Tafuta

Don Bosco Mwalimu wa Vijana. Don Bosco Mwalimu wa Vijana. 

Sikukuu ya Mtakatifu Yohane Bosco:Mwalimu na Mlezi wa Vijana

Ni tukiwa na matumaini na mahujaji pamoja na vijana tu ili kwa pamoja nao tunaweza kutoa ushuhuda wa imani ulio wa kweli na wa kuvutia zaidi na kila mmoja wetu aweze kutoa tabasamu,ishara ndogo ya urafiki,jicho la huruma,sikio la kusikiliza,tendo jema,kwa ufahamu kwamba,katika Roho wa Yesu hizi zinaweza kuwa kwa wale wanaozipokea, mbegu za matumaini zilizotajirika.

Na Padre Philemon Chacha wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco.

Ndugu Msikilizaji wa Radio Vaticani. Kila mwaka ifikapo tarehe 31 Januari Kanisa huadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane Bosco, ambaye ni Baba, Mwalimu na Rafiki wa Vijana. Hivyo tuna kila sababu ya kufurahi na kusheherekea, kwanza kwasababu mwaka 2025 ni mwaka unaobeba tukio muhimu la kikanisa la Jubilei ambayo Baba Mtakatifu Fransisco alitangaza katika Waraka wake Spes Non Confundit yaani “Tumaini halitahayarishi” (Warumi 5:5). Pili, mwaka huu sisi kama wasalesiani wa Don Bosco tunaadhimisha kumbukumbu ya miaka 150 tangu kutumwa kwa wamisionari wa kwanza na Don Bosco mwenyewe kwenda Argentina. Kumbe, mwaka 2025 ni mwaka wa kipekee.

Katika waraka wake Baba Mtakatifu Fransisco anaeleza maneno yaliyobeba kauli mbiu ya Jubilei yaaani “Tumaini halitahayarishi” kuwa ni maneno ya Mtume Paulo katika roho ya tumaini na ya kutia moyo kwa jamii ya Wakristo wa Roma. Hivyo, kufikiria kuhusu Jubilei inamaanisha kufikiria kila mmoja kama mahujaji katika tumaini. Tutakuwa mahujaji wengi wa matumaini katika kila kona ya dunia, katika Makanisa mengi maalum; tutakuwa mahujaji katika hija na vijana, kwenye safari ambayo itatupeleka katika kukutana kwetu sisi wenyewe na kukutana na Yesu, ambaye ni "mlango" wa wokovu (Rej. Yn 10:7,9). Pamoja tutaweza kushuhudia kwamba yeye, Yesu, ndiye "tumaini letu" (1 Tim 1:1).

Baba Mtakatifu anasema: "Kila mtu anajua maana ya kutumaini. Katika moyo wa kila mtu, tumaini hukaa kama shauku na matarajio ya mambo mema yanayokuja, licha ya kutokujua kile ambacho nini kitakachotokea katika siku zijazo. Hata hivyo, kutokuwa na uhakika kuhusu siku zijazo kunaweza wakati mwingine kusababisha hisia zinazokinzana, kuanzia imani thabiti hadi hofu, kuanzia utulivu hadi wasiwasi, kuanzia imani ya kweli hadi kusitasita na shaka. Mara nyingi tunakutana na watu waliofadhaika, wenye kukata tamaa na waliosheheni ukosoaji kuhusu siku zijazo, kama vile hakuna chochote kinachoweza kuwaletea furaha" (Spes non confundit, 1). Tukikabiliwa na hali hii ambayo ni sehemu ya maisha yetu kama wasalesiani, sehemu ya familia za vijana na ya vijana wenyewe, tunaamini kwamba huu mwaka wa Jubilei, utakuwa ni fursa kubwa kwa kila mtu kuishi katika tumaini.

Maisha ya Mtakatifu Yohane Bosco yalikuwa ni maisha yaliojaa tumaini. Yeye, aliyekuwa daima na uwezo wa kuona mambo kutokea mbali zaidi, katika nyakati ngumu aliinua macho yake kuelekea mbinguni, hakuwahi kuacha kujitolea kwa sababu alikuwa akisubiriwa huko mbinguni. "Kumbuka kwamba Paradiso itakuwa zawadi yako," "Fanya kile unachoweza na umtegemee Mungu wa huruma asiye na mwisho" haya ni baadhi tu ya maneno yaliyojaa tumaini ambayo Yohane Bosco alikuwa akiwaambia vijana wake mara kwa mara, akiwahimiza kuwa na matumaini, kujikabidhi katika huruma ya Mungu, na kutokata tamaa kwa sababu ya magumu ya maisha ya hapa duniani. Na aliendelea kusema kuwa "Paradiso hurekebisha kila kitu," akiwa na manaa ya kuwa tunapofikiria kuhusu Paradiso tunajikumbusha kuwa yatupasa kupambana, kuishi kikamilifu, na kuvumilia shida zote kwa sababu Bwana anatuelekeza huko, na pamoja naye hatupaswi kuogopa. Hivyo kuishi na kukubali changamoto katika wakati huu wa sasa kunaweza kutupeleka kwenye lengo thabiti ambalo ni utakatifu na kuingia mbunguni.

