Tafuta

Papa Francisko: Heri za Mlimani ni dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo! Papa Francisko: Heri za Mlimani ni dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo! 

Papa Francisko: Heri za Mlimani ni dira na mwongozo wa Kikristo!

Tabia ya baadhi ya waamini kupenda kuwashutumu jirani zao; watu kutaka kumezwa na malimwengu pamoja na ubinafsi ni mitindo ya maisha inayosigana kimsingi na Ukristo. Kuna baadhi ya watu wanapenda kuwagawa watu kwa makundi, wema na wabaya; kielelezo cha kukosa haki mbele ya wengine na kwamba, hawa ni waamini wanaotaliwa na nguvu za Shetani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtindo wa maisha bora ya Mkristo yanafumbatwa katika Heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake! Kuna baadhi ya waamini wanajigamba kuwa ni Wakristo kweli kweli, lakini ukiangalia mtindo wa maisha na mwenendo wao ni kinyume kabisa cha mafundisho ya Kristo! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 21 Januari 2019 wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, wakati Kanisa likiadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Agnes, Bikira na Shahidi.

Baba Mtakatifu amefafanua kwa kina na mapana kuhusu kufunga, upya na ukuukuu wa maisha, kwa kukazia umuhimu wa kutunza divai mpya katika viriba vipya kama anavyosema Kristo Yesu katika Injili kama ilivyoandikwa na Mk. 2: 18-22. Tabia ya baadhi ya waamini kupenda kuwashutumu jirani zao; watu kutaka kumezwa na malimwengu pamoja na ubinafsi ni mitindo ya maisha inayosigana kimsingi na Ukristo. Kuna baadhi ya watu wanapenda kuwagawa watu kwa makundi, wema na wabaya; kielelezo cha kukosa haki mbele ya wengine na kwamba, hawa ni waamini wanaotaliwa na nguvu za Shetani, kwani Shetani kadiri ya Maandiko Matakatifu ndiye baba wa shutuma dhidi ya wengine!

Kristo Yesu katika maisha na utume wake, daima alikemea tabia ya watu kuwashutumu jirani zao na badala yake, watu wawe na ujasiri wa kuangalia undani wa maisha yao, tayari kutoa boriti lililoko machoni pao, ili hatimaye, kuona kibanzi cha jirani zao. Yesu aliwataka wafuasi wake kujitenga na unafiki kwa kuwaambia kwamba, asiyekuwa na dhambi awe wa kwanza kurusha jiwe! Tabia ya kuishi kwa kuchambua na kutafuta makossa ya wengine si Ukristo hata kidogo. Hii ni tabia ya watu kumezwa na malimwengu. Hawa ndio wale waamini wanaoweza kukiri imani kwa kichwa, lakini, katika ukweli wa mambo ni watu waliomezwa na malimwengu!

Ni watu wanaotaka kujikweza, ni watu wenye kiburi na ukiangalia kwa karibu sana ni watu ambao kimsingi wana uchu wa mali, fedha na madaraka! Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kristo Yesu anawakirimia waja wake divai mpya, lakini kwa bahati mbaya, wengi hatawaki kutubu na kuongoka. Ni watu wanaotaka kujionesha mbele ya watu kuwa ni waamini wa kweli na kusahau kwamba, “debe tupu kamwe haliachi kutika”. Waamini wanapaswa kujifunza na kuiga mifano kutoka kwa Kristo Yesu, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, walionesha unyenyekevu wa hali ya juu katika maisha na utume wao!

Leo hii katika maisha ya kijumuiya kuna mtindo mwingine wa maisha unaofumbatwa katika ubinafsi na tabia ya kutoguswa na mahangaiko ya jirani! Hawa ni watu wanaojitaabisha kuchochea vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; ni mashuhuri kupandikiza magonjwa na kuona watu wanateseka! Huu ni unafiki ambao daima Kristo Yesu ameukemea katika maisha! Baba Mtakatifu anawataka waamini kuondokana na mitindo ya maisha inayokwenda kinyume cha Heri za Mlimani. Kamwe wasipende kuwashutumu jirani zao, kumezwa na malimwengu pamoja na ubinafsi. Heri za Mlimani ni mtindo mpya wa maisha ya Wakristo unaofumbatwa katika uhalisia wa maisha na kamwe haitoshi kukiri imani au kusali Sala ya Baba Yetu kwa kichwa, ikiwa kama Heri za Mlimani hazina nafasi katika uhalisia wa maisha yao.

Papa: Heri za Mlimani

 

 

21 January 2019, 13:44
Soma yote >