Tafuta

Ushuhuda wa Kanisa unafumbatwa katika: Ekaristi Takatifu, Matendo ya Huruma na Damu ya Mashuhuda wa imani! Ushuhuda wa Kanisa unafumbatwa katika: Ekaristi Takatifu, Matendo ya Huruma na Damu ya Mashuhuda wa imani!  (Vatican Media)

Ushuhuda wa Kanisa unafumbatwa katika: Ekaristi na Matendo ya hu

Kanisa kwa namna ya pekee kabisa linajidhihirisha katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu linalomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu katika Kristo Yesu. Ushuhuda wa wafiadini na waungama imani ni kielelezo kisichokuwa na mvuto kwa walimwengu anasema Baba Mtakatifu Francisko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Alhamis, tarehe 15 Novemba 2018 amesema, Kanisa linakua, linapanuka na kusonga mbele katika hali ya ukimya pasi na kutafuta makuu mbele ya watu na kwamba, Kanisa kwa namna ya pekee kabisa linajidhihirisha katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu linalomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu katika Kristo Yesu.

Ni katika Jumuiya ya waamini kila mtu anaonja upendo wa Mungu unaowakumbatia na kuwaambata watu wote bila ubaguzi! Mahubiri ya Baba Mtakatifu ni sehemu ya Injili ya Lk. 17:20-25. Baba Mtakatifu amekazia adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu na Matendo ya huruma, hata kama si habari inayopewa kipaumbele cha pekee kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii! Kwa njia hii, Kanisa linazidi kusonga mbele bila ya makelele kama yale ya Mafarisayo. Huu ndio mfano wa mpanzi wa mbegu ambalo ni Neno la Mungu, linalokua na hatimaye, kuzaa matunda.

Papa Francisko anasema, huu ndio mtindo wa maisha ya Kanisa na matunda yake ni matendo ya huruma, yanapoonekana watu wanamsifu na kumtukuza Mungu. Ekaristi Takatifu ni sadaka ya Kristo Msalabani na matunda ya sadaka hii, yanapaswa kuwa ni matendo mema! Mchakato wa ukuaji wa Kanisa unafumbatwa kwa namna ya pekee katika ushuhuda, maisha ya sala, maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa sanjari na kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kama anavyotaka.

Hii ni changamoto kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaokoa kutoka katika kishawishi cha kutaka kujionesha, kwa kupenda mno: matukio, sherehe na tafrija zisizokuwa na mashiko. Baba Mtakatifu amekazia: ukimya wa Kanisa, matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na maadhimisho ya Fumbo la Pasaka ya Kristo ndiyo mambo ya kupewa kipaumbele cha kwanza. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kwa bahati mbaya, ulimwengu mamboleo umesheheni kishawishi cha kutaka kuonekana na hata wakati mwingine, kumezwa na anasa na matukio makubwa makubwa!

Hiki ni kishawishi ambacho hata Kristo Yesu alikutana nacho kabla ya kuanza maisha ya hadhara kwa kuambiwa atende miujiza ili watu wapate kumwamini. Lakini, Kristo Yesu katika maisha yake, akajikita zaidi katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu; maisha ya sala na ukimya pamoja na matendo ya huruma, kielelezo makini cha “Msalaba” na “Mahangaiko ya watu”. Fumbo la Msalaba na mateso ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa! Kwa njia ya sala na sadaka za mashahidi na wafiadini, Kanisa linaendelea kukua na kukomaa. Leo hii kuna umati mkubwa wa wafiadini pengine kuliko hata wakati wowote ule wa historia, utume na maisha ya Kanisa, lakini, hawa si sehemu ya habari zinazovuta hisia za watu kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii, kwa sababu walimwengu kamwe hawawezi kuvumilia kuwaona wafiadini! Watu kama hawa wanaangaliwa kwa “jicho la kengeza”.

Papa: Kanisa: Ushuhuda
15 November 2018, 06:37
Soma yote >