Papa Francisko: Upendo wa kweli unafumbatwa katika kumpenda Mungu, Jirani na kutekeleza Amri za Mungu katika maisha Papa Francisko: Upendo wa kweli unafumbatwa katika kumpenda Mungu, Jirani na kutekeleza Amri za Mungu katika maisha  (Vatican Media)

Papa Francisko upendo wa kweli: Mungu, jirani na Amri za Mungu

Shetani ni baba wa utengano unaokita mizizi yake katika maisha ya mtu mmoja mmoja, familia na hatimaye, “kusambaa kama moto mabua katika jamii”. Upendo kwa Mungu na jirani ni kielelezo cha upendo thabiti unaopaswa kushuhudiwa na Wakristo anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Upendo wa kweli unamwilishwa katika upendo kwa Mungu, jirani pamoja na kutekeleza Amri za Mungu, kama kielelezo cha imani ya kweli kwa Mwana mpendwa wa Mungu, yaani Kristo Yesu! Kwa maana kila kitu kilicho zaliwa na Mungu huushinda ulimwengu, kwa njia ya imani thabiti! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 10 Januari 2019, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, kwa kuwataka waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia nguvu ya kupenda kwa dhati kwa sababu imani kwa Kristo Yesu imeushinda ulimwengu pamoja na Shetani baba wa uwongo na asili ya kinzani na migawanyiko kati ya watu!

Mtakatifu Yohane anawataka waamini kukita mapambano yao katika imani, ili kuweza kumshinda Shetani, anayewalaghai watu kwa kutaka kuonekana kwa nje, bila kuwa na msingi thabiti wa maisha ya kiroho, matokeo yake ni watu kutaka umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko. Mtu anayemwamini na kumshuhudia Mwana wa Mungu anayo nguvu ya maisha ya kiroho na kwamba, hawezi kuteteleza kamwe, ikilinganishwa na nguvu ya Shetani anayependa kuwaghilibu watu kwa mambo ya kidunia.

Kwa waamini ambao wanaongozwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, daima watajitahidi kutenda mema na kwamba, upendo kwa jirani unakuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha yao ya kila siku. Shetani ni baba wa utengano unaokita mizizi yake katika maisha ya mtu mmoja mmoja, familia na hatimaye, “kusambaa kama moto mabua katika jamii”. Upendo kwa Mungu na jirani ni kielelezo cha upendo thabiti unaopaswa kushuhudiwa na Wakristo anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Waamini wajifunze kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea jirani zao kama kielelezo cha kwanza cha upendo. Hawa wanaweza kuwa ni majirani wanaowapenda au wale wanaodhani kwamba, ni maadui zao! Jambo la pili anasema Baba Mtakatifu, waamini wamwombe Roho Mtakatifu ili aweze kuwaponya na madonda ya wivyu usiokuwa na mvuto wa mashiko, ili waweze kukua na hatimaye, kukomaa katika upendo wa dhati! Umbea na uzandiki ni sumu hatari sana kwa ushuhuda wa maisha ya Kikristo, kwani ni sawa na upanga wenye makali kuwili. Waamini wajifunze kushinda malimwengu, kwa kwa njia ya imani thabiti kwa Mwenyezi Mungu. Upendo kwa Mungu na jirani pamoja na kushika Amri za Mungu ni kielelezo makini cha mwamini anayepambana na Shetani, ili kamwe asimezwe na malimwengu!

Papa: Upendo: Mungu & Jirani
10 January 2019, 15:16
Soma yote >