Papa Francisko anawataka waamini kuachana na chachu ya unafiki! Papa Francisko anawataka waamini kuachana na chachu ya unafiki!  (Vatican Media)

Papa Francisko anawaalika waamini kuachana na chachu ya unafiki!

Chachu ya Mafarisayo iliwadumaza watu na hivyo kushindwa kusonga mbele. Kristo Yesu, anawapatia chachu ya imani inayowawezesha kukua na kukomaa, ili hatimaye, kuwa ni warithi wa maisha ya uzima wa milele!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Unafiki ni sumu ya maisha na utume wa Kanisa. Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni mashuhuda wa ukweli na uwazi pamoja na kuendelea kumtegemea Roho Mtakatifu, ili waweze kuwa ni chachu ya urithi na amana ya imani ambayo Kristo Yesu amewaachia wafuasi wake. Huu ni mwaliko wa kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho kwa kuondokana na unafiki ulioshuhudiwa wakati ule wa Yesu na: Mafarasayo, Walimu wa Sheria, Masadukayo! Hawa ni watu waliopekenyuliwa sana na ubinafsi, kiasi cha kujifungia ndani mwao, wakajikita zaidi katika mwonekano wa nje, kwa kukazia usalama na nafasi zao katika jamii.

Wanafiki ni watu waliojigamba kutoa sadaka na daima walipenda watu wengine wafahamu matendo yao! Lakini, ni wale wale ambao hawakuwa tayari kumsaidia yule mtu aliyepambana na majambazi, wakapita pembeni, lakini, akaokolewa na yule Msamaria mwema, kielelezo cha imani tendaji! Ni watu waliokuwa maarufu kuwasukumiza wengine pembezoni mwa jamii kutokana na magonjwa kama ilivyokuwa kwa wakoma na wadhambi. Chachu hii ya unafiki anasema Kristo Yesu ni hatari sana katika maisha ya kiroho na hivyo anawataka wafuasi wake kujilinda na chachu ya Mafarisayo ambayo ni unafiki, kwani haya ni mazoea mabaya na kamwe hayawezi kusaidia katika malezi, majiundo na ukomavu wa mtu!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 19 Oktoba 2018 wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Mafarisayo walikuwa kama makaburi yaliyopakwa chokaa kwa nje, lakini ndani yalikuwa yamejaa mifupa na uvundo mkali, uharibifu na wala hawakuwa nafasi ya kukua na kukomaa katika utashi wao wa ndani. Chachu ya Mafarisayo iliwadumaza watu na hivyo kushindwa kusonga mbele. Kristo Yesu, anawapatia chachu ya imani inayowawezesha kukua na kukomaa, ili hatimaye, kuwa ni warithi wa maisha ya uzima wa milele!

Waamini kwa njia ya Kristo Yesu, wamefanywa kuwa warithi, kwa kuchaguliwa tangu awali sawa sawa na kusudi na mapenzi ya Mungu. Hii ni chachu inayowafanya waamini kukua na kukomaa kiasi hata cha kuweza kuonekana kama mashuhuda wa imani. Kuna wakati wanaweza kuanguka, lakini wanajisahihisha na kusonga mbele. Ni watu wanaoweza kuanguka dhambini, lakini, wakasimama tena kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kufikia furaha ya kweli ambayo kimsingi ni utukufu na sifa kwa Mwenyezi Mungu.

Hii ndiyo chachu ya Roho Mtakatifu inayowasukuma waamini kuwa ni sehemu ya utukufu na sifa kwa Mwenyezi Mungu. Roho Mtakatifu ndiye arabuni ya urithi wao.  Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kuwa waaminifu hata kama wanaanguka na kutenda dhambi! Wajijengee uwezo wa kuratibu maisha yao, ili kukua na kukomaa kutoka katika undani wao, kwa kuondokana na unafiki. Waamini wakimbilie chachu ya Roho Mtakatifu, chachu ya matumaini, sifa na utukufu wa Mungu, ili kuambata furaha ya kweli. Baba Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake kwa kusema, wanafiki ni watu ambao wamesahau maana ya kuwa na furaha katika maisha!

Papa: Wanafiki
19 October 2018, 13:53
Soma yote >