Kardinali Pierre,Kongamano la Ekaristi kitaifa,Marekani:Mungu hana ajenda anatupenda!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kardinali Christophe Pierre, Balozi wa Vatican nchini Marekani, akiwa katika Kongamano la Kitaifa la Ekaristi Takatifu la Marekani, katika Uwanja wa Lucas Oil, Indianapolis tarehe 17 Julai 2024 alihutubia washiriki zaidi ya 55,000 wakiwa ni maaskofu, mapadre, mashemasi wa daraja na wa kudumu, watawa wa kike na kiume na waamini watu wa Mungu. Akianza hotuba yake alionesha furaha kuwa pamoja nao katika Kongamano hilo na kwamba ni sherehe ya kihistoria kwa nchi hiyo. Alitoa asanta kwa Askofu Andrew Harmon Cozzens wa Jimbo la Minneapolis, kwa kazi yake isiyochoka ya kuongoza Uamsho huu wa Ekaristi, alimshukuru Tim Glemkowski, Afisa Mkuu Mtendaji wa Kongamano la Kitaifa la Ekaristi na washiriki wa timu ya uongozi, na wote ambao wamesaidia kujiandaa kwa Kongamano hilo. Aliomba kwamba bidii yao ya utumishi ipate thawabu ya kukutana na Kristo katika siku hizo zenye kufariji.
Kardinali alieleza alivyokuwa hapo kama mwakilishi binafsi wa Baba Mtakatifu nchini Marekani. Kwa hivyo, kuwa kwake hapo ilikuwa ni njia ya kuelezea ukaribu wa kiroho wa Papa wao na umoja wake na wao katika nchi hiyo. Kama Mtaguso wa Pili wa Vatican unavyofundisha kwamba: “Papa wa Roma, kama mrithi wa Petro, ndiye kanuni ya kudumu na inayoonekana na msingi wa umoja wa maaskofu na waamini.” Kardinali Pierre aliongeza kusema: “Ni zawadi gani hii! Hii ni zawadi iliyoje, kwamba tunaweza kuunganishwa kama Kanisa kupitia Baba yetu Mtakatifu. Wakati huo huo, kile kinachotuleta pamoja katika Kongamano hili - Ekaristi Takatifu - pia ni zawadi kubwa kwa umoja. Kama Mtakatifu Yohane Paulo II alivyosema, “Ekaristi ni sakramenti na chanzo cha umoja wa Kanisa.” Hatuhitaji kutafuta umoja mahali pengine, bali katika Ekaristi.” Kwa kuongezea alisema “Labda sala yetu kuu kwa Kongamano hili la Ekaristi liwe hili: Ili sisi, kama Kanisa, tuweze kukua katika umoja wetu, ili tuwe na matunda zaidi katika utume wetu. Hii ndiyo sala ambayo Yesu alimwomba Baba usiku ule alipoanzisha Ekaristi: “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.” Ili kutambua umoja huu ambao Bwana wetu anatamani tuwe nao, Kardinali alisema “ inaweza kuwa na manufaa kurejea swali la msingi. (Mara nyingi, maswali ya msingi sana ndiyo muhimu zaidi!) Swali ambalo ningependa kutafakari ni hili: “Uamsho wa Ekaristi ni nini”? Na kufanya swali kuwa la kibinafsi zaidi: Tutajuaje kwamba tunapitia uamsho wa Ekaristi?”
Kardinali Pierre akijibu maswali hayo alisema kuwa: “Katika kipindi cha miaka michache iliyopita, tumekuwa sehemu ya juhudi iliyopangwa vizuri sana ya kuelekeza akili na mioyo ya Wakatoliki juu ya uwepo halisi wa Kristo katika Ekaristi. Tumefanya juhudi hii katika parokia zetu, katika majimbo yetu, na sasa katika ngazi ya kitaifa - yote ambayo yamekuwa yakijengwa kwa aina fulani hadi sasa. Katika viwango vyote, tumeona fursa nyingi za kuabudu na kubarikiwa. Kumekuwa na katekesi juu ya Ekaristi na, bila shaka, maandamano. Kwa kuonesha Sakramenti Takatifu kwa ajili ya ibada na kuongeza matendo yetu ya ibada, tumevuta fikira kwa mara nyingine tena kwenye Sakramenti hii kuu ili “kuchochea” imani iliyofanywa upya, ndani ya Wakatoliki wenzetu na sisi wenyewe. Tumevutia hata udadisi wa watu wa imani zingine. Na kuwa wazi kabisa: yote ni nzuri! Lakini kwa kurejea swali la awali: Uamsho wa Ekaristi ni nini? Tunajua kwamba uamsho kama huo, ingawa daima unaambatana na ibada ya kisakramenti, lazima uenee zaidi ya mazoea ya ibada pia.
