Vatican News
Misa katika Kanisa la Mtakatifu Marta:je mimi ninafanya nini kwa ajili ya amani ya dunia? Misa katika Kanisa la Mtakatifu Marta:je mimi ninafanya nini kwa ajili ya amani ya dunia?   (Vatican Media)

Papa:tafuta amani rohoni,familia na duniani bila kuumiza wengine

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Misa asubuhi katika Kanisa la Mtakatifu Marta mjini Vatican anakumbusha kuwa, kipindi cha majilio ni kipindi cha kujenga amani katika roho binafsi, ndani ya familia na katika dunia, bila samahani kwa kufanya vita na kuumiza wengine

Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Kujiandaa katika Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Bwana ni kutafuta kila njia ili kujenga amani katika roho binafsi, katika familia na katika dunia. Kufanya amani kwa njia ndogo ni kama kuiga Mungu kwa unyenyekevu, bila kuwasengenya wengine au kuwaumiza. Ndiyo ushauri wa Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Misa Takatifu, siku ya Jumanne asubuhi, tarehe 4 Desemba 2018, katika Kanisa la Mtakatifu Marta mjini Vatican. Tafakari yake, imejikita kuanzia somo la kwanza katika Liturujia ya siku (Isa 11,1-10) na Injili Lk 10,21-24).

Bwana atafanya amani

Katika maneno ya Isaya, Baba Mtakatifu anasema, kuna ahadi inayoonesha kwa jinsi gani itakuwa kipindi cha mwisho atakapo kuja Bwana: “Bwana atafanya amani, na kila kitu katika amani”. Isaya anaelezea vema kwamba: “Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kimono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza”. Baba Mtakatifu anasema kuwa, Yesu analeta amani yenye uwezo wa kubadili maisha na historia na ndiyo maana anaitwa mfalme wa amani kwa sababu anataka kutoa amani hiyo.

Kuomba Mfalme wa amani ili kutuliza amani ya roho

Kipindi cha Majilio ni kipindi mwafaka; ni kipindi cha kujiandaa katika ujio wa Mfalme wa amani. Ni kipindi cha kuwa na amani, Baba Mtakatifu anasisitiza. Hiyo ina maana kwamba: zaidi ya yote ni kutafuta amani kuanzia katika roho binafsi. Mara nyingi sisi siyo watu wa amani, kwa maana tumejaa na wasiwasi, uchungu na bila kuwa na matumaini. Swali ambalo Bwana anauliza: je, roho yako ikoje leo? je, unayo amani? na kama hauna, lazima uombe Mfalme wa amani, ili aweze kukutuliza, ujiandae kukutana na Yeye. “sisi tumezoea kutazama roho za watu wengine na kumbe ni lazima utazame roho yako, Baba Mtakatifu ameshauri.

Kuleta amani ndani ya familia: je kuna madaraja au kuta?

Katika kuendelea na ufafanuzi juu ya amani: “kuna haja ya kutengeneza amani ndani ya nyumba na ndani ya familia. Ni masikitiko makubwa kuona ndani ya familia hakuna amani kutokana na uwepo wa mapambano kati yao na vita vidogo vidogo, na mara nyingi kukosekana kwa muungano, kwa maana hiyo Baba Mtakatifu anawaalika waamini katika kesi hiyo kujiuliza kama ndani ya familia, ipo amani au vita, mapambano kati ya mmoja na mwingine, na kujiuliza, kama hakuna muungano, madaraja au kuna kuta zinazotenganisha!

Uliza watoto, wanapigana wao kwa wao au wanafanya amani

Mantiki ya tatu ambayo Baba Mtakatifu amejikita nayo katika kueleza juu ya amani ni ile ya kuomba amani duniani, mahali ambapo anaonesha kuwa kuna vita badala ya amani, kuna vita na ukosefu wa muungano, ipo chuki na unyanyasaji, kwa maana hiyo hakuna amani. Maswali ya kujiuliza: je mimi ninafanya nini kwa ajili ya amani ya dunia?

Baba Mtakatifu ametoa mfano: Wengine wanasema, padre dunia iko mbali; lakini je, wewe unafanya nini ili amani iweze kuwapo katika mtaa wako, shuleni kwako na katika sehemu ya kazi?  Unatafuta samahani ili ujiingize katika vita, chuki na kusengenya wengine? Huo ni mtindo wa kufanya vita!  je mimi ni mpatanishi? Natafuta namna ya kutengeneza madaraja? Nahukumu wengine? Na katika hilo, pia Baba Mtakatifu amebainisha inabidi kuuliza hata watoto na vijana: je mnafanya nini shuleni? Iwapo kuna mwenzao shuleni ambaye hampendi au kumchukia kidogo kwa sababu ni mdhaifu, je anafanya nini au anafanya amani ? Je unasamehe yote? Je mimi ni fundi wa amani? Yote hayo yanahitajika katika kipindi cha Majilio, ili kujiandalia vema ujio wa Bwana ambaye ni Mfalme wa amani.

Kufanya amani ni kuiga Mungu kidogo

Amani daima inakwenda mbele na wala haisimami na inatoa matunda lakiii inaanzia katika roho na baadaye hurudi mara baada ya kufanya mchakato wote wa amani  kwa maana, Baba Mtakatifu anabainisha: kufanya amani ni sawa na kuiga Mungu kidogo. Yeye alipotaka kufanya amani na sisi, alimtuma Mwanae atengeneze amani na kuwa Mfalme wa amani. Katika kufafanua vizuri , Baba Mtakatifu anatoa mfano: lakini mwingine anaweza kusema, padre mimi sikusoma kwa hiyo sijuhi ni jinsi gani ya kufanya amani na siyo mtaalam, sielewi, au mimi ni kijana ….   Katika Injili Yesu anatuelezea ni kwa jinsi gani: “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza”. Kwa maana hiyo Baba Mtakatifu Francisko anongeza kusema, ndiyo wewe hukusoma, wewe siyo mwenye hekima… lakini unaweza kuwa mdogo, mnyenyekevu na mtumishi wa wengine. Kuwa mdogo na Bwana atakupatia uwezo wa kujua jinsi gani ya kutengeneza amani na nguvu ya kufanya hivyo.

Kusimama mbele ya viashiria ya vita ndogo

Kwa kuhitimisha mahubiri yake Baba Mtakatifu anafafanua zaidi: Maombi ya kipindi hiki, yatazame hasa katika uwezekano wa vita ndogo, iwe ya nyumbani, hata ndani ya mioyo, iwe shuleni, hata katika kazi. Kusimama na kutafuta namna gani ya kufanya amani, lakini kamwe ifanyike bila kuumiza wengine. Baba Mtakatifu amehitimisha akiomba Bwana aweze kutuandaa mioyo hiyo kwa ajili ya Kuzaliwa kwa Bwana na Mfalme wa amani, zaidi kufanya kila njia kuanzia katika moyo wangu binafsi, amani ndani ya familia, shuleni, mtaa na katika kazi na hatimaye wote tunaweza kuwa wanaume na wanawake wa amani.

04 December 2018, 14:53
Soma yote >