Tafuta

Tumwombe Mungu atujalie neema zake ili Kristo aliye nasi tusimzoee mno mpaka kupuuza Umungu wake na kumfukuzia mbali. Tumwombe Mungu atujalie neema zake ili Kristo aliye nasi tusimzoee mno mpaka kupuuza Umungu wake na kumfukuzia mbali.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Dominika ya IV,Mwaka C:Uongozi ni wito wa kutumikia!

Katika Dominika ya 4 ya mwaka C:Somo la I linatufundisha kuwa wito ni zawadi toka kwa Mungu anayemwita mwanadamu kabla ya kuzaliwa kwake.Somo la II ni msisitizo wa upendo katika kutenda na kuwahudumia wengine kwa vipawa na vipaji tulivyojaliwa.Injili inasimulia Yesu kukataliwa na watu wa kijijini kwake kwa sababu walimfahamu yeye,ndugu zake na wazazi wake tu na hivyo kumwona kuwa ni mtu wa kawaida asiyestahili kuwa Nabii,Kuhani na Mfalme.Mazoea huleta dharau!

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 4 ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo ya domenika hii umejikita katika wito wa kinabii. Lakini Nabii ni nani? Nabii ni mjumbe wa Mungu anayeitwa na kutumwa kuwaeleza watu mambo yahusuyo uhusiano uliopo kati ya Mungu na watu wake. Ni mjumbe wa watu kwa Mungu (Hab.1,3) naye anateuliwa na Mungu mwenyewe (Yer.1:5). Kanisa linatufundisha kuwa kwa sakramenti ya ubatizo kila mbatizwa anashirikishwa unabii, ukuhani na ufalme wa Kristo. Hivyo kila mbatizwa anaitwa na Mungu ili amtumikie Yeye katikati ya watu wake.

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Yeremia (Yer 1:4-5, 17-19). Somo hili linahusu kuitwa kwa Yeremia na kumweka wakfu kuwa Nabii wa Mataifa (Yer 1:5). Katika kuitwa huko, Yeremia anaogopa na kusema: “Ee, Bwana Mungu! Tazama, siwezi kusema, maana mimi ni mtoto!” (Yer 1:6). Mungu anamwimarisha na kumtia nguvu akimwambia; Usiogope, mimi nipo pamoja nawe, utanena yale nitakayokuamuru kwani nimetia maneno yangu kinywani mwako. Kumbe tunaona kuwa wito ni zawadi toka kwa Mungu anayemwita na mkumchangua mwanadamu hata kabla ya kuzaliwa kwake. Mtume Paulo anashuhudia juu ya hili akisema: “Lakini Mungu aliyenitenga tangu tumboni mwa Mama yangu, akaniita kwa Neema yake, alipoona vyema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa Habari zake, mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu” (Gal 1:15-16).

Katika kumwita Yeremia, Mungu anamwambia kuwa atapata upinzani na mateso mkali. Ni kweli Yeremia alipata mateso na upinzani mkali kutoka kwa familia yake, viongozi wa dini, viongozi wa serikali na hata kwa watu wengine, wakimshutumu kwa uasi, uhaini, na usaliti. Kwa mashtaka haya Yeremia alitupwa jela na baadae kupelekwa uhamishoni Misri. Katika hali hii, kuna nyakati ambazo alikataa tamaa na kutaka kuacha kazi aliyopewa na Mungu. Yeye mwenyewe anashuhudia akisema: “Nami nikasema, sitamtaja, wala sitasema tena kwa Jina lake.” Lakini uaminifu wake kwa Mungu ulikuwa ni kichochoe cha kusonga mbele kama anavyosema. “Basi ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia” (Yer 20:9). Hivyo akiongozwa na Roho wa Mungu Yeremia aliyashinda majaribu yote hata akawa ishara ya yale yatakayompata Bwana wetu Yesu Kristo yaani mateso na kifo chake.

Nasi tulioshirikishwa unabii, ukuhani na ufalme wa Kristo hatupaswi kuwa na mashaka, woga, wala wasiwasi katika kuusimamia ukweli na katika kutetea haki za wanyonge. Na tunapoitwa na Mungu, tusiogope, bali tujikabidhi kwake, tuseme na kufanya kile tu anachotuamuru. Kama kiitikio cha wimbo wa katikati kinavyotualika kusema; “Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako”. Naye mzaburi anasisitiza daima tujiweke chini ya ulinzi wa Mungu akisema; “Nimekukimbilia Wewe, Bwana, nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye, uniopoe, unitegee sikio lako, uniokoe. Uwe kwangu mwanga wa makazi yangu, nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe, ndiwe genge langu na ngome yangu. Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi” (Zab. 70:1-4).

