Tafuta

Ushiriki wa Ulimwengu wa Mawasiliano 24-26 Januari 2025. Ushiriki wa Ulimwengu wa Mawasiliano 24-26 Januari 2025.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Jubilei ya Ulimwengu wa Mawasiliano:Tuwe matumaini kwa waliokata tamaa

Kuna haja ya umuhimu wa kuunda mtandao mpana wa kiulimwengu kuanzia waandishi wahabari wa Kanisa katika Kanisa Mahalia na wale watu binafsi ambao wameanzisha vyombo binafsi kwa ajili ya kuinjilisha na vyombo vya habari vya kimataifa.Haya yaliibuka katika mikutano mbali mbali ya Jubilei ya Ulimwengu wa Mawasiliano Ulimwenguni 24-26 Januari na 27-29 Januari 2025.

Na Sarah Pelaji na Angella Rwezaula -Vatican.


Jubilei ya Ulimwengu wa Vyombo vya Mawasiliano Ulimwenguni ilikuwa ya Kwanza kabisa kufungua Jubilei kuu zilizopanga kufanyika mjini Vatican kwa mwaka huu Mtakatifu 2025, uliofunguliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika mkesha wa Noeli tarehe 24 Desemba 2024 kwa kufungua Mlango Mtakatifu wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo inaongozwa na kauli mbiu: “Mahujaji wa matumaini.” Baba Mtakatifu Francisko alitoa mwongozo wa Mwaka Mtakatifu kwa Tamko lake: “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi,”kutoka katika Barua ya Mtakatifu Paulo kwa Warumi(Rm 5:5) na kwamba, maadhimisho haya ni matumaini yanayowawezesha watu waamini wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa maisha na uzima wa milele.

Ulimwengu wa Mawasiliano
Ulimwengu wa Mawasiliano

Ni katika muktadha huo ambapo Wataalamu wa Tasnia ya Vyombo vya Habari Ulimwenguni walifika kuanzia tarehe 24 hadi 26 katika Jubilei yao kuu. Miongoni mwa wawakilishi mbali mbali kutoka katika kurugenzi za Mawasiliano ya Mabaraza ya Maaskofu ni Sarah Pelaji aliyewakilisha Kurugenzi ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania(TEC) na ambaye baada ya kumaliza matukio yote alitembelea Vyombo vya Habari mjini Vatican na kutoa ushuhuda wake  kuhusu siku hizi za neema katika hija yake mjini Vatican kwenye mwaka Mtakatifu na zaidi ameelezea kile kilichomgusa zaidi katika fursa hii. Yafuatayo ni maelezo yake:

Ibada ya Toba
Ibada ya Toba
Ibada ya Toba
Ibada ya Toba

Mahujaji walipofika eneo la Basilika ya Mtakatifu Petro(Peter’s Square) walipitia kwenye lango Kuu lililokuwa limefunguliwa na Papa Fransisko katika Mkesha wa Sikukuu ya Noeli tarehe 24 Desemba 2024 ambapo alifungua Jubilei Kuu. Tukio hili la kupita kwenye mlango Mkuu liligusa mahujaji wengi huku, wengi wakisali na kuomba toba ili kupata rehema kamili kisha mahujaji wakapata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ndani Basilika hiyo kwa sala mbalimbali. Baada ya kufanya hija hiyo ya kiroho mahuaji walekea ukumbi wa Paulo VI, uliopo ndani ya mji wa Vatican ambapo mahujaji walikutana na Baba Mtakatifu Fransisko. Papa alipata wasaa wa kuwakaribisha mahujaji wote, huku akitoa hotuba fupi na kukabidhi hotuba aliyoiandaa kwa Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano na kisha mada mbalimbali zilitolewa.

Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano Dk Paolo Ruffini
Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano Dk Paolo Ruffini
Katika Ukumbi wa Paulo VI
Katika Ukumbi wa Paulo VI

Katika Dominika tarehe 26 Januari 2025 ilifanyika Misa Takatifu katika madhabahu ya Mtakatifu Petro ikiongozwa na Baba Mtakatifu ambapo maelfu ya mahujaji walihudhuria misa hiyo, ikiwa ni kufunga Jubilei ya Ulimwengu huu wa Tasnia ya Mawasiliano, na wakati huo huo, Dominika hiyo ilikuwa ni Dominika ya VI ya ‘Neno la Mungu’ iliyoanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako 2019, kwa lengo ka kuhamasisha zaidi usomaji wa Neno la Mungu. Katika Ibada hiyo waamini 40 kutoka Mataifa mbali mbali walipewa huduma ya Usomaji wa Neno la Mungu huku wakikabidhiwa Biblia Takatifu. Katika kufanya ishara iliyo hai, Baba Mtakatifu pia alitoa zawadi ya Injili ya Luka kwa wale wote waliodhuria maadhimisho hayo.

