Tafuta

Papa Francisko: Sifa kuu za Askofu mahalia ni: unyenyekevu na huduma! Papa Francisko: Sifa kuu za Askofu mahalia ni: unyenyekevu na huduma!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Sifa kuu za Askofu mahalia: Unyenyekevu na huduma!

Mtakatifu Paulo, Mtume anamwandikia Tito mambo msingi yanayopaswa kufuatwa na kutekelezwa na Maaskofu, kwa kukamilisha yale yanayopungua katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kuwachagua na kuwasimika wazee wanaofaa kwa ajili ya uongozi wa Kanisa; watu wema na wenye kiasi, wapenda haki na watakatifu; watu wenye mifano bora ya kuigwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu ni alama ya utimilifu wa Daraja Takatifu ambamo Askofu anapewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ni dhamana inayofumbatwa katika unyenyekevu na upendo na kamwe Maaskofu wasijisikie kuwa ni wafalme. Mtakatifu Paulo, Mtume anamwandikia Tito mambo msingi yanayopaswa kufuatwa na kutekelezwa na Maaskofu, kwa kukamilisha yale yanayopungua katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kuwachagua na kuwasimika wazee wanaofaa kwa ajili ya uongozi wa Kanisa; watu wema na wenye kiasi, wapenda haki na watakatifu; watu wenye mifano bora ya kuigwa.

Maaskofu wanapaswa kuratibu maisha na utume wa Kanisa, daima wakimwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza na kuwasimamia. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Mtaguso Mkuu wa kwanza wa Yerusalemu, ulioweka mambo sawa na Injili ya Kristo ikasonga mbele! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 12 Novemba, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Kanisa linapofanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Yosafat, Askofu na Shahidi.

Mtakatifu Paulo, kwa busara ya kichungaji alimwacha Tito mjini Krete ili aweze kuweka taratibu katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutoa vigezo muhimu vinavyopaswa kuzingatiwa kwa mtu kuteuliwa kuwa Askofu, kama msimamizi wa mafumbo ya Kanisa na wala si mtawala anayeelemewa na uchu wa mali na utajiri. Askofu anapaswa kuwa ni wakili wa Mungu na kiongozi anayejiaminisha na kutembea mbele ya Mungu kama ilivyokuwa kwa Mzee Ibrahimu, Baba wa imani. Askofu anapaswa kuwa ni mtu wa Mungu; mtu wa watu na asiyependa makuu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, pengine inafaa kwa Kanisa kuchunguza sifa hizi kwa wale wanaotarajiwa kuteuliwa kuwa Maaskofu kabla ya kusonga mbele na uchunguzi wa mambo mengine. Lakini, kimsingi Askofu anapaswa kuwa mtu mnyenyekevu, mpole na ambaye yuko tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Huu ni mwongozo unaoobubujika kutoka katika Neno la Mungu na ambao unapaswa kufuatwa. Maaskofu wenye sifa na karama kama hizi, ndio wenye uwezo wa kuratibisha maisha na utume wa Kanisa kwa ubora zaidi! Kinachotakiwa mbele ya Mungu ni unyenyekevu na moyo wa huduma; umahiri wa kuhubiri ni nyongeza tu. Kwa maombezi ya Mtakatifu Yosafat, Askofu na shahidi, awaombee Maaskofu wenzake, waweze kusimika maisha na utume wao kadiri ya vigezo vya Mtakatifu Paulo kwa Tito!

Papa: Sifa za Askofu

 

12 November 2018, 14:00
Soma yote >