Dominika ya IV ya Mwaka C:Tumpokee Kristo aliyekuja kwa ajili yetu!
Na Padre Joseph Herman Luwela - Vatican.
Mpendwa msikilizaji na msomaji Leo ni Dominika ya 4 ya mwaka C. Katika somo la kwanza na Injili tutaona jinsi wajumbe wa Mungu wanavyopata magumu katika utume wao, kwa sababu ya majivuno ya Waisraeli. Katika Injili Kristo anakataliwa kwao na kufukuzwa na ndugu na watu wa nyumbani kwake Nazareti. Basi nawaalikeni nyote tutafakari namna tunavyompokea Kristo au tunavyomkataa katika maisha yetu ya kila siku. Pamoja tutafakari wazo hilia
Ufafanuzi
Wapendwa katika Kristo, Maandiko Matakatifu yanaeleza ukweli huu kwamba Waisraeli waliteuliwa na Mungu kwa malengo maalum. Mojawapo ya sehemu ya hotuba ya Musa kwa Waisraeli inasema, “Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu. Bwana, Mungu wako amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi” (Kum 7:6). Waisraeli walizingatia kwa dhati imani hiyo kwamba wao si kama mataifa mengine. Sababu ya tofauti hiyo ni maagano yaliyofanywa na Mungu kwa Mababu zao. Agano la Kale hutia mkazo kuwa kuteuliwa kwa Waisraeli ni tendo la huruma ya Mungu tu. Siyo kwamba walistahili hivi, bali Mungu alipenda kutimiza uapo wake aliowaapia baba zao (Kum 7:7-9). Hivyo fahari ya kujisikia ni wateule inapigwa vita katika Agano Jipya, kwani uchaguzi wa Mungu unategemea jinsi anavyoita mwenyewe na si matendo ya binadamu (Rum 9:12). Agano Jipya halipingi ukweli huu kwamba Mungu aliwachagua Waisraeli, bali kinachopingwa ni kule kujisikia wateule mno hata wakashindwa kuwapokea wajumbe wa Mungu waliotumwa kwao.
Katika somo la kwanza tumemsikia Mungu akimwita Yeremia kuwa nabii na mjumbe wake kwa mataifa. Kwa kuwa Mungu alijua magumu yatakayompata, alimfariji na kumpa nguvu akamwambia, “Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda;…” habari hii inaonesha kwamba wajumbe waliotumwa na Mungu kwa Waisraeli, watu waliojihesabia haki, waliteseka, wakapigwa na wengine wakauawa. Kutokana na majivuno waliyokuwa nayo Waisraeli wengi iliwapelekea hata kumkataa Masiha waliyemngojea. Ushahidi wa jambo hili tumeusikia katika Injili ya leo. Kristo wanamkataa hata watu wa nyumbani kwake Nazareti, alikolelewa. Hivyo, watu wa Nazareti walishindwa kumtambua Masiha wao kwa sababu hasa ya historia yao ya kujisikia wateule iliyowafanya wamdharau Kristo. Zaidi ya sababu hiyo Wanazareti walidhani kuwa walimfahamu vizuri Yesu tangu utoto wake; waliwafahamu wazazi wake kama ni watu wa kawaida tu katika jamii ile. Hivyo, kule kumfahamu Kristo kama binadam tu, kulikuwa kikwazo kwao, wakashindwa kutambua Umungu wake, wakayadharau mafundusho yake na kumfukuza.
Katika Maisha
Wapendwa, sisi tuliobatizwa tunaitwa wana wa Mungu na Wakristo; yaani wafuasi wa Kristo. Hivyo Kristo ni Bwana wetu. Maandiko Matakatifu yanasema, wanaoongozwa na Roho wa Mungu hao ndiyo wana wa Mungu (Rum 8:14). Hawa ni wale wanaoishi upendo wake. Katika somo la pili tunaambiwa kuwa upendo ni fadhila kuu; nao haujivuni wala haukosi kuwa na adabu. Hivyo tukiongozwa na upendo tutakuwa tunampokea Kristo. Sisi wakristo wa leo hatutofautiani sana na Waisraeli. Tupo wengi tuliyoridhika tu kuitwa wakristo tukidhani tumekwisha mfahamu Kristo. Hali hiyo imewapoteza wengi hasa Wakatoliki.Waisraeli walimtazama Kristo kama binadamu tu, hawakwenda zaidi; na hivyo hawakutegemea lolote jipya kutoka kwake. Leo hii sisi nasi tupo katika mazingira kama hayo. Hivi tunahitaji kumfahamu Kristo taratibu na kwa uvumilivu, ili twende zaidi. Hapa imani inahitajika.
Tusiwe na mazoea tukadharau matakatifu
Ndugu, daima ukilizoea mno jambo fulani unaweza kudhani umelifahamu kutosha. Wengine tunazoea kupokea Ekaristi Takatifu na kuona kitu cha kawaida na pengine tunadharau. Ndiyo maana wapo wenzetu ambao hawakominiki lakini hawaoni kama ni tatizo kwao; wengine kurudi kundini si jambo la msingi kwao. Hali hii ni kumkataa Kristo katika maisha yetu. Wapo wakatoliki wenzetu walioasi kwa sababu ya kuona ni kitu cha kawaida, kwani hawamwoni Kristo tena. Hapa tujitahidi sana kuwafundisha watoto wetu imani na maadili yetu. Sisi tulio bado wakatoliki twendelee kumpokea kwa imani, kuwa Yeye ni Mungu. Basi, tuwasilikilze viongozi wetu wa Kanisa ambao ni wajumbe wa Mungu. Tumpokea Kristo mara kwa mara, ili atusaidie kumfahamu Yeye kweli kwa usahihi. Kwa kuishi ukristo wetu twampokea Kristo. Basi tumwombe Mungu atujalie neema zake ili Kristo aliye nasi tusimzoee mno mpaka kupuuza Umungu wake, na kumfukuzia mbali.