Kumbukizi ya Miaka Mitatu Ya Kifo Cha Rais Dkt. John Pombe Magufuli
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Watanzania wanaendelea kumkumbuka na kumwombea Hayati Dr. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021, akiwa na umri wa miaka 61 kwa: Uzalendo, Uchapakazi, Upendo, Uaminifu, Kujitoa na kujisadaka bila ya kujibakiza; Uvumilivu, Usikivu na Ucheshi; Upole na Huruma kutoka kwake. Kama sehemu ya kumbukizi ya miaka mitatu tangu Rais Magufuli afariki dunia, Dominika tarehe 17 Machi 2024, imeadhimishwa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea, Hayati Magufuli kwenye Parokia ya Mtakatifu Yohane Maria Muzeyi, Chato, Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameshiriki ibada hii ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. "Kama alikuwa na mapungufu Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo amsamehe na kumkaribisha katika ufalme wa mbinguni maana huenda yeye kama binadamu kuna mahali alikosea" amesema Makamu Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge Ngara, Padri Ovan Mwenge wakati akiongoza ibada hiyo. "Siyo kazi yetu kuhukumu, kazi yetu ni kumwombea, kama kuna watu hawaamini katika kumwombea marehemu, wabaki hivyo hivyo na kama kuna watu wanaamini basi siku moja tutakutana" amesema Padri Mwenge.
Akitoa salamu kwenye Misa hiyo, Dkt. Biteko amesema Hayati Dkt. Magufuli alikuwa na ndoto ya kuwaunganisha watanzania kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo na sasa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendeleza miradi hiyo. "Dkt. Samia ameendeleza ujenzi wa bwawa la umeme la Mwalimu Julius K. Nyerere, Reli ya kisasa ambayo majaribio yamefanyika kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro pamoja na ujenzi wa daraja la Kigongo- Busisi ambalo limefikia zaidi ya asilimia 80 likiunganisha mikoa ya Geita na Mwanza, nataka niwahakikishie hakuna kitakachosimama" amesema Dkt. Biteko.
"Rais wetu Dkt. Samia aliposema “Kazi Iendelee” alikusudia kuyaendeleza yale yote yaliyobuniwa na Hayati Dkt. Magufuli na nataka niwahakikishie kwamba yote aliyoyaanzisha Rais wetu atayaendeleza kwa kasi kubwa ili watanzania wayapate kama yalivyokusudiwa kwa Hayati Magufuli" amesema Dkt. Biteko. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na wanafamilia wakiongozwa na mke wa Hayati Dkt. Magufuli Mama Janeth Magufuli, wananchi, viongozi wa dini na Serikali. Tarehe 5 Septemba 2018, Hayati Rais John Pombe Magufuli aliwahutubia watu wa mkoa wa Mara na akagusia mambo mbalimbali yenye masilahi mapana ya Taifa, yakiwemo utajiri wa Tanzania na matumizi mabaya ya fedha ya umma na rasilimali za nchi yanayoendelea kuwatumbukiza watanzania katika dimbwi la umaskini.