Tunapo huishwa kiukweli na Ekaristi, basi kukutana kwetu na uwepo halisi wa Kristo katika Sakramenti hutufungua kukutana naye katika maisha yetu yote. Hii inamaanisha kumuona kila mahali tunapokwenda. Inamaanisha kukutana Naye katika maingiliano tuliyo nayo na wengine. Hayupo tu katika familia, marafiki, na jumuiya zetu; lakini pia yumo katika kukutana kwetu na watu ambao tungejiona kuwa tumegawanyika. Hii inaweza kujumuisha watu kutoka tabaka tofauti za kiuchumi au kabila, watu wanaopinga njia yetu ya kufikiri, na watu ambao mtazamo wao unasababishwa na uzoefu ambao ni tofauti sana na wetu. Tunapokutana na watu kama hao - na wakati mantiki ya ushindani ya ulimwengu inatuhimiza kujilinda - Kristo yupo kuwa daraja. Kristo, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote, anataka kuwa daraja kati ya watu ambao ni washiriki wa familia moja ya kibinadamu: watu ambao ni watoto wa Baba yule yule wa mbinguni, na ambao hatima yao ni kuunganishwa katika upendo ndani ya nyumba ile ile ya milele. Ikiwa tunapitia ‘uamsho wa Ekaristi’, basi moja ya ishara itakuwa harakati kubwa zaidi kwa upande wetu kujenga madaraja ya umoja.
Kwa nini kuhusika kwetu na Ekaristi hutusukuma kuelekea umoja? Kwa sababu, tunapoadhimisha Ekaristi, tunapata uzoefu wa Yule aliyejenga daraja la kwanza, ambaye alivuka umbali na kujifanya kuwa mmoja pamoja nasi, na hata tulipotengwa naye. Huyu ndiye aliye pamoja nasi, akijifanya kuwepo katika hali halisi ngumu lakini thabiti ya maisha yetu ya kila siku. Na kwa hivyo, kuamini uwepo halisi wa Kristo sio tu kusema: Katika aina hizi za mkate na divai ni mwili wake, damu, roho, na uungu wake. Bila shaka hiyo ni kweli! Lakini Kristo pia yuko katika kusanyiko la watu wake wanaoamini. Si hivyo tu, bali yuko kwa watu wanaotatizika kuungana Naye kwa sababu ya majeraha, hofu, na dhambi. Tunahitaji kuwa pale pamoja Naye, tukiandamana na watu kama hao, na kuwasaidia waone uwepo halisi wa upendo wa Kristo.
Kuabudu, ni muhimu kwa uhusiano wetu na Kristo - lakini ni muhimu tuichukue kama hiyo: uhusiano. Ikiwa, katika tendo la kuabudu Ekaristi, tungeitazama Sakramenti kama “kitu” cha kustahiki tu, basi tungebaki, kana kwamba, ni “nje.” Kuabudu Kristo ni kuhusiana Naye. Papa Benedikto XVI alieleza kuwa: “Neno la Kilatini la kuabudu ni ad-oratio—kugusana mdomo kwa mdomo, busu, kukumbatia, na hivyo, hatimaye upendo. Kujisalimisha kunakuwa muungano, kwa sababu Yeye tunayenyenyekea kwake ni Upendo. Kwa njia hii utii hupata maana, kwa sababu haulazimishi chochote kutoka nje, bali hutuweka huru ndani kabisa.” Juu ya kuhusiana na Kristo kwa njia hii kwa njia ya kuabudu, tunaweza pia kuhusiana na wengine kwa njia ambayo inaheshimu uwepo wa Mungu ndani yao. Kuabudu kunaenea katika maisha yetu ya kila siku: maisha yetu ya kuhusiana na wengine, njia yetu ya kuona wengine. Tunapohuishwa kwa kweli na Ekaristi - tuseme, kubadilishwa na Ekaristi, hatubaki vile tulivyokuwa. Tunapompokea Kristo, sio tu kwa nje na kwa sehemu, lakini ndani na kikamilifu, ndipo tunaanza kuona tofauti. Tunaona kwa macho ya Kristo; tunaona ukweli kwa macho yake. Tunafikiri kwa njia tofauti, kwa sababu, kama vile Mtakatifu Paulo asemavyo, “tuna akili ya Kristo.” Uamsho wa Ekaristi, basi, lazima uhusishe uwongofu wa kichungaji.
