Tafuta

Changamoto kuhusu hukumu ya mwisho inajibiwa kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Changamoto kuhusu hukumu ya mwisho inajibiwa kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Maswali tete yanajibiwa kwa ushuhuda wa imani!

Papa Francisko anasema, maswali haya yanajibiwa kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili: Kwa kuwalisha wenye njaa, kuwatembelea wafungwa; kwa kutenda haki! Maswali haya magumu na tete yawe ni changamoto kwa kila mwamini katika maisha yake na kwamba, wajitahidi kuyatibu kila mtu kadiri ya hali na mazingira yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Adamu uko wapi? Bwana akamwambia Kaini, “Yuko wapi Habili ndugu yako?” Haya ni maswali tete ambayo Mwenyezi Mungu alimuuliza Adamu na Kaini katika Kitabu cha Mwanzo, kwenye Agano la Kale. Ni maswali katika mtindo huu, ambayo Mwenyezi Mungu anaendelea kuwauliza watu hata katika ulimwengu mamboleo! Yuko wapi ndugu yako mgonjwa, mfungwa, mwenye njaa na kiu ya haki. Haya ni maswali mintarafu Injili ya Mathayo, Sura 25.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 18 Februari 2019 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican. Kimsingi haya ni maswali tete sana katika maisha ya binadamu na majibu yake yanamnyong’onyesha mtu kama ilivyokuwa kwa Kaini aliyejibu kwa unyonge mkubwa, Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Kaini anataka kukumbia sura na uwepo wa Mungu na kusahau kwamba, mbio za sakafuni huishia ukingoni!

Haya ndiyo maswali mazito ambayo Kristo Yesu aliwauliza akina Petro mtume, Je, unanipenda? Je, watu husema kuwa mimi ni nani? Je, ndugu yako yuko wapi? Maswali magumu ambayo yanadai ushuhuda wa maisha wenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu anakaza kusema, haya ni maswali yanayopaswa kujibiwa kutoka katika undani wa mtu na wala si kwa kujisikia tu! Ni maswali yanayogusa uhalisia wa maisha ya watu: wagonjwa, watu wenye njaa na kiu ya haki; wafungwa gerezani; watu wanaoteswa na kunyanyaswa; watu wanaotaka kuona haki ikitendeka katika maisha yao!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, maswali haya yanajibiwa kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kwa kuwalisha wenye njaa, kuwatembelea wafungwa; kwa kutenda haki! Maswali haya magumu na tete yawe ni changamoto kwa kila mwamini katika maisha yake na kwamba, wajitahidi kuyajibu kila mtu kadiri ya hali na mazingira yake. Ndugu na jirani yako ni wale wote wanaoteseka kutokana na sabababu mbali mbali kama anavyobainisha Mwinjili Mathayo katika Sura ya 25 kuhusu “Hukumu ya Mwisho”.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni muhtasari wa Mafundisho Jamii ya Kanisa ambayo yanapaswa kuwa ni dira na mwongozo wa kuona matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo, tayari kuzipatia ufumbuzi kwa mwanga wa tunu msingi za Kiinjili! Uko wapi? Ndugu yako yuko wapi? Ni maswali ambayo yanataka kumkwamua mwamini kutoka katika maisha ya giza na utupu, ili kumwonesha njia ya mwanga wa kufuata kadiri ya Mafundisho ya Kristo Yesu.

Vinginevyo, anasema Baba Mtakatifu, mwamini atateleza na kutumbukia katika dhambi na ubaya wa moyo. Adamu aliogopa kukutana na Mwenyezi Mungu mubashara kwa sababu ya aibu ya dhambi iliyoingia maishani mwake! Kwa bahati mbaya, pengine hata leo hii, inakuwa ni vigumu sana kwa watu kuona aibu kutokana na mazoea! Watu wanashindwa kuona mateso na mahangaiko ya jirani zao; kwa sababu ya mazoea au hata wakati mwingine, hawataki kuona na kushuhudia ukweli. Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni mwa mahubiri yake, anawaalika waamini kujibu maswali yote haya kadiri ya ukweli na uhalisia wa maisha; kwa furaha na unyoofu wa moyo!

Papa: Mahubiri
18 February 2019, 14:14
Soma yote >