Cerca

Vatican News
Papa Francisko: Mambo ya Mwisho wa Nyakati: Siku ya huruma ya Mungu, furaha na raha ya kukutana na Mwenyezi Mungu. Papa Francisko: Mambo ya Mwisho wa Nyakati: Siku ya huruma ya Mungu, furaha na raha ya kukutana na Mwenyezi Mungu.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Siku ya Hukumu ya Mwisho: Huruma na furaha!

Katika Kitabu cha Ufunuo, Yohane anazungumzia kuhusu Siku za mwisho, Kikristo Yesu na Malaika watakapokuja kuvuna, hapa ndipo mahali ambapo, waamini wanapaswa kuonesha ubora wa ngano ya maisha yao! Ni siku ya kukutana na Mwenyezi Mungu na kuonesha yale yaliyojiri katika maisha yake hapa duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu aliwafundisha wanafunzi wake mambo ya mwisho wa nyakati, kama angalisho la kuwataka wautumie vyema muda walionao sasa, kwa kukesha, tayari kutoa hesabu ya matendo yao mema hapa duniani. Kitabu cha Ufunuo kinajaribu kugusia mambo ya mwisho wa nyakati, lakini jambo la msingi kwa waamini ni kuendelea kuwa tayari kukutana na Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, ili siku hii iwe ni siku ya furaha na matumaini ya maisha ya uzima wa milele!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 27 Novemba 2018 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Mwisho wa nyakati, yaani mwisho wa maisha ya kila mwanadamu ni kipindi cha neema, kinachomtaka mwamini kuchunguza vyema dhamiri yake ili aweze kujiandaa vyema kukutana kwa furaha na Mwenyezi Mungu. Lakini, jambo la kusikitisha na kuona kwamba, watu wengi wamejawa na hofu na mashaka kuhusiana na mambo ya mwisho wa nyakati.

Katika Kitabu cha Ufunuo, Yohane anazungumzia kuhusu Siku za mwisho, Kristo Yesu na Malaika watakapokuja kuvuna, hapa ndipo mahali ambapo, waamini wanapaswa kuonesha ubora wa ngano ya maisha yao! Ni siku ya kukutana na Mwenyezi Mungu na kuonesha yale yaliyojiri katika maisha yake hapa duniani! Mapungufu na madhaifu ya kibinadamu ni sehemu ya maisha, lakini jambo la msingi ni kutambua kwamba, mwisho wa nyakati kila mtu, atapaswa kutoa hesabu ya ubora wa maisha yake.

Waamini watambue kwamba, hakuna mtu anayefahamu siku wala saa atakapokuja Mwana wa Adamu, lakini ikumbukwe kwamba, iko siku, itabidi watoe hesabu zao. Waamini wajiulize ikiwa kama leo hii wanaitwa mbele ya Mungu kutoa hesabu ya ubora wa maisha yao, mambo yangekuaje? Baba Mtakatifu anasema, Siku ya Hukumu ya Mwisho, itakuwa ni siku ya huruma, furaha na raha! Huu ni mwisho wa kazi ya uumbaji, maisha, kumbe, ni vyema, waamini wakachukua nafasi kufanya tafakari kuhusu mambo ya nyakati za mwisho katika maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu anawahamasisha waamini kuendelea kuyafakari mambo ya mwisho wa nyakati, kwa kuchunguza dhamiri; kwa kurekebisha na kusahihisha yale mapungufu ambayo yamejitokeza katika maisha yao, ili kuendelea kukuza na kuboresha matendo mema katika mwanga na hekima ya Roho Mtakatifu. Siku ya mwisho ni wakati muafaka wa kukutana na Kristo Yesu, Hakimu mwenye huruma na mapendo, kiini cha imani ya Kikristo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusali na kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia kujiandaa vyema kukutana na Mwenyezi Mungu Siku ile atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho!

Papa: Mahubiri

 

27 November 2018, 15:06
Soma yote >