Kwa kukumbuka jinsi ambavyo Papa Francisko alizungumza juu ya uongofu wa kichungaji. Matatizo ambayo utume wetu wa uinjilishaji lazima ukabiliane nayo si matatizo ambayo tunaweza kuyatatua sisi wenyewe. Jinsi ya kukabiliana na usasa, jinsi ya kumpenda mtu anayefikiri tofauti, jinsi ya kuondokana na mgawanyiko, na jinsi ya kukabiliana na mateso: haya sio matatizo na ufumbuzi wa kibinadamu tu. Ni nguvu ya Mungu pekee inayoweza kuponya migawanyiko, kukomboa mateso, na kusema neno la kuokoa kwa wale ambao wametekwa kwa hila. Nguvu ya Mungu hutujia katika Ekaristi. Lakini hatuwezi kuwa mawakala wa nguvu za Mungu ikiwa tunasisitiza kuona sawa, kufikiri sawa, na kudhibiti zawadi za Mungu. Hii ndiyo mbaya zaidi. Tunajifanya kuwa bwana wa mchezo. Kinyume chake tunapaswa tujiachie tuwe na Roho wa Mungu, na kwenda mahali ambapo Roho anapotuongoza. Tuwe waaminifu. Tuwe waaminifu. Sisi, wote kwa sababu, tunaogopa kwenda mahali ambapo Roho anatuongoza. Je, hiyo si kwel.? Aliuliza Swali Kardinali Pierre. Labda hili liwe tunda kuu la uamsho wa Ekaristi. Yaani la kuwa watu waliohuishwa na Roho. Watu wenye uwezo wa kusikiliza sauti ya Roho. Kardinali alikumbusha wakati Papa Francisko alipozungumza kuhusu sinodi, anasema, hatua ya kwanza ni: “ Sikilizaneni ninyi kwa ninyi na msikilize Roho ndani ya mtu tunayemsikiliza.”
Kuwa tunda la uamsho wa Ekaristi. Kardinali Pierre alisisitiza kuwa wote kuomba kwa ajili ya uamsho wa kweli wa Ekaristi. “Uamsho huu na ufungue macho yetu kwa njia ambazo Kristo anaishi na kutenda katika uhalisi mbele yetu, na utusukume kuungana Naye katika kazi Yake.” Kwa njia hiyo aliwatia moyo, wakati wa kuabudu kwao siku hizo, kumruhusu Bwana awafunulie sehemu zozote za upinzani. Kujua nini maana ya upinzani. Tuna kila aina ya upinzani. Tunajua, jinsi ambavyo tungependa, lakini hatufanyi hivyo.” Papa Francisko alizungumza kuhusu suala la kubaki katika eneo letu la faraja la kijizungukia. Na kwamba je wanajua, jinsi ambavyo hata Kanisa la Marekani, linaweza kuwa eneo lao la faraja, sivyo? Kardinali Pierre aliongeza ni sawa hawakubalini naye, lakini alikuwa sawa na maoni yake kwamba wanahitaji muda wa kufikiri juu ya hilo. “Mara nyingi, tunapinga kazi ya Kristo tunapoogopa kuachilia ufahamu wetu wenyewe na udhibiti na kuogopa kuruhusu hekima na uwezo Wake kuongoza. Lakini Ekaristi ni zawadi kutoka kwa Mungu.” “Hatuifanyi Ekaristi, bali tunaipokea. Lakini kwa kusalimisha utegemezi wetu juu ya uhakika wetu wenyewe, mipango yetu wenyewe, ajenda zetu… Na hivi tunajua tuna ajenda zote, na sisi ni werevu vya kutosha kufuata ajenda zetu, na kujihakikishia kwamba ajenda yetu ni bora kuliko ajenda ya Mungu.” Hata hivyo Mungu hana ajenda. Mungu anatupenda! Naye anatuongoza kwa Upendo. Sio kutudanganya. Sio kufikia ajenda yake. Yeye ndiye pekee anayeweza kutuongoza kwenye maisha mapya. Kwa kumfuata, tunaweza kuwa mitume wa kweli wa Ufalme Wake.”