Papa Francisko awataka waamini kukumbatia ufukara wa Kiinjili katika maisha na utume wao Papa Francisko awataka waamini kukumbatia ufukara wa Kiinjili katika maisha na utume wao  (Vatican Media)

Papa Francisko awataka waamini kujikita katika ufukara wa Kiinjili katika maisha na utume wao!

Papa Francisko anasema, changamoto ya kwanza kwa waamini ni kuondokana na uchu wa mali na madaraka, pili ni kukubali na kupokea madhulumu kwa ajili ya Injili ya Kristo Yesu na tatu ni ufukara unaosimikwa katika upweke chanya, kiasi cha kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, dakika zile za mwisho wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 18 Oktoba, Mama Kanisa anasherehekea Siku kuu ya Mtakatifu Luka, Mwinjili na mtunzi wa Kitabu cha Matendo ya Mitume. Katika maisha, utume na safari zake za kimisionri, alifuatana na Mtakatifu Paulo, Mtume, ndiyo maana anakumbukwa katika nyaraka mbali mbali. Mwinjili Luka ni mtetezi wa maskini, wagonjwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha mjini Vatican amekazia umuhimu wa wafuasi wa Kristo Yesu kuondokana na uchu wa mali na madaraka; kuvumilia madhulumu kwa ajili ya Injili ya Kristo pamoja na kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kwamba, ufukara ni changamoto changamani kwa wafuasi wote wa Kristo Yesu pasi na ubaguzi!

Baba Mtakatifu anasema, changamoto ya kwanza kwa waamini ni kuondokana na uchu wa mali na madaraka, pili ni kukubali na kupokea madhulumu kwa ajili ya Injili ya Kristo Yesu na tatu ni ufukara unaosimikwa katika upweke chanya, kiasi cha kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, dakika zile za mwisho wa maisha! Kristo Yesu aliwatuma wafuasi wake 72 kwenda katika maeneo ambamo angepitia na kuwataka kujikita katika ufukara badala ya kuelemewa na mizigo ya vitu, kwani wangeshindwa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao wa kutangaza na kushuhudia Injili.

Baba Mtakatifu ameendelea kufafanua aina tatu za ufukara ambazo zinapaswa kufumbatwa katika maisha ya mwamini, kwa kuondokana na uchu wa fedha na mali kama mwanzo wa mchakato wa ufuasi wa Kristo. Huu ndio ufukara wa moyo unaopaswa kuwa ni sehemu ya ushuhuda wa Kanisa na taasisi zake zote. Utajiri mkubwa wa wafuasi wa Kristo ni fursa ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa, katika uhuru na ukweli wa maisha. Ufukara ni kielelezo makini cha ushuhuda wa Injili wenye mvuto na mashiko!

Ufukara wa kukubali na kudumu katika uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake una mvuto mkubwa kama wanavyoshuhudia Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Kuna wakristo wanaoteseka na kudhulumiwa sehemu mbali mbali za dunia kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kuna madhulumu wanayofanyiwa watu kwa kuchafuliwa utu, heshima na majina yao. Huu pia ni ushuhuda wa ufukara katika maisha ya Kikristo!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, aina ya tatu ya ufukara ni ile hali ya kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kama alivyofanya Mtakatifu Paulo, aliyejikuta akiwa amesimama peke yake mahakamani, ili kujitetea baada ya kukimbiwa na watu waliokuwa karibu naye! Huu ndio ushuhuda unaotolewa na vijana wanaoacha yote kwa ajili ya kumfuasa Kristo katika maisha na utume wa kikasisi na kitawa. Baadaye wanakumbana na changamoto za maisha: nyanyaso, dhuluma, wivu usiokuwa na mashiko na hatimaye, upweke unaowapelekea katika kifo, ili kupumzika katika amani ya Kristo! Baba Mtakatifu anawataka wafuasi wa Kristo kuhakikisha kwamba, wanafuata njia hii kama sehemu ya ushuhuda wa ufuasi wao kwa Kristo na Kanisa lake, kama alivyofanya Mtakatifu Petro katika uzee wake, akaishia kutundikwa Msalabani, miguu juu, kichwa chini!

Mwinjili Luka
18 October 2018, 15:37
Soma yote >