Tafuta

Vatican News
Toba na wongofu wa ndani vinafumbatwa katika ufukara, upole na upendo. Toba na wongofu wa ndani vinafumbatwa katika ufukara, upole na upendo.  (Vatican Media)

Toba na wongofu wa ndani vinafumbatwa katika ufukara na upendo!

Papa Francisko anakazia: Ufukara, unyenyekevu na upendo ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na wale wote wanaotumwa na Kristo Yesu, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Kwa bahati mbaya, kuna wale walioteuliwa na hatimaye kutumwa, badala ya kujikita katika mambao haya makuu matatu wamekuwa ni watu wanaotafuta masilahi yao binafsi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mchakato wa toba na wongofu wa ndani unafumbatwa kwa namna ya pekee katika moyo wa ufukara; fadhila ya unyenyekevu na upendo. Unyenyekevu unamwezesha mwamini kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, ili kuomba huruma, msamaha na utakaso wa dhambi, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Unyenyekevu ni tunda la roho linalomwezesha mwamini kumfuasa Kristo Yesu kwa ari na moyo mkuu tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 7 Februari 2019 amekazia dhana ya uponyaji, kama sehemu ya tafakari kutoka katika Injili ya Marko 6:1-13 inayoelezea jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyowatuma Mitume wake wawili wawili, ili kuwaganga na kuwaponya watu kama alivyotumwa mwenyewe hapa duniani, ili kwa kuwaganga na kuwaponya watu, waweze kuwa tena na maisha mapya.

Mafundisho ya Yesu ni dawa iliyokuwa inawaponya watu, kwa kuwataka kwanza kabisa kutubu na kuongoka! Kwa njia hii, waamini wanaweza kumfungulia Mwenyezi Mungu malango ya maisha yao, ili aweze kuwaganga na kuwaponya. Wongofu wa ndani ni mchakato wa kumfungulia Mungu malango ya maisha, ili aweze kuingia na hatimaye, kumganga na kumponya mwamini. Lakini, ikiwa kama wamini amefunga malango ya moyo wake na huku anaendelea kuteketea kwa ndani ni sawa nakaburi ambalo limepakwa nje chokaa, lakini kwa ndani kuna mifupa!

Waamini wanapaswa kujisikia ndani mwao kwamba, wanaalikwa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Ili kutangaza na kushuhudia wongofu huu, mchungaji anapaswa kushikamana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yake, kwa kumpatia nafasi ya kwanza badala ya kujitaabisha kuchukua: chakula, mkoba na fedha ya kibindoni. Kwa maneno mengine, wafuasi wa Kristo Yesu wanapaswa kuambata ufukara wa maisha, ili kamwe wasitumbukie na hatimaye, kumezwa na malimwengu kwa kupenda fedha, anasa na umaarufu usiokuwa na mashiko wala mvuto kama anavyofafanua Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anakazia mambo makuu matatu: ufukara, unyenyekevu na upendo ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na wale wote wanaotumwa na Kristo Yesu, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Kwa bahati mbaya, kuna wale walioteuliwa na hatimaye kutumwa, badala ya kujikita katika mambao haya makuu matatu wamekuwa ni watu wanaotafuta masilahi yao binafsi. Kwa njia hii, Baba Mtakatifu anakaza kusema hakuna mtu atakayeweza kuponywa wala kuwaponya wengine, kwa kumfungulia Kristo Yesu mlango ya maisha yao kusudi waingie! Kwa njia ya unyenyekevu, Neno wa Mungu amefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake, katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi. Ufukara una ambata unyenyekevu na upendo wa dhati, mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kumfungulia malango ya nyoyo zao!

Madaraka na mamlaka aliyo nayo mtu hayana budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu. Kwa njia ya wongofu wa ndani, kiongozi anaweza kutambua uwepo wa Shetani pamoja na dhambi! Kwa kuongozwa na dhamiri nyofu, kiongozi anapaswa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake! Ufukara, unyenyekevu na upole, unampatia mwamini mamlaka na madaraka ya kusema “tubuni” yaani “mfungulieni Mungu malango ya maisha yenu”, ili aweze kuwasamehe na kuwataka dhambi zenu!

Baba Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake kwa kusema, kila mwamini anaweza kupona, ikiwa kama ataweza kumruhusu Mwenyezi Mungu aweze kumpatia faraja katika safari ya maisha yake. Nguvu ya mamlaka na madaraka vinaweza kuwaponya watu kwa neno na ushauri makini; kwa uvumilivu na subira; kwa tabasamu na unyenyekevu wa moyo! Waamini wote wanahitaji kuponywa na magonjwa mbali mbali ya maisha ya kiroho yanayowaandama. Ni kwa njia hii, hata wao wanaweza kuwaponya jirani zao. Hata leo hii Kristo Yesu anaendelea kuganga na kuwaponya watu kwa njia ya: ufukara, unyenyekevu na upole pamoja na kuwapatia nguvu na mamlaka ya kumwadabisha Shetani. Waamini wa wagangane na kuponyana; watoe pia nafasi kwa Kristo Yesu ili aweze kuwanganga na kuwaponya.

Papa: Ibada ya Misa Takatifu
07 February 2019, 14:29
Soma yote >