Somo la pili la Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 12:13-31,13). Katika somo hili Mtume Paulo anatilia msisitizo juu ya upendo katika kutenda na kuwahudumia wengine kwa vipawa na vipaji tulivyojaliwa Mungu. Mtume Paulo anatoa mafundisho na maonyo haya kwa kuwa yalitokea mafarakano na malumbano kati ya Wakristo Wakorintho na kutokuelewana wao kwa wao, kwa sababu wapo walijiona ni wa maana zaidi kwa karama walizonazo na kuwadharau wengine. Hivyo anasisitiza kuwa kule kunena kwa lugha, kuwa nabii na kujua siri zote na maarifa yote, kuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kutoa mali ili kuwalisha maskini, kuutoa mwili uungue moto, kama huna upendo, haikufaidii kitu. Kila tendo au jambo jema lisipotangulia na upendo halifai machoni pa Mungu. Baada ya maonyo hayo, Mtume Paulo akatoa wasifu wa upendo akisema kuwa; upendo huvumilia, hufadhili, hauhusudu, hautakabari, haujivuni, haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, hauoni uchungu, hauhesabu mabaya, wala haufurahii udhalimu. Upendo hufurahi pamoja na kweli, huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wowote. Kumbe basi tujitahidi kujibidisha kufanya yote kwa upendo kwa ajili ya sifa na utukufu wake ili nasi tutakatifuzwe nao.

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 4:21-30). Sehemu hii ya Injili inasimulia Yesu kukataliwa na watu wa kijijini kwake kwa sababu tu walimfahamu yeye, ndugu zake na wazazi wake na hivyo kumwona kuwa ni mtu wa kawaida asiyestahili kuwa nabii, kuhani na mfalme. Mazoea huleta dharau. Nasi pia tunaweza kuwa na mazoea ya mambo mbalimbali ya kiimani na hivyo kuyadharau. Inawezekana tukawa na mazoea ya kusikiliza neno la Mungu na kuliona ni la kawaida. Inawezekana tukawa na mzaoea ya kupokea Ekaristi Takatifu na kuona kitu cha kawaida na pengine tunadharau hivyo hatuoni kuwa kutokupokea Ekaristi Takatifu kama ni tatizo. Hali hii ni kumkataa Kristo katika maisha yetu.

Hata katika maisha ya kawaida Viongozi wa dini, siasa au serikali wanaweza kudharauliwa kwa sababu tu wanafahamika wao mwenyewe na ya familia zao. Mwingine anawezakuwa anaheshimika sana katika jamii au anakofanya kazi; lakini ndani ya nyumba yake hana heshima iwe kwa mke wake, mme wake au watoto. Hata katika hali hii, kiongozi anapaswa kutambua kuwa yeye ni chombo cha Mungu na amtegemee yeye kwa yote kwa kuwa kazi anayoifanya sio yake ni ya Mungu naye asipoifanya kadiri ya mapenzi yake yeye mwenyewe atakuadhibu. Ndivyo alivyomwambia Nabii Ezekieli “Basi, wewe mtu, nimekuweka kuwa mlinzi wa Waisraeli. Utakaposikia neno kutoka kwangu utawapa onyo langu. Nikimwambia mtu mwovu: “Wewe mtu mwovu hakika utakufa”; lakini wewe husemi chochote ili kumwonya yule mtu mwovu aachane na mwenendo wake; mtu huyo hakika atakufa kwa kosa lake; lakini nitakudai wewe kifo chake. Lakini ukimwonya mwovu aachane na mwenendo wake mbaya, naye haachani na mwenendo wake mbaya, yeye atakufa kwa kosa lake; lakini wewe utakuwa umeyaokoa maisha yako” (Eze.33:7-9). Hivyo ndivyo Paulo alivyomuasa Timotheo akimwambia; “…hubiri huo ujumbe, sisitiza  na kuutangaza iwe ni wakati wa kufaa au wakati usiofaa, karipia, onya na himiza watu ukiwafundisha kwa uvumilivu wote (2Tim.4: 2).

Kwa njia hiyo msomaji/msikilizaji wa Vatican News, kiongozi yeyote yule daima anapaswa kumtegemea Mungu; usiogope hata ikionekana watu hawapendi kusikiliza ujumbe unaowatangazia. Kumbuka ahadi za Mungu kwa watu wanaofanya kazi yake: “Bwana anazijua siku za wakamilifu, na urithi wao utakuwa wa milele. Hawataaibika wakati wa ubaya, na siku za njaa watashiba (Zab.37:18-19). “Heri yenu ninyi watu wakiwatukana na kuwadhulumu na kuwasingizia kila aina ya uovu kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Hivyo ndivyo walivyowadhulumu manabii waliokuwako kabla yenu” (Mt.5:11). “Nao watapigana nawe lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe…ili nikuokoe (Yer 1:19). Basi tumwombe Mungu atujalie neema zake ili Kristo aliye nasi tusimzoee mno mpaka kupuuza Umungu wake, na kumfukuzia mbali.

Neno la Mungu katika Dominika ya 4 ya mwaka C


 

01 Februari 2025, 11:26