Tafuta

Papa Francisko: Mtangazeni ni kumshuhudia Kristo kwa njia ya maisha adili na matakatifu. Papa Francisko: Mtangazeni ni kumshuhudia Kristo kwa njia ya maisha adili na matakatifu.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Mtangazeni na kumshuhudia Kristo kwa matendo!

Kiini cha Habari Njema anasema Baba Mtakatifu ni kwamba, Kristo Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Hii ni habari nzito inayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya Wakristo kwa njia ya matendo na wala haya si matangazo ya biashara!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Kila mwaka ifikapo tarehe 30 Novemba, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Andrea Mtume, fursa makini ya kuonesha mshikamano wa kiekumene na Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican amewataka waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa njia ya maisha yao yenye mvuto na mashiko kama walivyofanya Mitume wa Yesu, waliothubutu kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Hii ni changamoto ya kuondokana na kishawishi pamoja na dhambi ya kusikiliza Neno la Mungu, lakini wanashindwa kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao kama anavyosema Mtakatifu Paulo katika somo la kwanza kwamba, kwa maana kwa moyo wa mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu! Habari Njema ya Wokovu haina budi kutangazwa na kusikilizwa kwa makini, ili watu waweze kuokoka na kupata maisha ya uzima wa milele.

Kiini cha Habari Njema ni Kristo Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Hii ni habari nzito inayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya Wakristo kwa njia ya matendo na wala haya si matangazo ya biashara! Kwa hakika Kristo Yesu alikuwa mwema na mtakatifu wa Mungu, alitenda miujiza na kuwafundisha watu matendo makuu ya Mungu! Dhamana na wajibu wa Wakristo katika ulimwengu mamboleo si wongofu wa shuruti, bali ni kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa kwa njia ya maisha yenye mvuto na mashiko!

Wakristo wakumbuke kwamba, wameitwa na kutumwa na Kristo Yesu, changamoto na mwaliko wa kujisadaka bila ya kujibakiza ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kama walivyofanya wafidiadini na waungama imani wanaokumbukwa na Mama Kanisa. Wakristo wawe makini ili wasitumbukie katika upagani mamboleo kwa kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa njia ya maneno matupu! Ushuhuda wa maisha ndiyo sadaka anayoitaka Kristo Yesu kutoka kwa wafuasi wake kama njia ya kuitikia wito na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Mwenyezi Mungu kwa njia ya ufunuo, amewawezesha watu kumtambua Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kashfa iliyowaacha watu wengi wakiwa wamepigwa na bumbuwazi! Yesu alishinda kishawishi cha Shetani kwa kutimiza mapenzi ya Mungu mpaka dakika ya mwisho! Yesu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho na Pasaka, amekuwa ni shuhuda wa Baba wa milele kama ilivyo hata kwa mashuhuda wa imani na wafiadini, bila kusahau maelfu ya waamini wanaoendelea kusadaka maisha yao katika hali ya ukimya ndani ya familia na jamii katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu anasema, hawa ni wale mashuhuda wanaotekeleza mapenzi ya Mungu katika hali ya ukimya. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanapewa utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sanjari na kuendelea kuiga mfao bora kutoka kwa Kristo mwenyewe aliyetangaza na kufundisha kwa mifano ya maisha yake! Kinyume chake ni kashfa dhidi ya Kristo hatari kubwa kwa familia ya Mungu!

Mt. ANDREA MTUME

 

30 November 2018, 15:16
Soma yote >