Cerca

Vatican News
Papa Francisko anawataka waamini kuadhimisha Noeli kwa imani na matumaini makubwa pasi na kumezwa na malimwengu! Papa Francisko anawataka waamini kuadhimisha Noeli kwa imani na matumaini makubwa pasi na kumezwa na malimwengu!  (ANSA)

Papa Francisko: Ombeni neema ya kuadhimisha Noeli kwa imani kuu!

Si rahisi sana kuweza kuhifadhi na kulinda imani kutokana na changamoto mbali mbali ambazo waamini wanakabiliana nazo! Baba Mtakatifu alikuwa anafanya rejea kwenye Injili ya Luka, 5:17-26 pale mgonjwa wa kupooza alipoponywa na kuondolewa dhambi zake kutokana na ujasiri wa ushuhuda ulioneshwa na jumuiya yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 10 Desemba 2018, amewashauri waamini kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kuweza kujiandaa kikamilifu kwa imani na matumaini, ili kuweza kuadhimisha Sherehe ya Noeli. Si rahisi sana kuweza kuhifadhi na kulinda imani kutokana na changamoto mbali mbali ambazo waamini wanakabiliana nazo! Baba Mtakatifu alikuwa anafanya rejea kwenye Injili ya Luka, 5:17-26 pale mgonjwa wa kupooza alipoponywa na kuondolewa dhambi zake kutokana na ujasiri wa ushuhuda ulioneshwa na jumuiya yake, kiasi hata cha kumgusa Kristo Yesu, kumwonea huruma na hatimaye, kumwondolea dhambi zake.

Katika maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho, waamini wanaalikwa na Mama Kanisa kumwomba Mwenyezi Mungu awakirimie imani! Hii ni katekesi endelevu juu ya fadhila ya imani inayoshuhudiwa kwa njia ya ujasiri kama ilivyokuwa katika Injili ya siku! Si rahisi sana watu kuamua kutoboa juu ya dari, ili kupata mwanya wa kumshusha mgonjwa, apate kukutana na Kristo Yesu! Watu hawa walikuwa na imani thabiti kwa Kristo Yesu na wala hawakuwa na mashaka hata kidogo juu ya nguvu na uwezo wake wa kuponya na kusamehe dhambi.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanajiandaaa kuadhimisha Sherehe ya Noeli kwa imani thabiti na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu! Iwe ni fursa ya kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, kama ilivyokuwa kwa yule akida aliyeomba huruma ya Yesu kwa ajili ya mtumwa wake aliyekuwa karibu ya kufa, akaponywa au yule mwanamke aliyekuwa akitokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, aliyethubutu kugusa upindo wa vazi lake na mara akaponywa! Lakini, Yesu pia aliwakemea watu kama Mtume Petro waliokuwa na imani haba na hivyo kuwahakikishia kwamba, yote yanawezekana kwa mtu anaye amini!

Waamini wamwombe Mwenyezi Mungu neema ya kuweza kuadhimisha vyema Fumbo la Umwilisho, kwa imani thabiti pasi na kumezwa mno na malimwengu! Kristo Yesu anawataka wafuasi wake, kujiandaa kikamilifu ili kuadhimisha Fumbo hili kwa imani. Waamini wawe na jicho la imani ili kumtambua Kristo kuwa ni Masiha na Mkombozi wa ulimwengu. Huu ni mwaliko kwa waamini kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwalinda dhidi ya vishawishi vya mwovu shetani.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujitaabisha kusoma Injili ya Yohane: Sura ya 9:1-41 inayomzungumzia Yesu alivyomponya yule kijana aliyezaliwa kipofu, shida na mahangaiko aliyopata kutoka kwa Mafarisayo, lakini hatimaye, alipokutana na Kristo Yesu akamwambia: “Naamini, Bwana”. Katika mahangaiko ya imani yao, waamini wanahimizwa kumwomba Mwenyezi Mungu neema, aweze kuwaongezea imani, awapiganie wanapokodolewa macho na malimwengu; wanapotumbukia kwenye ushirikina! Awasaidie kulinda imani na kuimwilisha katika matendo, kwani si rahisi sana na kweli yataka moyo anasema Baba Mtakatifu Francisko!

Papa: Mahubiri
10 December 2018, 14:24
Soma yote >