Kwetu sisi Wasalesiani na Familia nzima ya Don Bosco, hatuwezi kuzungumza kuhusu maisha ya Don Bosco, bila kuzungumzia kuhusu ndoto zake. Alihifadhi ndoto zake akilini na moyoni mwake katika maisha yake yote, hata baada ya kuzitimiza. Vijana wakiongozwa na ndoto ya Don Bosco na kwa yale wanayoishi kupitia katika mazingira yetu ya Kisalesiani, wataona kuwa matamanio yao mazuri ndiyo nguvu inayopelekea waweze kufanya mambo makubwa na watajifunza kuwa kila changamoto inaweza kukabiliwa kwa ujasiri na kujiamini. Vijana wana ndoto kubwa, lakini wanapaswa kutiwa moyo wa kuwa na maono! Na sisi kama waelimishaji tuna jukumu hili: kuwaongoza kwenye njia ya kweli ya maisha. Vijana wana haki ya kuota ndoto ya kesho iliyo bora; wanao uwezo mikononi mwao wa kuzaliwa upya na kuanza upya kila mara, wa kusoma na kufanya kazi, wa kujenga mustakabali uliojaa ubinadamu na matumaini.

Tunaposheherekea sikukuu hii ya Mtakatifu Yohane Bosco tunakumbuka tukio muhimu sana la kimisionari katika Shirika letu. Leo hii tunafurahia matunda ya wasalesiani wamisionari wa kwanza ambao Mtakatifu Yohane Bosco aliwatuma miaka 150 iliyopita kwenda Argentina kueneza karama ya kisalesiani. Tuna kila sababu ya kufurahi na kumshukuru Mungu kwa tukio hili kwasababu leo tunaona matunda yake ndani ya mti mkubwa ambao ni Familia ya Kisalesiani, Familia ya Don Bosco, ambapo leo hii tupo katika mataifa 134 duniani ikiwemo Tanzania, Kenya, Sudani na Sudani Kusini. Papa Fransisco, katika Waraka wake kwa ajili ya Jubilei ya mwaka 2025, anatueleza kwamba “Ishara za nyakati, ambazo zinajumuisha hamu ya mioyo ya binadamu inayohitaji uwepo wa kuokoa wa Mungu, zinapaswa kuwa ishara za matumaini” na anatualika Kanisa la ulimwengu – na sisi kama sehemu ya Kanisa – kuishi mwaka huu wa Jubilei na wa kimisionari kwa kujitolea kuwa ishara za matumaini zinazoonekana.

Papa anatualika – na tunafanya mwaliko wake kuwa wetu – kuishi tukiwa tumejikita katika matumaini kwa sababu hii, pamoja na imani na upendo, ndiyo inayounda kiini cha maisha ya Kikristo, lakini zaidi ya yote “matumaini ni fadhila ambayo, kwa namna nyingine, inatoa mwelekeo wa ndani na kusudi kwa maisha ya waamini... tunahitaji ‘kuzidi kuwa na matumaini’ (taz. Rum 15:13). Sikukuu hii ya Mtakatifu Yohane Bosco ambayo tunasheherekea katika Mwaka huu wa Jubilei tunataka na tunapaswa kufanya hivyo pamoja na vijana, kama Familia ya Kisalesiani na kama kauli mbiu ya kisalesiani, yaani Strenna ya mwaka huu inavyotuambia “Tukiwa na matumaini, tu mahujaji pamoja na vijana” ili pamoja nao tuweze kutoa ushuhuda wa imani ulio wa kweli na wa kuvutia zaidi, na “kila mmoja wetu aweze kutoa tabasamu, ishara ndogo ya urafiki, jicho la huruma, sikio la kusikiliza, tendo jema, kwa ufahamu kwamba, katika Roho wa Yesu, hizi zinaweza kuwa, kwa wale wanaozipokea, mbegu za matumaini zilizotajirika.”

Nawatakia heri na Sikukuu njema ya Mtakatifu Yohane Bosco kwenu nyote na Familia nzima ya Kisalesiani, na Maadhimisho mema ya Mwaka wa Jubilei pamoja na miaka 150 ya safari ya kwanza ya kimisionari ya wana wa Don Bosco kwenda Argentina.

Siku Kuu ya Don Bosco
30 Januari 2025, 09:22