuzi katika mazingira ya amani na utulivu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa kawaida Mwenyezi Mungu anapenda kwa dhati kabisa kutoka katika undani wa moyo wake na wala si katika nadharia. Ni wajibu wa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia kipaji cha kuweza kulia na kuomboleza, pale mwanadamu anapokumbwa na majanga asilia, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale, Gharika kuu ilipotokea na watu wengi wakapoteza maisha yao! Leo hii, mwanadamu anakumbana na aina mbali mbali za majanga asilia; dhuluma, nyanyaso pamoja na vita!

Kuna watu wanakufa kutokana na vita sehemu mbali mbali za dunia kana kwamba, si mali kitu! Watu wanarushwa mabomu, utadhani ni peremende za kuwagawia watoto wa shule! Hapa kuna changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na moyo wa huruma na upendo, ili kutambua kwamba, watu wameumbwa kwa sura na mfao wa Mungu. Wanayo haki ya kukasirika, kuhuzunika na kusonekana kama alama ya mshikamano kati ya watu na Mwenyezi Mungu na kati yao wao wenyewe!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 19 Februari 2019, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu alikita tafakari yake kwenye Gharika kuu, Mwenyezi Mungu alipotaka kumfutilia mbali mwanadamu, lakini Nuhu akapata neema machoni pa Mungu. Yote haya yanaonesha kuwa Mwenyezi Mungu anawapenda watu wake kwa dhati na wala si kwa nadharia, wala wazo la kufikirika! Mwenyezi Mungu anapenda na kufariji kwa moyo, lakini anapotoa adhabu, anaitoa kweli kweli, lakini anayeteseka zaidi ni Mwenyezi Mungu kwani ni mwingi wa huruma na mapendo!

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, hata nyakati hizi si kwamba, mambo yamebadilika sana kuliko ilivyokuwa wakati wa Gharika kuu. Hata leo hii bado kuna matatizo na changamoto mbali mbali. Kuna umaskini wa hali na kipato; kuna watoto wanaoteseka kwa njaa na utapiamlo wa kutisha; kuna watu wanaoteseka na kunyanyasika sehemu mbali mbali za dunia; kuna maelfu ya watu wanaofariki dunia vitani! Kuna watoto ambao hawana nafasi ya kupata malezi na makuzi katika mazingira ya amani na utulivu. Kuna watoto yatima na wale wanaolazimishwa kupelekwa mstari wa mbele kama chambo cha vita! Haya ni magharika yanayoendelea kumwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo!

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa mahubiri yake, anawaalika waaamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie kuwa na moyo unaofanana na moyo wa Mungu, ili kuguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya watu wengine! Waamini waombe neema ya kuwa na moyo kama kibinadamu kama ule wa Kristo Yesu, ili, hatimaye, waweze kuwa ni vyombo vya faraja. Leo Gharika kuu linaweza kuonekana katika vita ambayo waathirika wakuu ni “Akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” pamoja na watoto ambao hawana nyenzo za kuwasaidia kusonga mbele. Watu wote hawa wafarijiwe na Mwenyezi Mungu katika safari ya maisha yao. Magharika mbali mbali katika maisha ya mwanadamu ni kazi ya Shetani, Ibilisi anayetaka kuharibu kazi ya uumbaji iliyotekelezwa na Mwenyezi Mungu.

Papa: Gharika la Mwanadamu
19 February 2019, 13:53
Soma yote >