Afrika Kusini:Baada ya watawa 3 kuuawa,Padre mwingine apigwa risasi kanisani
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Padre mmoja wa Kanisa Katoliki aliuawa tarehe 13 Machi 2024 katika Kanisa moja nchini Afrika Kusini alipokuwa akijiandaa kuadhimisha Misa Takatifu. Ni Padre William Banda, wa Jumuiya ya Mtakatifu Patrick kwa ajili ya Utume wa Kigeni (Mababa wa Kiltegan), aliyeuawa kwa kupigwa risasi katika Kanisa Kuu la Tzaneen, takriban kilomita 350 kaskazini-mashariki mwa Pretoria kwa mujibu wa Shirika la Habari za Kimisionari la Fides.
Ni baada ya sala ya Rosari
Ilikuwa saa 1.45 asubuhi na Padre mwenye asili ya Zambia alikuwa akiongoza rozari Takatifu inayotangulia Misa ya saa 2.00 kamili Asubuhi. Waamini waliona mtu wasiyemfahamu akiingia kanisani. Alikuwa ni mwafrika aliyevalia vizuri sana alimwendea padri na kumsogelea kuketi karibu naye. Mara baada ya kumalizika sala kwa maombi hayo, Padre Banda alielekea kwenye sakramenti ili kuvaa nguo zake za kuadhimisha ibada ya misa. Yule mgeni alimsogelea na, Padre alipokaribia kuingia, sakrestia akachomoa bunduki mfukoni mwake na kumpiga risasi kisogoni. Kisha akaelekea njia ya kutokea kanisani lakini mara alipofika kwenye kizingiti akageuka nyuma tena, akamsogelea padre akaanguka chini na kufyatua risasi ya pili kichwani. Kisha akaingia kwenye gari lililokuwa likimsubiri na kuondoka kwa kasi.
Watawa wengine watatu wa Kiorthodox wauawa huko Pretoria
Mauaji hayo yalifanyika siku moja baada ya kuchomwa visu watawa watatu wa Kiorthodox, raia wa Misri, tarehe 12 Machi 2024 katika monasteri ya Mtakatifu Marco Mtume na Mtakatifu Samweli Muungamishi huko Cullinan, yapata kilomita 30 mashariki mwa Pretoria. Katika taarifa, ya Kanisa la Kiothodoksi la Coptiki linasema kwamba watawa waliouawa kwa mashambulizi ya visu walikuwa Padre Takla El-Samouili, wa jimbo; Ndugu Youstos Ava-Markos; na Mina Ava-Markostre. Hadi sasa bado hakuna jipya katika uchunguzi huo, ambao pia utalazimika kufafanua nia ya mauaji hayo mara tatu!