Kunako tarehe 27 Januari 2025, Baba Mtakatifu pamoja na mikutano mingine alikuwa na Mkutano na Maaskofu Wenyeviti na Wakurugenzi wa Mawasiliano kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulimwenguni. Papa alihutubia mkutano huo akisema kuwa “ Jubilei ni muda wa kuwasilisha tumaini kwa mtu binafsi na kwa wengine.” Na kwamba “mawasiliano ni kusiliza wengine. Kusikiliza historia za wengine na kuwapa matumaini.” Aliwataka waandishi wa habari “waandike habari zenye ukweli , zinazoleta tumaini na kujenga upya ulimwengu uliojeruhiwa.”

Lakini pia mkutano huo ukiwa sehemu ya Jubilei uliokuwa unafungua Mkutano wa Maaskofu Wenyeviti wa Mawasiliano na Wakurugenzi wa Mawasiliano katika Mabaraza ya Maaskofu katoliki Duniani kwa siku mbili tarehe 27-29 Januari, katika Chuo Kikuu cha Kipapa Cha Urbaniano katika ukumbi wa Papa Benedikto wa XVI huku washiriki wakipata maarifa muhimu kutoka kwa wataalam wa mawasiliano wanaotambulika kimataifa, na kubadilishana maoni na uzoefu, kushiriki warsha na mijadala mbalimbali ili kubuni mbinu mbalimbali zitakazoimarisha mawasiliano ya ndani ya Kanisa. Kwa njia hiyo mkutano huo, kama sehemu ya Jubilei ulijikita na baadhi mada ambazo mara nyingi waandishi wa habari wa Kanisa wanakutana nazo.

Kati ya watoa mada katika mkutano huo, kulikuwa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Kwanza katika Makanisa Maalum alisisitiza juu ya “kusikiliza historia za wengine, kujenga urafiki katika mawasiliano, kukuza mtandao mpana wa mawasiliano hasa kwa wale ambao wanaonekana ni wanyonge Zaidi.” Kardinali alisisitiza juu ya kuwa na mawasiliano ya upendo, yenye kuleta matumaini kwa wengine na kwa mtu binafsi. alieleza kwamba “katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi ya kidijitali, kuna haja ya Kanisa kubadili mifumo ya mawasiliano ya sasa ili kuwafikia watu wengi Zaidi.” Zaidi ya hayo, Kardinali Tagle alieleza kuwa “ijapokuwa Kanisa linahudumu katika ulimwengu uliojawa na migogoro, ubaguzi, taarifa potofu, kutopendezwa na vyombo vya habari vya kilimwengu na hata mateso ya waamini lakini halitanyamaza kuendelea kuinjilisha kupitia vyombo vya habari.”

Kwa upande wake Askofu Bernadini Mfumbusa wa Jimbo Katoliki la Kondoa nchini Tanzania ambaye alitoa mada kuhusu kujilinda na taarifa potofu huku akisisitiza kwamba “waandishi wa habari wanalo jukumu la kuchuja habari, kuzihakiki na kutafuta ukweli wa taarifa kabla ya kuisambaza ili kuzuia taarifa potofu zinazoleta mitafaruku katika Kanisa.” Zipo taarifa za uongo zinazosambazwa kwa makusudi, wengine kutokuwa na taarifa sahihi hivyo kusambaza uongo usiokusudiwa na wengine kudhamiria kupotosha taarifa, suala ambalo limeleta mkanganyoko katika jamii,”alisema.

Pia ilitolewa mada kuhusu Akili Mnemba AI(Artifical Inteligence) ambapo “ikitumiwa vizuri inaweza kusaidia katika masuala mbalimbali ya uinjilishaji ijapokuwa bado Kanisa halijapata utaalamu na uelewa mpana juu ya AI.” Kwa njia hiyo Baraza la kipapa la mawasiliano limesisitiza “umuhimu wa kuunda mtandao mpana wa kiulimwengu kuanzia waandishi wahabari wa Kanisa katika Kanisa Mahalia na wale watu binafsi ambao wameanzisha vyombo binafsi kwa ajili ya kuinjilisha na vyombo vya habari vya kimataifa.” Hayo yalielezwa na Dk. Paulo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano.

Ukibonyeza chini hapa utaweza kusikiliza mahojiano kamili:

Mahojiano kati ya Vatican News na Saraha Pelaji

 

30 Januari 2025, 16:53